NHC: Hakutakuwa na maghorofa chakavu Kariakoo miaka mitatu ijayo

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Hamad Abdallah amesema miaka mitatu ijayo eneo la Kariakoo, jijini Dar Salaam halitakuwa na maghorofa chakavu.

Amesema hatua hiyo linatokana na mikakati wa shirika hilo na kwamba sasa kuna miradi 16 inaendelea kutekelezwa katika eneo hilo.

Mkurugenzi huyo ametoa kauli hiyo leo Juni 16,2025 baada ya ziara ya wahariri katika baadhi ya miradi ya shirika hilo.

Amesema katika miradi hiyo wanajenga nyumba za makazi pamoja na maeneo ya biashara na majengo ambapo yatakuwa  na ghorofa kuanzia 10 hadi 15.


“Tuna miradi ya uboreshaji miji, tunavunja majengo chakavu na kujenga ya kisasa kwa sababu ardhi inaweza kuwa na thamani zaidi kuliko jengo lililopo.

“Mfano hapa (Morocco Square) kulikuwa na majengo matatu ambayo kwa mwezi yalikuwa yanatuingizia Sh3 milioni, lakini sasa baada ya kujenga jengo la kisasa tunaingiza Sh600 milioni kwa mwezi” amesema.

Katika ziara hiyo, wahariri walitembelea mradi wa Kawe 711, Golden  Premier Residence, Samia Housing Scheme na Morocco Square.

Akizungumzia mradi wa Samia Housing Scheme, amesema umepewa jina hilo kutokana na hatua ya     Rais Samia Suluhu Hassan kukwamua miradi ya shirika hilo uliyosimama kwa miaka minane.

“Mradi wa Samia utajengwa nyumba 5,000. Asilimia 50 ya nyumba hizo zitajengwa Dar es Salaam kutokana na uhitaji, asilimia 30 zitajengwa Dodoma na asilimia 20 kwenye maeneo yenye soko na uhitaji,” amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile ameupongeza uongozi wa shirika hilo kwa kuikwamua miradi uliyosimama ujenzi kwa miaka minane iliyopita.

Related Posts