Kahama. Watu wanne wanaodaiwa kuwa ni vibaka wameuawa kwa kupigwa mawe na kisha kuchomwa moto na wananchi wenye hasira katika Mtaa wa Mhongolo Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga alfajiri ya kuamkia leo Juni 17, 2025.
Kijana aliyejeruhiwa kwa kukatwa panga eneo la kichwani na wanaodaiwa kuwa ni vibaka saa tano usiku wa kuamkia leo, Stephano Maganga amesema usiku huo mdogo wake alikuwa anaenda kwenye harusi ndipo akakutana nao, ndipo alipokwenda na kuishia kujeruhiwa.
Amesema vibaka hao walimpora simu mdogo wake ndipo akarudi nyumbani na kumweleza kaka yake, ambaye alifuatilia na kuwakuta vijana hao kisha kuanza kuwahoji hali iliyozua mtafaruku kati yao.
Amesema baada ya kuuliza simu ya mdogo wake ndipo walipotoa mapanga na kuanza kumpiga mabapa na baadaye kumkata eneo la kichwani.

Amesema, “mdogo wangu alikuwa anaenda kwenye harusi, alivyoporwa simu akarudi nyumbani akanieleza, akanipeleka walipo, baada ya kuwauliza wakaanza kunishambulia ndipo wakafanikiwa kunikata panga, lakini mdogo wangu hakujeruhiwa”
Naye mama ambaye hakutaka kutaja jina lake amesema alfajiri ya Juni 17, 2025 alikuwa anaenda kanisani na mtoto wake ndipo alipokutana na kundi la vibaka waliojaribu kumpora pochi yake.
Amesema wakati anavutana nao ndipo mwanawe aliyeingilia kutaka kumsaidia mama yake akajeruhiwa na vibaka hao, ndipo alipopiga kelele zilizopelekea watu kujaa na kuwashambulia vijana hao kisha kuwachoma moto.
Kijana Ibrahimu Jacob mkazi wa Mhongolo ambaye amepitia adha ya kupigwa na vibaka mara kadhaa na kunyang’anywa fedha, simu na vitu alivyokuwa navyo, amesema eneo hilo ni hatari kwa vibaka na kuliomba Jeshi la Polisi kudumisha ulinzi zikiwemo doria.

Amesema, “unakuta wewe unatoka kutafuta riziki, unaporudi saa moja usiku kukiwa na giza la wastani, unavamiwa unapigwa unanyang’anywa kila ulichobeba. Nilishawahi kupigwa na vibaka sio mara moja wala mara mbili, nikaporwa fedha, simu na matunda nilikuwa napeleka nyumbani.”
“Tunaliomba Jeshi la Polisi, hiyo gari yao iwe inafanya sana doria maeneo ya huku, angalau kidogo gari yao iwe inapaki maeneo ya shule ndipo mara nyingi wanajificha kwenye miembe,”ameongeza.
Naye Juma Bernard amesema changamoto ya vibaka kwenye mtaa huo inatokana na vijana wengi kutojituma kufanya kazi, badala yake wanashinda kwenye vijiwe, au kuzurura mitaani na kuwataka wajifunze kutokana na tukio hilo.
“Vijana wengi wa sasa hawataki kujituma wanazurura tu sasa matokeo yake ndio kujiingiza kwenye uporaji na kuishia mikononi mwa wananchi wanaochoshwa na vitendo hivyo. Haya mazingira yetu sio rafiki sana kwa usalama wetu, panya road ni wengi, hata ukipita wewe ni bodaboda wanakusimamisha kama mteja wanakukaba,” amesema Bernad.

Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Mhongolo, Emanuel Nangale amesema alipata taarifa za kuuawa kwa vijana hao leo asubuhi, baada ya kufika eneo la tukio akiambatana na viongozi wenzake wakakuta tayari wananchi wametekeleza kitendo hicho.
“Kwa taarifa nilizopokea kutoka kwa wananchi wangu ni kwamba wamekaba watu sana usiku wa kuamkia leo, jana usiku wamepora simu na wakamkata panga kaka wa aliyeporwa wakati akifuatilia simu ya mdogo wake.”
“Tena kuna mama mwingine alfajiri ya leo alikuwa anaenda kwenye maombi kanisani wakampora pochi, ndipo kwenye purukushani mwanaye akajeruhiwa. Miili ya vijana hao imechukuliwa na polisi na mimi nataka nifuatilie nijue ni vijana wa wapi,” ameongeza.
Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, Janeth Magomi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba upelelezi unaendelea ili kuwatambua vijana hao ambao bado hawajatambuliwa majina wala makazi yao, huku akilaani kitendo cha wananchi kujichukulia sheria mkononi.
“Ni kweli tumepokea taarifa ya kuuawa kwa watu wanne kwa kupigwa mawe na kuchomwa moto na wananchi wanaosemekana wana hasira kali na wamejichukulia sheria mkononi, mtaa wa Mhongolo Kahama, tunalaani vikali kitendo hiki maana kila mtu ana haki ya kuishi.”
“Tutahakikisha tunafanya msako mkali, nyumba kwa nyumba tunawakamata waliofanya kitendo hiki, kwa sababu hii tabia tukiiacha iendelee hapatakalika, kama mtu ni mkosaji inatakiwa itolewe taarifa ili vyombo husika vichukue hatua,”amesema.