Unguja. Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman amesema heshima ya utambuzi wa haki za nchi na wananchi ni kuzalisha vyanzo vya nafasi za ajira na kutoa huduma stahiki kwao bila ubaguzi.
Amesema ili kupatikana kwa heshima hiyo, chama chake kimeamua kusimamia msimamo wake wa kuinusuru Zanzibar na kuleta maisha ya nafuu kwa watu wake.
Hayo yameelezwa leo Juni 16, 2025 katika taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Kitengo cha Habari katika Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, akiwa katika ziara ya kikazi nchini Uingereza.
Othman ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, ameyasema hayo wakati akizungumza na wanachama na wafuasi wa chama hicho wanaoishi nchini Uingereza katika mkutano wa ndani uliofanyika Mjini Coventry.
Amesema Zanzibar ina rasilimali na vyanzo vingi vya kuiingiza nchi katika mafanikio ya kiuchumi, hata hivyo havionekani kwa sababu ya kukosa uongozi wenye wenye maono.
“Nchi yetu ina fursa nyingi, bali tunahitaji kuwa na misingi mizuri ya kuongoza nchi ili tuweze kunufaika nayo. Nami niwaombe tuendelee kuungana kuyafanikisha hayo,” imesema taarifa hiyo.
Mjumbe wa Kamati ya Wazee wa Diaspora ya Kaskazini mwa Uingereza, Abdallah Alawi Said amesema bado wanaendelea kuziunga mkono jitihada zote zinazongozwa na Othman na chama chake katika kuinusuru Zanzibar.
Pia, amesema licha ya mapito ambayo Zanzibar imeyapitia kila msimu wa uchaguzi, kuna haja ya kusimama kwa pamoja na ACT Wazalendo ili kuinusuru nchi yao.
Akisoma risala kwa niaba ya Diaspora Uingereza, Time Seif Sharif amesema suala la amani, kutenda haki na kusimamia sheria siyo suala la kisiasa tu, bali ni la mustakbali wa taifa kwa ujumla hivyo ni vyema kuilinda tunu hiyo.