Iringa. Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Iringa kimewaonya na kuwaasa wagombea wanaotarajia kuwania nafasi mbalimbali katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 mkoani humo, kuepuka matusi na kejeli dhidi ya viongozi wa chama hicho, badala yake wajikite katika sera na maadili.
Hayo yalielezwa Juni 16, 2025, katika kikao kilichofanyika katika ofisi za CCM Mkoa wa Iringa, zilizopo ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Iringa.
Kikao hicho kilihusisha viongozi wa CCM mkoani humo na waandishi wa habari, ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Daudi Yassin amelaani tabia ya baadhi ya watia nia wanaotangaza dhamira zao za kugombea kupitia vyombo vya habari huku wakijihusisha na matamshi ya kubeza, kudhalilisha na kuvunjia heshima viongozi wenzao ndani ya chama.
Yassin alisema kuwa mwenendo huo unakwenda kinyume na maadili, kanuni na miongozo ya CCM, na kusisitiza kuwa chama hakiwezi kuvumilia lugha za kejeli na dharau zinazotishia mshikamano, umoja na heshima miongoni mwa wanachama wake.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (CC) na pia Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Salim Faraj Abri (Asas), amesema kuwa tayari baadhi ya wanachama wanaotaka kugombea nafasi mbalimbali katika Uchaguzi Mkuu wa 2025 wameanza kuitisha mikutano na waandishi wa habari kwa ajili ya kueleza nia zao.

Hata hivyo, amesema ni jambo la kusikitisha kuona baadhi ya watia nia hao wakitumia majukwaa hayo kuwakashifu, kuwadhalilisha na kuwatuhumu viongozi wenzao wa chama, badala ya kujikita katika sera, hoja na maadili ya kisiasa.
Alionya kuwa mwenendo huo haukubaliki na unakwenda kinyume na misingi ya chama, ambayo inasisitiza mshikamano, heshima na nidhamu miongoni mwa wanachama wake.
Kwa mujibu wa Asas mfumo wa kuchuja wagombea si wa kumtenga yeyote bali ni mchakato wa kawaida kuhakikisha wanapatikana watu sahihi watakaoliwakilisha chama na wananchi kwa ufanisi.
“Nitoe mfano rahisi kupitia mapishi, unapopika mchele mzuri, ni lazima kwanza uuchambue kwa uangalifu ili kuondoa mawe na uchafu. Hapo ndipo unapata mchele safi unaofaa kupikwa. Vivyo hivyo katika CCM, tutawapepeta watia nia kwenye ungo ili kuwabaini wale wanaofaa kupewa dhamana ya kugombea.
“Wakati ukifika, kila mmoja atakuja kwenye ungo huo, na tutapima kwa umakini ili kubaini nani anastahili na nani hastahili kuendelea. Huo ndiyo mchakato wa kuchuja,” alifafanua Asas.
Naye Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa, Said Goha alisema mchakato rasmi wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu utaanza 28 Juni, 2025, kwa mujibu wa ratiba ya chama hicho.
“Huo ndiyo mwanzo wa mchakato rasmi na mtu yeyote anayeonekana kufanya mikutano kwenye matawi kabla ya tarehe hiyo ni wazi anakwenda kinyume na utaratibu wa chama, na hilo litachukuliwa kama kampeni za mapema,” amesema Goha.
Goha ameongeza kuwa CCM haitaruhusu aina yoyote ya kampeni za chinichini kabla ya muda rasmi uliopangwa, kwani hali hiyo huibua migogoro na vurugu za kisiasa.
Ili kuepusha migogoro inayotokana na kura za maoni, Goha amesema chama kitapitia kwa makini majina yote ya wagombea na kisha kuchuja hadi kubakiwa na majina matatu tu kutoka kila eneo na kufikia hapo wananchi ndio watachagua anayewafaa.