Sababu bima ya vyombo vya moto kuongoza, afya bado

Dar es Salaam. Sekta ya bima nchini inaendelea kushuhudia ukuaji mwaka hadi mwaka, huku bima ya vyombo vya moto ikiongoza kwa kuingiza mapato makubwa, ikifuatiwa na ya maisha, wakati ya afya ikishika nafasi ya tatu kwa mchango wake katika sekta hiyo.

Wadau wa sekta ya bima wanasema bima ya vyombo vya moto inaongoza kutokana na hofu ya hasara miongoni mwa wamiliki, pamoja na msisitizo wa kisheria wa kuhakikisha kila chombo kinakuwa na bima.

Kwa upande wa bima za afya, wadau wanataja gharama za vifurushi kuwa kikwazo kinachochangia ukuaji wake kuwa taratibu.

Akizungumza leo Jumanne, Juni 17, 2025 na Mwananchi, Denis Sikazwe ambaye ni mkazi wa Tabata Mwananchi amesema mkazo uliowekwa katika vyombo vya moto ndiyo unaweza kuwa sababu.

“Nani anaweza kuendesha gari au pikipiki kwa ujasiri mtaani bila kuwa na bima, hayupo, nguvu kubwa imewekwa katika kuhakikisha kila chombo kinakuwa na bima, huenda hiyo ndiyo sababu ya kuwa namba moja, lakini hata bei zao ni kubwa na watu hawagomi kwa sababu wanajua athari za kutokuwa na bima,” amesema Sikazwe.

Maneno yake yaliungwa mkono na Nelson Masanja, mkazi wa Tabata akisema watu wengi wanakatia bima vyombo vyao ili kuwa na uhakika wa matengenezo itakapotokea dharura.

“Sasa unajua ukiugua unaweza kutibiwa kwa pesa kiasi tofauti na pikipiki yako ikikanyagwa, ni fedha nyingi zinahitajika na ndiyo kitu kinafanya nyumbani mle, lazima uweke mazingira mazuri kwa ajili ya kitu kinachokuingizia kipato,” amesema Masanja huku akikiri kuwa bima ya afya ni muhimu lakini jitihada zaidi na elimu inahitajika sambamba na kufanya mapitio ya vifurushi.

Akizungumzia suala hilo, mtaalamu wa bima, Anselmi Ancellmi amesema bima ya afya kushika namba tatu haimaanishi kuwa watu hawaihitaji bali mifumo iliyopo ndiyo inayowafanya wengi kuendelea kusalia nje.

Amesema ili kuthibitisha hilo, zinahitajika tafiti zinazoweza kutoa mwongozo wa namna ya kupanga vifurushi vya bima ya afya ili watu wengi waweze kujiunga kulingana na uwezo wao, aina gani za bima wanazotaka.

“Pia, uwekezaji katika teknolojia, watu wanunue bima kwa urahisi wakiwa nyumbani, kungekuwa na uwekezaji katika teknolojia ingerahisisha hata upatikanaji wa huduma kwa kuondoa ule mlolongo wa mtu kupata shida mawasiliano yafanyike kwa watu hadi watatu ndiyo suluhisho lipatikane,” amesema Ancellmi.

Amesema changamoto iliyopo si kwamba watu hawahitaji kununua bima au hawazihitaji bali gharama na upatikanaji wa huduma.

Kwa mujibu wa taarifa ya hali ya uchumi ya mwaka 2024 iliyotolewa na Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, mauzo ya bima za kawaida yaliongezeka kwa asilimia 12.7 hadi Sh1.099 trilioni kutoka Sh974 bilioni mwaka 2023.

Katika mwaka huo, bima ya vyombo vya moto iliingiza Sh384.8 bilioni ikifuatiwa na bima ya moto (Sh189.9 bilioni) na afya (Sh162 bilioni).

Bima za maisha nazo ziliongezeka kwa asilimia 9.8, kufikia Sh290.5 bilioni kutoka Sh264.5 bilioni.

Watoa huduma wa bima waliongezeka hadi 2,208 kutoka 1,549 mwaka 2023 (ongezeko la asilimia 42.5) kutokana na kurahisishwa kwa usajili, matumizi ya mifumo ya kidijitali na huduma mpya. Ingawa kampuni za bima zilibaki 35, mauzo ya jumla yalipanda hadi Sh1.418 trilioni kutoka Sh1.24 trilioni.

Mauzo ya bima ya biashara za nje yaliongezeka kwa asilimia 4.8 hadi Sh28.6 bilioni na thamani ya mali za kampuni za bima ilifikia Sh2.339 trilioni kutokana na mapato ya ada, uwekezaji serikalini na maeneo mengine.

Wakati huohuo, Serikali imependekeza vyanzo vipya vinane vya mapato mwaka 2025/26 ili kufadhili bima ya afya kwa wote na kudhibiti maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU), ikitarajia kuongeza mapato ya Sh586.4 bilioni. Miongoni mwao ni kodi kwa vileo, mafuta, madini na michezo ya kubashiri.

Related Posts