Morogoro. Bodi ya Bonde la Wami-Ruvu imetangaza mpango wa kufukua kipande cha kilomita 1.7 cha Mto Morogoro na kuupeleka kwenye njia yake ya asili, ili kukabiliana na athari za mafuriko zinazoendelea kuathiri wakazi wa Mtaa wa Mambi, Kata ya Mafisa.
Kwa zaidi ya miaka 10, wakazi wa eneo hilo wamekuwa wakikumbwa na mafuriko, tatizo lililoanza kuongezeka tangu mwaka 2017 baada ya mto huo kuacha njia yake ya asili, kufuatia mvua kubwa zilizonyesha na kusababisha zoambatana tope, takataka na mchanga kuujaza kutoka milima ya Uluguru.
Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Bonde la Wami-Ruvu, Marthin Kasambala amesema taasisi hiyo imefanya tathmini kufuatia agizo la Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mussa Kilakala, na imependekeza kutumia Sh26 milioni kuufukua Mto Morogoro kwa urefu wa kilomita 1.7, ili kuokoa makazi ya wakazi.
“Tunashirikiana na wadau kama Tanesco, Manispaa ya Morogoro, Tarura na Bonde la Wami-Ruvu kutafuta suluhisho la pamoja kwa changamoto hii. Tuliandaa mpango wa kuanza kazi hiyo, lakini mvua zimechelewa kukata, hivyo mitambo haijaweza kuingia kazini,” amesema Kasambala.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi wote waliopo ndani ya mita 60 kutoka mtoni kuondoa makazi yao ili kuepusha athari zaidi kipindi cha mvua.
Akizungumza na Mwananchi, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mambi, Hamad Salum amesema kuwa hali hiyo imekuwa sugu kila msimu wa mvua, ambapo wakazi hupoteza mali na baadhi yao kuzingirwa na maji.
Amebainisha kuwa tangu Desemba 2024, nyumba 42 zilikuwa zimezingirwa, lakini idadi hiyo sasa imeongezeka hadi kufikia 114.
“Tumewahi kufanya juhudi za kuchangisha Sh4 milioni kwa ajili ya kukodisha skaveta ili kuchepusha mto, lakini hatukufanikiwa. Tumeendelea kuhamasisha wananchi na taasisi kushiriki kutafuta suluhu ya kudumu,” amesema Salum.
Yusuph Maruzuku, mkazi wa Mambi, amesema: “Taasisi za Serikali zina mitambo kama skaveta inayoweza kufanikisha kazi hii. Wananchi wapo tayari kushiriki, lakini kazi kama hizi zinahitaji vifaa rasmi.”
Kwa upande wake, Martha Mkude, mkazi wa eneo hilo amesema: “Watu wamehama nyumba zao baada ya maji kuingia ndani. Hali ni mbaya, tunaiomba Serikali na wadau wachukue hatua za haraka kurejesha mto kwenye mkondo wake wa asili.”
Rehema Nassoro, mkazi mwingine, ameeleza kuwa watoto wao wanashindwa kuhudhuria shule kwa siku tatu hadi saba mfululizo kwa sababu ya mafuriko, huku wazazi wakihofia watoto wao kupata maradhi wanapochezea maji machafu.