Arusha. Ikiwa zimepita siku 33 tangu Mchungaji wa Kanisa la Huduma ya Kristo, Steven Jacob (35) ,kutekwa na watu wasiojulikana na baadaye kuokolewa na walinzi wa mashamba ya ngano mkoani Kilimanjaro, Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limesema linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.
Mchungaji huyo anayehudumu kwenye kanisa lililopo Mtaa wa FFU, Kata ya Muriet, mkoani Arusha, alitekwa Mei 16,2025 asubuhi alipotoka nyumbani kwake kisha kupatikana Mei 17, 2025 katika eneo la West Kilimanjaro wilayani Siha, Mkoa wa Kilimanjaro.
Akizungumza na Mwananchi leo Juni 17,2025, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo amesema uchunguzi wa tukio hilo bado unaendelea ili kubaini ukweli wake.
“Bado uchunguzi unaendelea kufanyika ili tujue uhalisia na ukweli wenyewe na tutaangalia kama alitekwa au kuna watu alikuwa na shida nao, tutatoa taarifa uchunguzi ukikamilika,”amesema Kamanda Masejo
Mei 25,2025, baba mzazi wa mchungaji huyo ambaye pia ni mchungaji na balozi wa nyumba 10 wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Jacob Gumbo alisema kwa sasa wamemuachia Mungu suala hilo na wanaendelea kumuuguza ndugu yao.
“Polisi walishakuja tangu ile siku amepatikana hapo wakachukua maelezo ila baada ya pale hatujapata mrejesho wowote.Hakuna hatua nyingine yoyote tuliyochukua sisi tumemuachia Mungu na tunaendelea kumuuguza hapa nyumbani,”alisema.
Awali akisimulia tukio hilo Mchungaji Steven alidai watu hao waliomteka walijitambulisha kwake kuwa maofisa wa polisi, lakini hawakumuonyesha vitambulisho wakidai wanampeleka kituo kikuu cha polisi.
Alisema kutokana na namna walivyomchukua alielewa ametekwa,kwani hawakuwa na vitambulisho na hawakutaka aage mtu, badala yake walimchukua na kumfunga vitambaa viwili usoni na pingu mkononi, ndipo alipopiga kelele kuwa anatekwa, kisha watu hao wakamrusha kwenye gari na kuondoka naye kwa kasi.
Mchungaji huyo alidai waliomteka walimpeleka hadi eneo hilo la West Kilimanjaro ambako walichukua simu zake za mkononi na kumtaka afute picha mjongeo (video) alizokuwa amepandisha kwenye mtandao wa Youtube.
“Naomba nisiongee mengi kwa sababu ni ishu za mtandao nilipost Youtube. Baada ya kunipiga na kuchukua baadhi ya maelezo ambayo nafikiri nisingependa kuyaongea, baada ya pale nikasikia kama wananipeleka mahabusu ila haikuwa hivyo, wakanipeleka porini West Kilimanjaro.
“Walivyotaka nifute kwa bahati mbaya bando lilikuwa limeisha, ikabidi wafanye mpango wapate bando, wakasema wawili au mmoja abaki na mimi halafu wengine wakatafute bando ili nifute video,”alisema.
Mchungaji huyo alisema watu hao walimwambia alale chini wakamkanyaga shingoni, mmoja akawaambia wenzake wanamuachaje hapo. Alisema mambo mengine hawezi kuzungumza zaidi ila walimuacha wakaondoka na simu yake.
“Walivyoondoka nikaanza kubiringita na kutembea kwa magoti hadi barabarani, nikafika barabarani pakatokea bodaboda, alivyoona ile hali akapita, lori la mafuta nalo likaogopa.
“Wakaja watu wanaolinda tembo wasiingie kwenye mashamba, nikajitambulisha mimi ni mtumishi wa mtandaoni nimetekwa nimetupwa huku nisaidieni, mmoja wao alikuwa mwoga kesi isije kuhamia kwao, ila wakanisaidia. Nikaomba simu ili niwajulishe watu niko hai,”alisema.
Mchungaji huyo alisimulia: “Walinipeleka kwenye kambi yao na baadaye wakaniambia watu wale wamerudi kule kama wananitafuta, wakafanya mpango nikatolewa nikaenda sehemu nyingine, naomba mengine nisongee.”
Kumekuwa na kilio kuhusu utekaji nchini, tukio la hivi karibuni likiwa la kutekwa mwanaharakati na kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mdude Nyagali tangu Mei 2,2025 alipovamiwa na kushambuliwa nyumbani kwake ambapo hadi sasa hajulikani alipo.