Mpina amwambia Rais Samia jimboni kwake bado wanamdai

Dar es Salaam. Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina amemwambia Rais Samia Suluhu Hassan kuwa jimbo lake bado linamdai fedha za maendeleo na kwamba maeneo mengine yanayodai hayamdai, fedha zao zihamishiwe Kisesa.

Mpina ametoa kauli hiyo leo, Jumanne Juni 17, 2025, wakati wa mkutano wa hadhara unaofanyika Wilaya ya Meatu, mkoani Simiyu, ikiwa ni sehemu ya ziara ya Rais Samia mkoani humo.

Katika hotuba yake, Mbunge huyo amegusia pia changamoto ya ununuzi wa pamba kwa kutumia mnunuzi mmoja, akisema kuwa hali hiyo inapunguza ushindani na inazua matatizo iwapo mnunuzi huyo atapata changamoto za kifedha.

“Ombi la tatu Mheshimiwa Rais, suala la mnunuzi mmoja wa pamba linakwamisha ushindani. Na kule Kisesa bado tunakudai. Wanaosema hawakudai, hawakudai zile fedha zihamishwe zije zote Kisesa sababu bado tuna mipango mingi ya maendeleo katika maeneo yetu,” amesema Mpina.

Pamoja na hayo, ametoa pongezi kwa Rais kwa kuunda tume ya maboresho ya kodi, akisema hatua hiyo inaleta matumaini ya kutatua changamoto sugu katika mfumo wa kodi nchini.

Endelea kufuatilia Mwananchi.

Related Posts