Unguja. Sekta saba ikiwemo uvuvi, sanaa, ufugaji, utalii na elimu zinatarajiwa kushiriki katika Tamasha la Kizimkazi ili kutoa mafunzo kwa kuwajengea uwezo wananchi katika utafutaji na matumizi ya rasilimali zinazopatikana katika sekta hizo.
Imeelezwa kuwa mafunzo yanayotolewa katika tamasha hilo yamekuwa sababu mojawapo ya kuwasaidia wanajamii na kunufaika na tamasha hilo baada ya kumalizika.
Hayo yameelezwa leo Juni 16, 2025 na mwenyekiti wa tamasha hilo, Mahfoudh Said Omar wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari, Kusini Unguja.
“Tamasha hili litaanza kwa mafunzo maalumu kwa sekta saba ili kuwajengea uwezo wananchi katika kutafuta rasilimali na kukuza uchumi wao kupitia sekta hizo,” amesema Mahfoudh.
Mwenyekiti huyo amesema tamasha hilo litafanyika kwa siku nane kuanzia Julai 19 hadi Julai 20, 2025 katika Uwanja wa Sports Suluhu Academy, likiwa na kaulimbiu ya “Kizimkazi Kumenoga”.
“Katika tamasha hili, litaangazia kwa kina utajiri wa rasilimali ya bahari, utamaduni wa kipekee wa wakazi wa Kusini na sanaa mbalimbali zinazotambulisha eneo hilo ikiwa lengo ni kuutangaza mkoa huo kiutalii kupitia vivutio vilivyopo,” amesema.
Amesema lengo la kufanya hivyo ni kuonyesha uzuri unaopatikana katika mkoa huo ili kuwavutia watalii wa ndani na nje kutembelea maeneo hayo ya asili na utamaduni.
Ameeleza kuwa tamasha hilo limekuwa na mafanikio makubwa kwa wananchi kuwapatia fursa mbalimbali hasa za kibiashara kwa wajasiriamali, wavuvi na wafugaji kuuza bidhaa zao kwa wageni wanaotembelea maeneo hayo.
Katibu wa tamasha hilo, Hamid Abdulhamid Khamis amesema tamasha hilo litakuwa na kongamano la nishati safi ambalo litatoa fursa juu ya matumizi sahihi ya nishati.
Pia, amesema tamasha litakuwa na mashindano mbalimbali ikiwemo taarabu asilia, ngoma asilia, Bongo Fleva, dansi, mbio za ngalawa, baiskeli, bao, karate na zuma, na litaambatana na ufunguzi wa miradi ya maendeleo.
Hivyo, ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kujionea bidhaa na huduma zitakazotolewa.
Mmoja wa wasisi wa tamasha hilo, Said Hamad Ramadhan amesema katika wilaya hiyo ya Kusini, wanaiona miradi ya maendeleo inayozidi kuongezeka jambo ambalo limesababishwa na uwepo wa tamasha hilo.