Bunge lifanye marekebisho muhimu kabla ya kuvunjwa

Leo naanza kwa kumpongeza Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Tulia Ackson, kwa kutoa kauli ya wazi kuhusu mgawanyo wa madaraka baina ya mihimili mitatu ya dola.

Bunge, Serikali na Mahakama. Katika kauli yake, Dk Tulia alieleza dhana muhimu ya mgawanyo wa madaraka na mfumo wa kuwekeana mizani na udhibiti wa madaraka, dhana ambayo ipo kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ingawa utekelezaji wake umekuwa wa mashaka.

Spika Tulia alifafanua kuwa kazi ya Bunge ni kutunga sheria, Mahakama kutafsiri sheria hizo na kutoa haki na Serikali kutekeleza sheria pamoja na uamuzi wa Mahakama.

Alitoa kauli hiyo mbele ya Rais, Samia Suluhu Hassan ambaye ni mkuu wa Serikali na Jaji Mkuu mstaafu, Profesa Ibrahim Juma, wakati wa hafla ya kumuapisha Jaji Mkuu mpya Ikulu ya Chamwino, Dodoma.

Kauli hiyo imekuwa ikisisitizwa pia katika makala zangu za elimu ya Katiba, mara kwa mara nimeeleza kuwa mihimili yote mitatu, Serikali, Bunge na Mahakama, haijawahi kutimiza majukumu yake kikamilifu kwa mujibu wa Katiba.

Ikiwa kweli mihimili hii ingefanya kazi zake ipasavyo, leo hii Tanzania isingekumbwa na misukosuko ya kikatiba na kisiasa, wala hofu ya “kukinukisha.”

Kwa bahati mbaya, hali hii imezidi kuipa nchi taswira mbaya kimataifa, huku mashinikizo yakiongezeka kutoka Bunge la Ulaya, Marekani, Umoja wa Mataifa na sasa kuna hofu ya Mahakama ya Kimataifa ya uhalifu kuingilia kati.

Ibara ya 62 ya Katiba inaeleza kuwa kutakuwa na Bunge lenye sehemu mbili, Rais na Wabunge. Ibara ya 63 inatamka wazi kuwa Bunge ndicho chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano chenye mamlaka ya kuisimamia na kuishauri Serikali na vyombo vyake katika utekelezaji wa majukumu yao. Kazi kuu za Bunge ni mbili: kutunga sheria na kuisimamia Serikali.

Hata hivyo, hali halisi inaonyesha kuwa kazi ya kutunga sheria haifanywi kikamilifu na Bunge. Kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge (Ibara ya 80), miswada ya sheria imegawanyika katika aina mbili: miswada ya serikali na miswada binafsi.

Hii ina maana kuwa kivitendo, Serikali ndiyo inatunga miswada ya sheria na kuwasilisha Bungeni kwa ajili ya kujadiliwa na kupitishwa na Bunge hubaki kama mhuri tu wa kuhalalisha miswada hiyo.

Si mara moja au mbili Bunge limepitisha sheria ambazo baadaye zimetenguliwa na Mahakama kwa sababu ya kwenda kinyume na Katiba.

Swali ni hili, inawezekanaje Bunge lenye wasomi wa sheria wa kiwango cha juu, likiongozwa na Spika ambaye ni msomi mahiri wa sheria, linawezaje kutunga sheria ambazo ni batili kikatiba?

Jibu ni kwamba, sheria hizo batili zilitokana na muswada uliotungwa na Serikali kabla ya kuwasilishwa Bungeni.

Kwa msingi huo, hata kama Bunge ndilo lililopitisha sheria, mzizi wa matatizo upo kwenye upande wa Serikali, ambayo ndiyo ilianzisha muswada huo batili.

Kwa mujibu wa kanuni ya kuheshimiana kati ya mihimili, Bunge hupokea miswada hiyo, huijadili, na hatimaye kuipitisha, kisha huwasilishwa kwa Rais kusaini ili kuwa sheria.

Kwa kuwa Rais si lazima awe mwanasheria, hawezi kubeba lawama kwa kusaini sheria ambazo kimsingi ni batili.

Mahakama nayo, licha ya mamlaka yake ya kutengua sheria batili, haijawahi kuwawajibisha waliohusika kutunga miswada hiyo yenye dosari. Kwa nini? Kwa sababu ya hofu au kuheshimiana kupita kiasi kati ya mihimili.

Hivyo wito wangu, tunapokaribia Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu, bado kuna muda wa kutosha kwa Bunge kufanya marekebisho muhimu ya kikatiba na kisheria.

Marekebisho hayo yameelekezwa wazi na Mahakama ya Rufaa kupitia hukumu ya kuruhusu mgombea binafsi. Bunge lina wajibu wa kuitekeleza hukumu hiyo kabla ya kuvunjwa.

Kwa msingi huo, natoa wito kwa Spika wa Bunge, Dk Tulia kutumia nafasi yake kuongoza Bunge kutekeleza hukumu hiyo. Hii ni fursa ya pekee ya kurejesha imani ya wananchi kwa Bunge na kuheshimu mamlaka ya Mahakama.

Marekebisho hayo pia yatasaidia kuihalalisha Tume Huru ya Uchaguzi (INEC). Hivi sasa sheria iliyoiunda INEC haina msingi wa kikatiba kwa sababu Bunge halina mamlaka ya kuanzisha tume hiyo kwa mabadiliko ya kawaida ya sheria. Ni lazima kwanza iwekwe ndani ya Katiba, kisha sheria ifuate.

Kwa hiyo, kabla ya Bunge hili kuvunjwa, litimize wajibu wake wa kikatiba na kuheshimu uamuzi wa Mahakama ili taifa liweze kuwa na uchaguzi wa haki, huru na halali kikatiba.

Related Posts