Musoma. Mahakama Kuu Kanda ya Musoma imemuhukumu mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara pamoja na wenzake wawili kumlipa fidia ya Sh6 bilioni Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Eliakim Maswi baada ya kupatikana na hatia katika kesi ya kashfa dhidi yao.
Hukumu hiyo ilitolewa mahakamani hapo jana Juni 16, 2025 na Jaji Marlin Komba ambaye amesema kwa mujibu wa ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo, amejiridhisha pasipo na shaka kuwa watuhumiwa walitenda kosa hilo kinyume cha sheria.
Jaji Komba amewahukumu wadaiwa kumlipa Maswi Sh1 bilioni kama fidia ya adhabu ya udhalilishaji baada ya kubainika kuwa alitumia maneno ya uongo na kumkashifu Maswi.
Pia, Jaji Komba ameamuru Maswi kulipwa Sh5 bilioni kama fidia ya madhara ya jumla pamoja na kuombwa radhi hadharani kupitia vyombo vya habari.
Amesema kabla ya hukumu hiyo washtakiwa walitakiwa kuomba msamaha, lakini walikataa kufanya hivyo.
Jaji Komba amesema maneno hayo ya Waitara hayakuwa ya kashfa kwa Maswi pekee bali kwa watumishi wa umma kwa ujumla na kuwa Waitara aliamua kufanya hivyo kwa sababu hajawahi kuwa mtumishi wa umma.
Katika kesi hiyo, Maswi alidai kuwa Agosti 9, 2023, Waitara alitoa maneno ya kashfa dhidi yake katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Mtana, Kata ya Manga wilayani Tarime mkoani Mara, uliohudhuriwa na watu zaidi ya 500.
Alidai kuwa maneno hayo yaliandikwa na kuonyeshwa kupitia televisheni ya mtandaoni ya Mara TV kutoa maneno hayo yalikuwa ya uongo, yenye nia ovu, na yalilenga kushusha hadhi yake. Katika kesi hiyo waliunganishwa Karoli Jacob na Mara TV.
Maswi alidai kuwa kwenye mkutano huo, Waitara alisema Maswi anahusika na kuwajibika kwa vitendo vya rushwa na matumizi mabaya ya nafasi yake kwenye utumishi wa umma, kama Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Ununuzi (PPRA).
Maswi alidai televisheni ya mtandaoni ya Mara TV ilichapisha maneno hayo na kwamba hadi Agosti 13, 2023 chapisho hilo lilitazamwa na watu zaidi ya 280 kutoka duniani kote.
Alidai kuwa maeneo hayo ya kashfa mbali na kuwa ni ya uongo na yenye nia ovu, yalilenga kumshushia hadhi yake katika jamii.