Makombora yaliyorushwa na Israel yamelenga zilipo ofisi za makao makuu ya Televisheni ya Taifa ya Iran (IRIB) yaliyopo jijini Tehran nchini humo.
Al Jazeera imeripoti leo Juni 16, 2025, kuwa Jeshi la Israel (IDF) kabla ya kutekeleza shambulizi hilo lilitoa onyo likiamuru raia kuondoka maeneo yenye miundombinu ya umma.
Shambulio hilo lilikatiza matangazo kwa muda, ambapo mtangazaji aliondoka hewani katikati ya kipindi huku studio ikifunikwa na vumbi na moshi uliotokana na shambulio hilo. IRIB Ilionyesha jengo hilo likiwa linawaka moto baadaye.

Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz amethibitisha jeshi lake kuhusika kutekeleza shambilio kwenye kituo hicho baada ya wakazi wa eneo hilo kuhamishwa kwa wingi.
Awali, IDF ilikuwa imetoa wito kwa raia kuondoka katika baadhi ya maeneo ya wilaya ya tatu ya Tehran, ambako studio hiyo ya televisheni inapatikana.
Televisheni ya taifa ilirusha matangazo ya moja kwa moja yakionyesha jengo la vioo la makao yake makuu likiteketea kwa moto, pamoja na moshi mkubwa. Mwandishi wa habari wa kituo hicho alisema juhudi za kuzima moto zilikuwa zinaendelea, na akaongeza kuwa mabomu manne yaliligonga jengo hilo. Alisema bado idadi ya waliokufa haijapatikana.
Mkuu wa IRIB, Peyman Jebelli amesema vita hiyo iliyoanzishwa na Israel haitoathiri azma ya kituo hicho kuuhabarisha umma kuhusu mwenendo wa makombora hayo ya Israel.
Awali, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu alisema kuwa Israel imepata udhibiti wa anga ya Tehran, hatua aliyosema ni mabadiliko katika kampeni nzima.
Aliongeza kuwa Israel ipo njiani kulimaliza kabisa programu ya nyuklia ya Iran na uwezo wake wa makombora ya masafa marefu.
Mapema leo asubuhi Israel ilitangaza kuwa mashambulizi ya Iran yameua raia wanane katika kipindi cha saa 24 zilizopita nchini humo.
Kwa upande wa mamlaka nchini Iran zilisema Jumapili jioni kuwa raia zaidi ya 224 wameuawa kutokana na mashambulizi ya Israel nchini humo, wakiwemo maofisa 17 wa jeshi la nchi hiyo.
Mashambulizi hayo ya hivi karibuni yametokea wakati viongozi wa kimataifa wakiwasili nchini Canada kwa ajili ya mkutano wa kilele wa G7, ambapo miongoni mwa hoja zitakazojadiliwa ni jinsi ya kumaliza mzozo huo.