Hong Kong. Shirika la Ndege la India (Air India) limesema ndege yake namba AI315 imelazimika kurejea jijini Hong Kong baada ya kukutana na changamoto ya hali ya hewa isiyo rafiki.
Shirika la Habari la Associated Press limeripoti leo Jumatatu Juni 16, 2025, kuwa ndege hiyo aina ya Boeing 787 Dreamliner iliyokuwa ikisafirisha abiria kutoka Hong Kong kwenda New Delhi nchini India imelazimika kurejea Hong Kong leo saa 7 mchana (Saa za Hong Kong).
Mamlaka ya usimamizi wa viwanja vya ndege Hong Kong zimesema ndege hiyo ambayo ilitua Hong Kong salama, ilifanyiwa ukaguzi na kuruhusiwa kubeba abiria kwenda India hata hivyo, lengo hilo halikufanikiwa baada ya kukutana na changamoto angani.
“Imelazimika kurejea na kutua Hong Kong kwa sababu za kiusalama,” imeeleza taarifa ya mamlaka hiyo.
Tayari shirika hilo limetoa taarifa ya kuomba radhi na kuwa limeitisha msaada wa kupata ndege mbadala kwa ajili ya kuwasafirisha abiria wake kwenda nchini India.
Tukio hilo limetokea zikiwa zimepita siku nne tangu ndege nyingine ya shirika hilo iliyokuwa ikitokea kwenye uwanja wa Ahmedabad nchini India kwenda London, Uingereza kuanguka dakika chache baada ya kuacha njia ya kurukia kisha kugonga jengo la ‘hosteli’ za chuo cha afya kilichoko Ahmedabad Kaskazini Mashariki mwa India.
Katika ajali hiyo, ndege ya Air India ilisababisha vifo vya watu 270 wakiwemo waliokuwemo 241 na wengine 29 waliofariki baada ya jengo la hosteli kugongwa.
Hata hivyo, kuna abiria mmoja wa ndege hiyo ambaye ni raia wa Uingereza mwenye asili ya India, Vishwashkumar Ramesh alinusurika katika ajli hiyo na hali yake imeanza kuimarika hospitalini anakopatiwa matibabu.
Ramesh alipoulizwa namna gani alinusurika katika ajali hiyo, amesema baada ya ajali hiyo kutokea aliruka kupitia mlango wa dharura uliopo nyuma ya ndege hiyo kisha wasamalia wema kumchukua na kumpeleka ilipokuwa Ambulance.