Moshi. Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Hashimu Rungwe amelazwa hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini, KCMC baada ya kupata changamoto za kiafya.
Rungwe ambaye alikuwa katika ziara ya operesheni ya C4C mkoani Kilimanjaro, alipata changamoto hiyo ya afya Juni 14, 2025 na kuwahishwa katika Hospitali ya KCMC kwa ajili ya uchunguzi wa kidaktari.
Licha ya Rungwe kutajwa kuwepo kwenye ziara hiyo ya kikazi mkoani Kilimanjaro, hakuonekana katika mikutano ya hadhara ambayo ilifanyika Mji mdogo wa Himo na viwanja vya Stendi Kuu ya Mabasi Moshi Mjini.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya kiongozi huyo, Ofisa Uhusiano Hospitali ya KCMC, Gabriel Chiseo amesema Rungwe alifikishwa hospitalini hapo juzi Juni 14, huku changamoto kubwa ikionekana kuwa homa iliyosababishwa na uchovu.
“Juzi tulimpokea Hashimu Rungwe kwenye idara yetu ya magonjwa ya dharura na baadaye tukaenda kumlaza wodi ya watu mashuhuri, moja ya changamoto iliyokuwa ikimsumbua ni uchovu kulingana na shughuli zake,” amesema Chiseo.
Ameongeza kuwa, “Vipimo vyetu vya awali vimeonyesha kwa sababu ya uchovu wa shughuli zake ilisababisha kupata homa, hivyo madaktari wetu wataalamu wa afya walishauri apate muda wa kutosha kupumzika, wakifuatilia afya yake na kuendelea na vipimo zaidi.”
Chiseo amesema kwa sasa kiongozi huyo afya yake imeimarika baada ya kupewa huduma za awali za matibabu na muda wote wowote anaweza akaruhusiwa kutoka hospitali.
“Mpaka leo asubuhi ameimarika sana na wakati wowote tunaweza kumruhusu na kuendelea na shughuli zake, lakini madaktari wamemshauri namna ya kufanya shughuli zake kwa sababu ya afya yake,” amesema Chiseo.
Akizungumza hospitalini hapo, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar, Issa Abbas Hussein amesema hali ya kiongozi huyo ilibadilika na kuonekana amechoka walipokuwa wakitoka Wilaya ya Mwanga kwenda Wilaya ya Same kwa ajili ya kuhitimisha ziara yao eneo la Hedaru.
Amesema walipofika kutokana na kubadilika kwa afya yake, walimpeleka kituo cha afya Hedaru na ndipo alipewa rufaa kwenda Hospitali ya KCMC.
“Tulikuwa njiani kuelekea Hedaru mkutano wa mwisho ili turudi Dar es Salaam kwa mapumziko sasa hapo ndio tulipata taarifa Mzee anaonekana amechoka sana, hivyo tukasema tumpeleke hospitali hapa Hedaru kwa uangalizi na pale wakasema hapana na alivyochoka wakasema apelekwe KCMC, hivyo tulikuja naye hapa,” amesema.
Aliongeza kuwa, “Baadaye alipimwa na kwa sababu ni mtu wa presha na sukari, akaonekana presha imepanda kutokana na mitikisiko ya safari, akapewa dawa za kushusha presha na sukari na sasa yupo vizuri.”
Amesema kwa sasa anaendelea vizuri kutokana na huduma nzuri alizozipata hospitalini hapo na sasa hivi wanasubiri majibu ya mwisho ya daktari.