Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezindua chaneli ya kwanza nchini (Somakwanza Tv) yenye maudhui ya kitaaluma, itakayorusha vipindi vya elimu kuanzia ngazi ya awali, msingi hadi sekondari kwa saa 24 bila kukatika.
Chaneli hiyo, inayosimamiwa na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), itakuwa na vipindi vya masomo mbalimbali kwa ngazi zote za elimu, ikilenga kuwapa walimu na wanafunzi fursa ya kujifunza kwa urahisi na ubora zaidi.
Akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya TET, leo Jumanne Juni 17, 2025 Majaliwa aliyekuwa mgeni rasmi, amesema uzinduzi wa televisheni hiyo (chaneli) ni hatua muhimu katika kupanua fursa za ujifunzaji kwa watoto, kwa kuwapa maudhui yenye tija wanapotazama televisheni.
Majaliwa amesema katika dunia ya sasa inayosukumwa na maendeleo ya sayansi na teknolojia, elimu imeendelea kuwa nguzo kuu ya maendeleo ya mtu binafsi na Taifa kwa jumla.
Hivyo, kuanzishwa kwa chaneli hiyo kutakuwa msaada mkubwa wa kusambaza maarifa kwa njia rahisi, jumuishi na ya kuvutia kwa wanafunzi na walimu kote nchini.
“Tunaamini kupitia televisheni hii itatolewa elimu kuhusu maadili, uzalendo, afya ya jamii na masuala ya kijamii. Vipindi vitakuwa vyenye kujenga jamii yenye mshikamano, inayozingatia maadili mema na uzalendo,” amesema Majaliwa.
Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dk Aneth Komba amesema televisheni imeanzishwa kwa ushirikiano kati ya Serikali kupitia TET na Shirika la Soma Kwanza Initiative.
“Hii ni TV ya kwanza ya Serikali ambayo imelenga kuandaa na kurusha maudhui ya kielimu kwa saa 24 ikiwamo vipindi mbalimbali katika mtalaa kuanzia elimu ya awali, mpaka vyuo vya ualimu.
“Kwa sasa inapatikana kwenye king’amuzi cha Star Times Channel 105, lengo kwa siku za usoni ni kurusha kwenye vingamuzi vyote ili kuweza kuwafikia walengwa wengi zaidi. Vilevile, kupitia ushirikiano huu tuna lengo la kuanzisha TET/SOMA Kwanza Radio,” amesema.
Felista Njolay ambaye ni mwalimu wa sekondari amepongeza hatua hiyo akieleza kuwa kwa kutumia televisheni, wanafunzi wanaweza kupata masomo muhimu bila hitaji la kuwa darasani moja kwa moja.
“Hii ni suluhisho la changamoto ya uhaba wa walimu na miundombinu isiyotosheleza katika baadhi ya shule nchini. Pia, itakuwa msaada mkubwa kwa wanafunzi wanaojiandaa na mitihani ya kitaifa,” amesema.
Katika hatua nyingine, Majaliwa amepongeza watu walioshiriki kuchangia kampeni ya kitabu kimoja mwanafunzi mmoja iliyofanikisha kukusanya Sh2.6 bilioni.
Ameahidi kiasi hicho cha fedha kitatumika kwa dhumuni lilikokusudiwa ambalo ni kuhakikisha mwanafunzi anapata kitabu kwa kila somo.
“Kwa upande wetu Serikali tutaendelea kutenga fedha kuhakikisha utekelezaji wa lengo hili linakuwa endelevu, pia tuendelee kufanya uwezekaji kwenye Tehama (Teknolojia ya Habari na Mawasiliano),” amesema Majaliwa.
Kuhusu uandaaji wa vitabu, Dk Aneth Komba amesema katika kipindi cha miaka 50 taasisi hiyo imefanikiwa kuandaa vitabu vyote vya kiada pamoja na Kiongozi cha Mwalimu kuanzia ngazi ya elimu ya awali mpaka ualimu kwa shule na vyuo vinavyotumia Kiswahili na Kiingereza kama lugha za kufundishia.