Tabora. Catherine Inocent Petro (21) mkazi wa kata ya Kalunde Manispaa ya Tabora amefariki dunia baada ya kunywa dawa ya kuulia wadudu, huku chanzo cha uamuzi huo kikidaiwa kuwa ni migogoro ya mapenzi.
Taarifa ya tukio hilo imetolewa leo Juni 17,2025 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao.
Amesema Catherine Inocent Petro amefikia uamuzi huo baada ya kuwa na migogoro ya mapenzi na mume wake na kuamua kunywa sumu ya kuulia wadudu ambapo alipelekwa katika zahanati ya Umanda na kupata huduma ya kwanza, kisha akapewa rufaa na kutakiwa kupelekwa Hospitali ya Milambo kwa matibabu zaidi.
“Tuna tukio la kujiua na limetokea huko Umanda kata ya Kalunde lakini chanzo ni migogoro ya kifamilia kati ya marehemu na mume wake ambapo Juni 14,2025 mume wa marehemu akitoka matembezi usiku alimkuta mke wake anagalagala nje alipomuuliza akasema amekunywa sumu ya kuulia wadudu, alimpeleka zahanati lakini baada ya huduma ya kwanza walitakiwa kumpeleka Hospitali ya Milambo, hata hivyo marehemu hakupelekwa badala yake walimrudisha nyumbani ambapo Juni 15,2025 alifariki dunia,”amesema Kamanda Abwao.
Kamanda huyo amewahimiza wananchi mkoani Tabora kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi badala yake, wanapokuwa na mgogoro washirikishe wapendwa wa karibu hata kwenda hospitali au kituo cha Polisi kwani kuna huduma za ushauri na tiba za saikolojia ambapo anaweza akazipata na akarejea katika hali ya kawaida.
“Hospitali zetu na vituo vya polisi pia zipo huduma za saikolojia na ushauri pia ambao unaweza kumfanya mtu aone ni vitu vya kawaida na akaweza kuidhibiti changamoto yake badala ya kukaa kimya inapelekea mtu kuchukua maamuzi magumu na ya uvunjaji wa sheria” amesisitiza.
Mkurugenzi wa Shirika la Akili nchini, mwalimu Robert Roghat ameshauri kuwa na tabia ya kubadili mazingira endapo anakua na hali ya huzuni au hasira ili kujiepusha kufikia hatua mbaya ya kujitoa uhai.
“Kwa mfano kama una hasira ikiwa umesimama inabidi ukae au utembee hatua chache kitendo hicho kitakufanya ubadili maamuzi na pia kujenga tabia ya kuangalia wanyama ile humfanya mtu kutuliza akili, lakini pia kujenga tabia ya kushirikisha watu matatizo yanayokukabili kwani ukilizungumza jambo kuna sumu hua inapungua hivyo kubadili dhima ya ubongo kwa muda huo”ameshauri Robert.