:::::::
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ametoa wito kwa wakuu wa mikoa na wilaya nchini kuhakikisha wanaendelea kuhamasisha wananchi kutumia huduma ya kisheria ya Mama Samia ili iwasaidie kutatua changamoto zao za kisheria.
Amesema kuwa juhudi za utoaji haki haziwezi kufikiwa na Serikali pekee bali zinahitaji ushirikiano wa dhati kutoka kwa kila mmoja ikiwemo viongozi, wazazi, jamii, taasisi za dini, mashirika ya kiraia na wananchi kwa ujumla.
Amesema hayo leo Jumatatu (Juni 16, 2025) alipomwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia katika Mkoa wa Dar es Salaam iliyofanyika kwenye viwanja vya Maturubai Mbagala jijini Dar es Salaam.