Dar es Salaam. Tuko timamu kwa uchaguzi mkuu 2025, ndio kauli ambayo Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) kinajipambanua nayo, baada ya kufanya mikutano ya hadhara katika kanda nne kukiandaa chama hicho na uchaguzi.
Katika kuthibitisha kimedhamiria kushika dola, Chaumma kinasema kamwe hakiwezi kususia uchaguzi kwakuwa si dawa huku kikisisitiza kuwa, “huwezi kumuachia nyani shamba la mahindi anaweza kumaliza shamba lote.”
Chaumma kimehitimisha ngwe ya kwanza ya Operesheni yake ya Chaumma For Change (C4C), kwa kufanya mikutano ya hadhara kwa Kanda nne kukiandaa chama hicho tayari kwa uchaguzi Mkuu wa Oktoba, baadaye mwaka huu.
Mbali na shabaha hiyo, C4C iliyozinduliwa Juni 3, 2025 katika viwanja vya Furahisha jijini Mwanza, ilikuwa na lengo la kutambulisha safu ya uongozi wa kitaifa wa chama hicho, pamoja na kupita kuziba ombwe kwa nafasi za uongozi ngazi ya mikoa zilizo wazi na kupokea wanachama wapya.

Katika ngwe hiyo ya kwanza, kanda nne zilizopitiwa na amsha amsha ya operesheni hiyo waliyokuwa wanatumia usafiri wa Chopa na magari ya kawaida ni Kaskazini, Victoria, Magharibi na Serengeti.
Siku ya uzinduzi wa kampeni hiyo, haikupata mvuto mkubwa uliotarajiwa na kuna walioanza kukikatia tamaa chama hicho, lakini kadri walivyokuwa wanaendelea kufanya mikutano hiyo, umma ulikuwa unajitokeza kwa wingi kuwasikiliza.
Mikutano waliyoanza kufanya mkoani Mara, eneo la Musoma Mjini, watu wengi walifurika na kichocheo kikubwa cha kujaza watu ilikuwa usafiri wa Chopa uliokuwa unatumika kama turufu ya kushawishi umma.
Mbali na Chopa iliyokuwa inatumia mbinu ya kufanya mizunguko mikubwa eneo la uwanja kutafuta usawa wa kutua, kishawishi kingine ni Mwenyekiti wa chama hicho, Hashim Rungwe, wengi walikuwa wanafurahia kumsikiliza kwa namna alivyokuwa anaifafanua sera ya Ubwabwa kutolewa bure kwa umma.
Kampeni hiyo iliyotumia siku 12, kuanzia Mei 3 hadi 14, 2025, miongoni mwa viongozi waliokuwepo ni pamoja na Kaimu Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara, Devotha Minja na wa Zanzibar Issa Abbas Hussein.

Wengine ni Katibu Mkuu wa chama hicho, Salum Mwalimu, Naibu Katibu Mkuu Bara, Benson Kigaila na Mkurugenzi wa Mawasiliano kwa umma, John Mrema na makada wengine wa chama hicho walionogesha mikutano hiyo.
Kupitia mikutano hiyo viongozi hao kwa nyakati tofauti walitoa elimu kwa umma juu ya sababu ya baadhi ya viongozi wao kukihama Chama cha Demokrasi na Maendeleo (Chadema) na kujiunga na Chaumma kuwa ni kutaka washiriki uchaguzi mkuu waweze kuchaguliwa na kuwawakilisha wananchi kwenye vyombo vyenye mamlaka likiwamo Bunge.
Sababu ya wao kushiriki uchaguzi
Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Bara, Kigaila alitaja sababu kuu tatu za kushiriki uchaguzi mkuu licha ya upungufu wa kisheria na mfumo usioweka sawa uwanja wa kisiasa kwa wagombea na vyama vyote vya siasa.
Sababu ya kwanza ni kutaka kushinda uchaguzi na kuongoza Serikali, akisema hilo ndilo lengo la msingi kwa chama chochote cha siasa.
“Sababu ya pili ni kukabiliana na CCM katika uwanja wa siasa ili kukizuia wagombea wa chama hicho kupita bila kupingwa,” anasema Kigaila.
Sababu nyingine ni kupata fursa ya kushiriki vikao vya kisheria na kikatiba ikiwemo bunge, kupigania mabadiliko ya Katiba, Sheria na mifumo ya kiuongozi.
“Mabadiliko ya Katiba na sheria hayapatikani mitaani kwenye vijiwe vya kahawa; mabadiliko yote ya kisheria yanapatikana kupitia bungeni. Sisi Chaumma tumeamua kushiriki uchaguzi tupate jukwaa la kupigania na kupata mabadiliko.”
Sababu nyingine ni chama hicho kinataka mabadiliko ya sheria ya muundo wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na Katiba mpya sambamba na mahitaji hayo yanapatikana kwa kupaza sauti bungeni.

“Kususa haiwezi kuwa dawa, huwezi kumuachia nyani shamba la mahindi, anaweza kumaliza shamba lote, Chaumma hatukubali hali hiyo tunaenda kupamba na CCM kwa kula nao sahani moja,” anasema.
Kaimu Makamu Mwenyekiti, Devotha Minja amewaomba Watanzania kukiunga mkono chama hicho ili kufanikisha lengo la kushinda uchaguzi na kuingia kwenye mabaraza ya madiwani ya halmashauri na bungeni kupigania mabadiliko chanya.
Amewasihi wanawake na vijana kukiunga mkono Chaumma ili kishike dola akiahidi kuwa endapo kitafanikiwa katika ndoto yake hiyo, kitabadilisha mfumo wa mikopo inayotolewa na halmashauri kuwezesha wengi kunufaika bila upendeleo.
Vijembe vilivyotawala mikutano
Mvutano baina ya Chaumma dhidi ya Chadema katika mikutano yote ya hadhara, ulitamalaki kwa viongozi kurushiana vijembe. Itakumbukwa wakati mikutano ya C4C ikiendelea, Chadema nao walikuwa wakiendelea na mikutano yao ya kunadi kampeni ya No Reform No Election.

Hivyo, katika mikutano hiyo, kila kiongozi aliyehutubia kwa nyakati tofauti, kila mmoja alirusha kijembe upande wa pili. Kuna hoja zilizoibuliwa na pande zote ikiwemo suala la usaliti, kununuliwa, njaa, kusaka vyeo na madaraka.
Zilikuwa zinatolewa kwa lengo la kujaribu kuteka umma uelewe kile wanachosimamia na kupuuza kile kinachoaminiwa na chama pinzani.
Kilichokuwa kinaendelea kwa vyama hivyo viwili ni mgongano wa mawazo kuhusu ushiriki wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2025. Hata hivyo, Chadema mpaka sasa kimewekwa kando na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), kwa kutosaini kanuni za maadili ya uchaguzi.
Chaumma kinaamini kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho kwa mazingira yoyote yale ni bora zaidi kuliko kuiacha CCM ishinde bila kupingwa.
Chadema kinaamini kulingana na mazingira ya mifumo ya Uchaguzi iliyopo haitoi uwanja sawa wa kuchuana na kupatikana mshindi halali, ndiyo maana kinashikilia msimamo wake wa ‘No Reforms No Elections'(bila mabadiliko hakuna Uchaguzi.
Chimbuko la hayo yote ni kumeguka kwa Chadema baada ya kundi kubwa la viongozi lililokuwa haliamini katika bila mabadiliko hakuna uchaguzi kuamua kuhamia Chaumma, likidai ni lazima kushiriki uchaguzi mkuu.
Tangu hapo, wawili hao wamekuwa mahasimu wa kisiasa kwa kila mmoja kutoka mbele ya umma kutoa kejeli kwa mwenzake na kutoa elimu ili waelewe wanachosimamia ikiwa ni njia ya kutaka kwenda kushinda dola.
Dk Malisa alivyoibukia Chaumma
Katika hali isiyokuwa ya kawaida,aliyekuwa kada wa CCM, Dk Godfrey Malisa aliibukia kwenye mkutano wa C4C huku akisema hawezi kuwa muoga na kubaki nyuma katika kupigania mdororo wa demokrasia nchini.
Dk Malisa alivuliwa uanachama wa CCM, Februari 10, 2025, na kugeuka gumzo kwa tuhuma za kukiuka katiba na maadili ya chama hicho taarifa ambayo ilitolewa na katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Mercy Mollel.

Hatua ya kufukuzwa Malisa ilitokana na kauli alizokuwa akizitoa kupinga maamuzi ya Mkutano mkuu wa chama hicho Taifa uliofanyika Januari 19, 2025 akidai uamuzi wa kupitisha mgombea Urais wa chama hicho ulikiuka katiba ya CCM.
Dk Malisa aliibuka kwenye mkutano wa C4C, uliofanyika Moshi Mjini, anasema suala la mdororo wa demokrasia nchini ni janga ndani ya CCM na nje ya chama hicho, kulimaliza hilo jamii haipaswi kuwa na uoga katika kukabiliana nalo.
“Tatizo kubwa tulilonalo Tanzania ni ukosefu wa demokrasia na shida hiyo si ya CCM pake yake hata huku nje kwa vyama vya upinzani hakuna demokrasia na hao waliotoka Chadema kuja Chaumma ni mivurugano ya demokrasia ndani ya chama,” anasema Dk Malisa.
“Kelele yangu kubwa ni kudai haki na demokrasia ya kweli na hata hapa ningesimama ningesema jambo hilo hilo hatuwezi kwenda kokote bila kupigania demokrasia na kuwaambia vijana waache uoga,” anasema.
Dk Malisa aliyekuwa amekaa jukwaa kuu la viongozi wa Chaumma, anasema Tanzania haiwezi kubadilika kama wataogopa kusema ukweli na kuongeza:- “Tunaogopa kuuawa, kutekwa nimepiga kelele muda wote huu.”
Nchi hii haiwezi kubadilika kama tunaogopa kuuawa, kutekwa nimepiga kelele muda wote huu wananishangaa kuniona … ohoo hujaondoka niende wapi … ohoo mzee huogopi? namuogopa nani ?,” anasema Dk Malisa.
Chaumma na sera ya ubwabwa
Chama hicho, kimesema kikiingia madarakani kitaboresha sera ya kilimo ili wananchi wafanye shughuli hizo kwa tija na wapate chakula cha kutosheleza milo mitatu kwa siku.
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Chaumma, John Mrema anasema uhakika wa chakula siyo tu utajenga jamii yenye uwezo wa kufanya kazi na kuzalisha, bali pia utamaliza tatizo la utapiamlo kwa watoto.
Anasema Tanzania imejaaliwa kuwa na ardhi yenye rutuba, misimu miwili ya mvua na idadi ya watu, hivyo inafaa kuongoza mataifa yote ya ukanda wa Afrika Mashariki na kati kwa uzalishaji wa chakula kwa kuboresha sera ya kilimo kuwezesha wananchi kulima kwa tija. Mrema anasema nchi imejaliwa kuwa na mabonde yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji yenye kuwezesha kilimo cha mpunga kuwezesha taifa kuzalisha mchele wa kutosha.
“Ukosefu wa chakula husababisha utapiamlo, watoto wenye utapiamlo hawawezi kukua vizuri, na hata wakikua hawataweza kufikiri wala kufanya kazi sawa sawa,” anasema nakuongeza wakiingia madarakani.
“Chaumma itafuta kodi zote za VAT za asilimia 18 kwenye bidhaa ya chakula ili bei ya chakula ishuke kuwezesha wananchi kununua chakula na mafuta,” anasema.
Mrema anafafanua Taifa lenye watu wasiomudu kupata milo angalau mitatu kwa siku huzalisha jamii yenye udumavu na isiyoweza kuzalisha.
Kufuta mikopo ya kausha damu
Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Ukombozi wa Umma- Bara, Devotha Minja amewaahidi Wananchi mpango wao wa kuchukua dola ukitimia Oktoba Mwaka huu, chama hicho kitakuja na mkakati madhubuti wa kufuta mikopo ya kausha damu inayowatesa akina mama na kuwaingiza kwenye umaskini.

Anasema baada ya kufuta mikopo, watatumia mikopo ya asilimia 10 iliyotolewa na kila Halmashauri kulikopesha kundi hilo, kuliwezesha kufanya shughuli zake kwa uhuru tofauti na ilivyo sasa fursa hiyo wananufaika wake ni wachache na wahitaji wengi hawafikiwi. Minja anasema kama kiongozi mwanamke anaumizwa anaposhuhudia kila uchwao madhila wanayopitia kuhangaika kufanya marejesho ya mikopo ya kausha damu.
“Kila mahali ukipita wanawake hawana furaha waliowengi wanaumizwa na vikoba, kausha damu ndugu zangu unakopa Sh50,000 baada ya wiki moja unaenda kulipa Sh10,0000.
“Chaumma tunasema tukishika dola asilimia 10 zinazotolewa na Halmashauri zitaenda kutibu jambo hili,” amesema Minja.
Anasema mikopo hiyo inaongeza umaskini kwa kundi hilo na jamii nzima na likiachwa hali itazidi kuwa mbaya.
“Hata vijana wetu hawana kazi wasingekuwa Wachina wanaleta hizi pikipiki ingekuwaje, hatupaswi kuwaza kuchukua kodi pekee lazima uangalie na namna ya kumkuza kija kiuchumi ili kutengeneza usawa,” anasema.
Kulingana na Minja anasema ili wafanikishe mpango huo ni lazima kwanza waungwe mkono na wananchi katika uchaguzi mkuu kwa kuwapigia kura waweze kupata madiwani na wabunge na rais wakaunde serikali iwe njia ya kurudisha tabasamu kwa kundi hilo.
“Mpango huu utaenda sambamba na sera yetu ya ubwabwa ya kudhamini afya ya wananchi, wekeni Chaumma madarakani nawaahidi tunaenda kuondoa hizi kaushadamu. kaushadamu tunaenda kufuta kabisa na kuweka sheria kali ya kuzuia,” anasema.