Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, limezuia mkutano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) uliopangwa kufanyika ukumbi wa Milllenium Tower Kijitonyama jijini hapa.
Mkutano huo ulipangwa kuhutubiwa leo Juni 17,2025 na Makamu Mwenyekiti wa Chadema ( Bara), John Heche ambaye hadi saa 4:45 alikuwa hajafika hotelini hapo kwa ajili ya kuzungumza kwenye mkutano huo.
Wakati waandishi wakiwa tayari wamekusanyika wanamsubiri Heche katika ukumbi wa uliopo ghorofa ya tano, ndipo akaja Brenda Rupia ambaye ni mkurugenzi wa mawasiliano na uenezi wa Chadema akabadilishana mawazo baadhi wanahabari kisha kuketi pembeni mwa meza kuu.
Ghafla wakaingia maofisa wa Polisi watatu mmoja akiwa amevaa sare waliojitambulisha wanatoka Kinondoni na Kanda Maalumu Dar es Salaam, wakauliza nani muhusika wa mkutano huo.
Polis: Nani kiongozi wa hili jambo?
Hawakujibiwa kukawa kimyaa…
Polisi tena: … nani muhusika wa hili jambo?
Ndipo Rupia akasimama na kujibu ni ‘mimi’
Pilisi: Unafanya mkutano kama nani?
Polisi: Humjui kama hamtakiwa kufanya mnachokifanya
Rupia: Nafanya kama Brenda
Polisi: Kwa taarifa za uhakika hapa kuna mkutano wa Chadema uliotangazwa toka jana ambao hauruhusiwi kufanyika kutokana na amri ya mahakama iliyotolewa.
Polisi: Any way iwe ni Brenda au Chadema sitisheni mara moja.
Brenda: Sioni kama ninachokifanya ni kosa kisheria.
Polisi 2: Iwe ni wewe au Chadema sitisheni mara moja kinachoendelea.
Polisi 1: Sio jambo la kutaka muda tena sitisheni sasa hivi.
Brenda: Kwani ulazima nisitishe mbele yenu nipeni japo muda nizungumze na niliowaalika.
Polisi 2: Hili sio ombi ni amri na waandishi si mpo hapa hakuna mkutano wala jambo litakaloendelea naomba mtoke nje ya ukumbi.
Baada ya muda wanahabari wakatoka nje ya ukumbi kushuka chini wakakuta gari za Polisi aina ya Defender mbili zenye askari polisi waliovaa kiraia na sare wamekaa.
Askari hao walikuwa wanahoji mkutano huo wa Chadema kufuatia uamuzi wa Mahakama kukizuia chama hicho kufanya shughuli za siasa hadi kesi ya msingi itakaposikilizwa. Uliotolewa Juni 10, 2025 na Jaji Hamidu Mwanga kufuatia kesi iliyofunguliwa na wanachama wa Chadema akiwemo aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti- Zanzibar, Said Issa Mohamed.
Kesi ya msingi kuhusu mgawanyo wa rasilimali za chama hicho imepangwa kuanza kusikilizwa Juni 24, 2025.
Licha ya amri hiyo, makada wa Chadema akiwamo Brenda walikuwa bado katika viunga vya hoteli kabla ya polisi kuingia ndani na kuwatoa kilazima nje ya ukumbi wa jengo hilo.
Hadi makada na walinzi wa Chadema wanaondoka, Polisi walikuwa wakizunguka katika eneo hilo, wakiimarisha ulinzi unaolenga kuzuia mkutano huo kufanyika.