Rais Samia Suluhu Hassan amejibu hoja za Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina, aliyesema jimbo lake linamdai, akisema kwamba mbunge huyo anaonekana kutumikia Taifa zaidi badala ya jimbo lake kwa kushindwa kuzungumzia masuala ya maendeleo ya jimbo hilo na badala yake anajitafutia umaarufu.
“Ndugu zangu, maombi kama haya yamekwishawasilishwa bungeni na mawaziri wakatekeleze. Kuleta maombi haya hapa kwenye mkutano wa Rais ni kujitafutia umaarufu na kuthibitisha kuwa Mbunge hakulifanyia haki jimbo lake,” amesema Rais Samia alipokutana na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Meatu, Simiyu, leo Jumanne Juni 17, 2025.
Rais Samia amesisitiza kuwa Mbunge anapaswa kutumia nafasi yake bungeni kutatua changamoto za wananchi badala ya kuzipigia kelele hadharani. Aidha, amekumbusha kuwa jimbo la Kisesa limepata maendeleo makubwa, kinyume na madai ya mbunge wake.
“Mbunge wa Kisesa anasema jimbo lake halina maendeleo, lakini rekodi za Serikali zinaonyesha kinyume chake. Hii ni kuonesha udharau kwa jimbo lake,” amesema Rais Samia huku akiwataka wananchi kuwachagua wabunge watakaoleta huduma za kweli badala ya siasa za kujitafutia umaarufu.