Dodoma. Wabunge wameitaka Serikali kuwekeza katika utafiti, teknolojia na elimu kwani ndiyo njie pekee ya kuwakomboa wananchi kiuchumi.
Pia, wameitaka kuweka adhabu kwa raia wa kigeni watakaokiuka masharti ya kanuni zilizowekwa katika shughuli za biashara, ikiwemo kuwafutia vibali vya kazi na viza wanapothibitika.
Wabunge wamesema hayo leo Jumatatu, Juni 16, 2025 katika siku ya kwanza kati ya saba za kujadili hali ya uchumi wa Taifa kwa mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka wa fedha 2025/2026 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Katika michango yao, wabunge hao wamepongeza namna ambavyo Serikali imepunguza kodi kwa baadhi ya maeneo ikiwemo waendesha bodaboda.
Mbunge wa kuteuliwa Shamsi Vuai Nahodha amesema bila kuwekeza katika elimu maendeleo ya nchi yatakuwa ndoto.
Nahodha ambaye ni Waziri Kiongozi mstaafu wa Zanzibar, amesema Edward Lowasa akiwa Waziri Mkuu alitaja vipaumbele vitatu ambayo ni elimu, elimu na elimu.
Lowassa alikuwa Waziri Mkuu kuanzia Desemba 30, 2005 hadi Februari 7, 2008 katika utawala wa awamu ya nne ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete. Alifariki dunia Februari 10, 2024.
Katika mchango wake bungeni, Nahodha amesema Mzee Lowassa katika sekta ya elimu na teknolojia aliweka nguvu nyingi katika kuhakikisha sekta hiyo inasonga mbele kwa kasi nchini Tanzania.
Akiwa Waziri Mkuu katika awamu ya kwanza ya Serikali ya awamu ya nne, Lowasa alisimamia ujenzi wa shule za sekondari kila kata shule ambazo zimetajwa kuwa mkombozi wa elimu kwa nchi nzima.
“Lowassa alisema akipewa nafasi ya kutaja vipaumbele vikuu vitatu vya mipango ya maendeleo ya taifa basi atataja kipaumbele cha kwanza elimu, cha pili elimu na cha tatu kitakuwa elimu kwani elimu inapaswa kuwa kipaumbele cha kwanza kwa mustakabali wa Taifa letu,” amesema Nahodha.
Amesema Taifa lolote linalotaka kujikomboa na kuondokana na umasikini, halina budi kuwekeza katika elimu ili wananchi wake waweze kuelimika.
Kwa upande mwingine, ameitaka Serikali kuwekeza katika Chuo Kikuu cha Nelson Mandela kwenye ujenzi wa mabweni na maabara kwani kimekuwa na sifa nzuri ya kuzalisha wataalamu lakini miundombinu yake imechoka.
Mbunge wa Kuteliwa Dk Leonard Chamulilo amesema ni muhimu kuwa na vipaumbele viwili ambavyo ni elimu na afya, kwa kuwa ndivyo vinagusa maisha ya kila siku kwa wananchi wa hali ya chini.
Dk Chamulilo amesema kwa sasa bajeti za Serikali zinatakiwa kulenga utoaji wa elimu kwa wananchi na hasa kundi la vijana ili kuwafanya wawe na ujuzi wa kiushindani.
Eneo la utafiti limechangiwa na wabunge wengi. Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospiter Muhongo amesema ili Tanzania ifikie malengo ya kiuchumi ni lazima ikubali kuwekeza katika elimu na hasa kwenye utafiti na ubunifu na isipofanya hivyo itaendelea kubaki nyuma.
Profesa Muhongo amesema kuna ulazima mkubwa kwa Serikali kutenga fedha kati ya asilimia moja hadi mbili ya bajeti, ili zielekezwe kwenye utafiti kwani kiasi kinachotengwa kwa sasa ni kidogo hakiwezi kuwafikisha watafiti mahali panapotakiwa.
Waziri huyo wa zamani wa nishati na madini amesema fedha zilizotengwa zinaonekana kuwa ni nyingi lakini kama zingegawanywa kwa Watanzania, kila mmoja ametengewa dola 306 (sawa na Sh76,500) kiwango alichosema ni kidogo ukilinganisha na nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mbunge mwingine wa Kuteuliwa, Profesa Shukrani Manya amesema iwe lazima kutenga fedha za kuendelea kufanya utafiti katika shughuli zote zinazohusu maendeleo akisema bila utafiti Tanzania haiwezi ‘kutoboa’.
Profesa Manya amesema ni wakati sasa kwa Watanzania kuwa wamiliki wakubwa wa rasilimali zao kuliko inavyofanyika kwa sasa ikiwemo maeneo ya uchimbaji mdogo ambako sheria inataka leseni zimilikiwe na wazawa lakini jambo la ajabu wanaomiliki ni wageni.
“Hali iko hivyo hata ukienda Kariakoo na maeneo mengine ambayo yamejaza wageni, hivyo tunaposema tunamiliki uchumi siyo kweli, haiendani na hali halisi ilivyo hasa huko vijijini,” amesema Profesa Manya aliyewahi kuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini.
Amesema mara nyingi Serikali inaweka bajeti lakini inakuwa kinyume hivyo akataka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, washirikiane na Wizara ya Kazi na Ajira ili kuwadhibiti wageni katika kazi ambazo Watanzania wanaweza kuzifanya.
Katika hatua nyingine mbunge huyo ameomba Serikali iweke mkakati miradi mikubwa ambayo inasimamiwa na wageni ili Watanzania wanaofanya kazi huo wawe wanapata ujuzi ambao mwishowe wawe wataalamu kwa kuwasaidia wengine.
Naye Mbunge wa Vunjo, Dk Charles Kimei amesema katika kipindi hiki ndicho utafiti unatakiwa zaidi kuliko wakati mwingine kama Serikali inataka kuufikia uchumi unaolengwa.
Dk Kimei aliyewahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya CRDB amezungumzia suala mikopo kwamba mabenki yanawaumiza wananchi kwani wanawakopesha kwa riba kubwa licha ya ahueni wanayopewa kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Mtaalamu huyo katika masuala ya fedha ameshangazwa na mikopo kuendelea kuwa katika viwango vya juu vya riba na wakati mwingine hawakopeshi, wakati anatambua kuwa BoT inatoa nafasi kubwa ya watu kukopeshwa.
Naye Mbunge wa Kalenga, Jackson Kiswaga amesema utafiti unaofanyika unapaswa kulenga katika matumizi bora ya ardhi eneo alilodai Serikali haijafanya vizuri kama inavyotakiwa.
Kiswaga ametaka kuwe na mkakati madhubuti wa kuwepo kwa akiba ya ardhi ambayo itakuwa kwenye mfumo ili anapoingia mgeni kutoka nje akitaka kuwekeza apewe taarifa wapi anatakiwa kuwekeza.
Hata hivyo, amesema inashangazwa kuona Watanzania wengi hawana elimu ya kulipa kodi, hivyo ameshauri kuwepo na elimu lakini ulazima kwa watu wenye sifa za kulipa kodi ili wafanye hivyo kwa kuwa bila ya kufanya hivyo hakuna namna ya kujikomboa.
Hoja ya Kiswaga iliungwa mkono na Mbunge wa Moshi Vijiji, Profesa Patrick Ndakidemi aliyetaka suala la kodi liwekewe uzito wake isiwe hiyari kama Tanzania inataka maendeleo kwa watu wake.
Profesa Ndakidemi alizungumzia taarifa za uchumi kwamba zipo katika makaratasi lakini kwenye uhalisia haiko hivyo, kwani wananchi wa vijijini wanaumia na maisha ni magumu.
Amehoji ni kwa nini uchumi wa Watanzania bado uko chini licha ya makaratasi kutaja vinginevyo, hivyo anaona ipo haja kuwekeza katika sekta ambazo zinawagusa moja kwa moja wananchi wa hali ya chini ikiwemo kilimo.
Hoja ya Profesa Ndakidemi iliungwa mkono pia na Mbunge wa Bahi Keneth Nollo aliyetaka mkakati uwekwe katika kuwaondoa wananchi kwenye jembe la mkono la kuwapeleka katika kilimo cha kutumia jembe la ng’ombe au matrekta na umwagiliaji.
Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Bunge ya Bajeti, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Oran Njeza amesema amesema Serikali imekusudia kuweka mazingira ya ufanyaji biashara baina ya wazawa na wageni kwa kufanya marekebisho kwenye Sheria ya utoaji wa Leseni za Biashara, Sura 101.
Njeza amesema marekebisho hayo yanalenga kumpa mamlaka waziri mwenye dhamana ya masuala ya biashara kuainisha shughuli za kibiashara ambazo hazipaswi kufanywa na wageni.
Ametaja hatua hiyo inalenga kuondoa kero iliyopo nchini ambapo wafanyabiashara wageni hufanya biashara za jumla, rejareja na uchuuzi ambazo ni maalumu kwa wazawa.
Katika hatua nyingine, amesema wameishauri Serikali kushughulikia suala la urejeshaji ukusanyaji wa mapato kwa Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (Tawa), Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA).
Ametaja sababu hizo ni hali ya ukwasi wa taasisi hizo ili ziweze kutekeleza majukumu yake kikamilifu kwenye sekta ya utalii na endapo kiwango kinachobakishwa kinaweza kukidhi mahitaji ya Taasisi kujiendesha kwa misingi ya kibiashara na kwa ufanisi.
Kama una maoni kuhusu habari hii tuandikie kupitia Whatsapp 0765864917.