IGP amhamisha RPC Dodoma | Mwananchi

Dar es Salaam. Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP) Camillus Wambura amefanya uhamisho wa makamanda watatu akiwemo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, George Katabazi.

Taarifa ya uhamisho huo imetolewa leo na Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime ikiwa ni siku 302 tangu Katabazi alipoteuliwa rasmi kukalia kiti hicho, Agosti 19 mwaka jana.

Katabazi anatolewa kuwa kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma na kupelekwa ofisi ya makao Makuu ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai Dodoma.

Nafasi yake imechukuliwa na Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Galus Hyera ambaye alikuwa Kamanda wa Polisi Kikosi cha Reli.

Katabazi alichaguliwa kuwa kamanda wa polisi Dodoma akichukua nafasi ya Theopista Mallya ambaye alitolewa katika nafasi hiyo ikiwa ni siku moja baada ya kutoa kauli juu ya mwenendo wa upelelezi wa tukio la ubakaji na ulawiti wa binti aliyedaiwa kuwa mkazi wa Yombo Dovya, jijini Dar es Salaam.

Aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, George Katabazi.



Tukio hilo ambalo lililoanza kusambaa katika mitandao ya kijamii Agosti 2, 2024 na kudaiwa kufanyika jijini Dodoma katika mwendelezo wake Kamanda Mallya aliliambia Mwananchi kuwa “Kilichobainika vijana hao hawakutumwa na askari, walikuwa kama walevi na wavuta bangi tu, lakini yule dada alikuwa kama anajiuza (kahaba).”

“Neno askari ni General (jumla) kwa kuwa hata mgambo ni askari, hivyo hatuwezi kulifafanua zaidi kwa kuwa haikubainishwa wazi na tunaliacha hivyo,” alisema Kamanda Mallya, baada ya kuulizwa nini kinaendelea juu ya uchunguzi wa watuhumiwa hao.

Hata hivyo, Jeshi la Polisi liliikana kauli hiyo na kusema haukuwa msimamo wa jeshi hilo, bali kauli sahihi ni zile zilizokuwa zimetolewa na msemaji wa jeshi hilo kwa umma Agosti 4, 6 na 9, 2024.

Msingi wa Jeshi la Polisi kutoa taarifa hiyo ni habari iliyochapishwa na Mwananchi, Agosti 19, 2024 yenye kichwa cha habari ” RPC: Anayedaiwa kubakwa, kulawitiwa na vijana wa ‘afande’ ni kama anajiuza.

Hata hivyo mpaka sasa haijaelezwa kama Mallya aliondolewa kwenye nafasi hiyo kwa ajili ya mkanganyiko uliojitokeza.

Mbali na kuhamishwa kwa Katabazi, pia Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Matride Kuyeto amehamishwa kutoka kuwa mkuu wa Polisi Wilaya ya Kinondoni kwenda kuwa Kamanda wa Polisi Kikosi cha Reli.

“Uhamisho huo ni mabadiliko ya kawaida yanayofanyika ndani ya Jeshi la Polisi katika kuongeza ufanisi wa utendaji kazi,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Related Posts