Rungwe. Ridhaa ya wanunuzi wa zao la parachichi wilayani Rungwe Mkoa wa Mbeya kukatwa Sh200 kumechangia kuanza ujenzi wa Shule ya Sekondari Avocado katika Kijiji cha Isajilo, Kata ya Mpuguso wilayani humo.
Hatua hiyo imetajwa ni matokeo ya mkutano wa wadau wa zao hilo, uliofanyika mwanzoni mwa mwaka huu, ambapo Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk Juma Homera alikuwa mgeni rasmi.
Katika mkutano huo Homera alitoa ombi la kuwataka wanunuzi kukatwa Sh200 za mauzo kwa ajili ya kuchangia ujenzi huo jambo ambalo lilikubaliwa.
Imeelezwa kuwa katika kata hiyo, wanafunzi wakichaguliwa kujiunga kidato cha kwanza wanalazimika kutembea umbali wa kilomita saba kufuata elimu hali inayosababisha baadhi yao kuacha masomo na kukimbilia mitaani au kufanya vibarua vya kulima.
Hayo yamesemwa leo Jumatatu Juni 16, 2025 na Diwani Kata ya Mpuguso, Japhet Mwakagugu baada ya Homera kuweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa shule hiyo.
“Mkuu wa Mkoa tunashukuru kwa ombi la maono yako uliyotoa kwenye kikao cha wanunuzi wa zao la parachichi, watoto wengi wameacha masomo kwa sababu mbalimbali hususan kukwepa kutembea umbali mrefu kufuata elimu, utoro na mazingira hatarishi ya njiani,” amesema.
Mwakagugu amesema kuna wakati wazazi hulazimika kudamka saa 10 alfajiri kwa ajili ya kuwasindikiza wanafunzi kuwahi masomo na wasidhulike na watu wasio waadilifu.
“Ujenzi huu ukikamilika utaondoa adha kwa wanafunzi kupata elimu sehemu salama na kutotembea umbali mrefu na kuongeza chachu ya kufanya vizuri kitaaluma,” amesema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Rungwe, Mpokigwa Mwankuga amesema baada ya wanunuzi wa parachichi kuridhia ombi la Homera, kama halmashauri walianza kusaka eneo kwa ajili ya utekelezaji na kutenga ekari sita.
“Tumekusanya Sh117 milioni, kati ya hizo Sh50 milioni, zimetumika kuanza ujenzi wa shule hiyo lakini Sh50 milioni, zimetumika ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa Shule ya Msingi Masebe na Sh17 milioni, kuotesha vitalu vya miche ya parachichi na kutoa kwa wananchi,” amesema.
Homera amesema ujenzi wa shule hiyo ni sehemu ya mikakati ya mkoa kushirikisha wadau wa sekta ya kilimo kuchangia kulingana na mazao wanayozalisha.
Amesema shule hiyo wamependekeza kuwa ya wasichana na wavulana ni baada ya kupata maoni ya wananchi kulingana na changamoto za umbali na kadhia wanazofanyiwa wanafunzi wakifuata elimu.
“Awali tumeanza ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Pareto Wilaya ya Mbeya vijijini, lakini Wilaya ya Chunya Kata ya Lupa tumejenga sekondari inayotokana na zao la tumbaku na Wilaya ya Kyela kuna Shule ya Wasichana ya Kakao, lengo la Serikali ni kuhakikisha mazao husika yanakuwa na mchango katika sekta ya elimu,” amesema.
Amesema uwekezaji huo ni busara za wazee wa Mkoa wa Mbeya, lakini amebaini changamoto ya miundombinu ya barabara kuelekea katika shule hiyo ambapo tayari ametoa maelekezo.
Katika hatua nyingine ameagiza halmashauri kuharakisha kukamilisha ujenzi huo ili ifikapo Januari 2026, wanafunzi waanze kupokewa.
Mkazi wa kijiji cha Isanilo, Joyce Kafulila amesema walipopata taarifa za Serikali kujenga sekondari walifurahishwa kwa kucheza ngoma kwenye ofisi ya kijiji.
“Kijiji hiki kinaongoza kwa watoto kuacha shule, kutokana na mazingira mabaya ya umbali na badala yake kujificha vichakani na kufanya vitendo vibaya,” amesema.
Amesema wanaishukuru Serikali kwa hatua hiyo na kwamba watashiriki kikamilifu kuwekeza nguvu kazi ili kukamilisha ujenzi huo.
Mnunuzi wa zao la parachichi, Joel Mwakitalima amesema wamefikia hatua hiyo baada ya kuona nia njema ya Serikali kunusuru kizazi cha sasa na kijacho kupata elimu.