Chuya haikosi kwenye pishi ya mchele

Mara nyingi tumeona wakulima wadanganyifu wakiloweka mtama kabla ya kuupeleka kwenye mzani.

Wengine wamekuwa wakitia mchanga kwenye mazao ionekane kama vile mchanga uliingia bahati mbaya wakati wa kuvuna.

Lakini lengo lao ni kuongeza uzani na kupata faida kubwa kutoka kwa mnunuzi. Huu ni wizi kama wizi mwingine, na mhusika anafaa kuchukuliwa hatua anazochukuliwa mwizi.

Wapishi hawakosi kuuchambua mchele na kuondoa kila kisicho mchele kwenye ungo. Unaweza ukashangaa kumwona mpishi akihangaika na mchele usio na chuya hata moja. Ukimwuliza anachopoembua kwenye mchele usio na tone la mchanga, hata mwenyewe hajui. Lakini ni utamaduni tu; kama vile kuku anavyochakura ngani safi iliyomwagwa sakafuni.

Shughuli ndogondogo kama kusuka, kutwanga na kuchambua chakula hutumika kama sehemu ya starehe.

Shughuli ayayoifanya mpishi hapa haitofautiani na shughuli ya sekretarieti ya chama inavyochambua wagombea uongozi.

Chama chenye sekretarieti makini hutuletea viongozi wazuri, lakini mchezo ukiwa ni “butua twende” wapiga kura wataumizwa kwa makosa ya kuviamini vyama.

Vyama vingine havina shughuli isipokuwa uchaguzi, hivyo usitegemee viongozi watatatunza rekodi za wanachama wao badala ya kutafuta hela ya kula. Hili ninanolisema hapa halimhusu mpiga kura peke yake. Linaanzia kwenye vyama vya siasa vinavyowapitisha wagombea na kuwaleta mbele za wapiga kura. Ridhaa ya chama kwa mgombea ina nafasi kubwa kwa mpiga kura kuchagua kiongozi bora au bora kiongozi.

Pamoja na mgombea kujulikana na wananchi katika baadhi ya mambo, chama ndicho kinachomjua zaidi weledi wake kwa kuwa ndicho kinachomlea.

Kuna vyama havifanyi mikutano yao ya ndani wala kupanga mikakati ya kuimarisha chama. Suala la kuwatafutia wananchi viongozi bora si sehemu ya kazi zao za kudumu. Mpaka msimu wa uchaguzi unapowadia, wao ndio kwa kuhamasishwa na ruzuku hukutana.

Tena ukute wajumbe wa kamati wanapigiana simu siku husika kuulizana nani yuko wapi. Kinachoendelea hapo ni kupeleka wagombea ili mradi nao wawemo.

Wapiga kura wanajikuta wakilazimishwa kuwaunga mkono wagombea kwa heshima ya vyama. Wakati huohuo wapiga kura hao wanashiriki uchaguzi kama waliolazimishwa, kwani wanajikuta wakibebeshwa maswali yasiyo na majibu vichwani mwao.

“Mgombea wetu ni mtu wa aina gani? Je, aliwahi kuwa kiongozi hapo kabla? Uongozi wake ulikuwaje?” na maswali mengine yasiyo na idadi.

Katika hali hii, mpigakura asitegemee kuyapata majibu yake kupitia mgombea kwani kila anayewamba ngoma huvutia upande wake.

Mara zote wagombea wanaoletwa kwa mtindo wa kubutua wanakosa sera. Ni watu wanaojikweza kwa kupitia madhaifu ya wapinzani wao. Hata kama wao watawazidi kwa mapungufu, watahangaika kuwajazia kashfa wenzao ili wao waonekane wana afadhali.

Huo ndio unaokuwa mwanzo wa kampeni chafu na za visasi. Wananchi wasidanganyike na figisu za namna hii. Kama hali itaonekana kuwa hivi, kila mpiga kura atumie akili yake ya ziada kuamua. Wawe kama Jeshi la mtu mmoja; wawatambue wagombea viti wenye ahadi za uongo na kuwaepuka ili kuhakikisha wanafanya uamuzi sahihi wakati wa uchaguzi.

Ikumbukwe kuwa uchaguzi hufanyika baada ya miaka mitano, hivyo kufanya maamuzi mabaya kutawagharimu miaka mingine mitano.

Wakati huu dunia inaenda kwa kasi kubwa sana. Kuachwa nyuma na kasi hii ni kujinyima maendeleo na kuendelea kuwa tegemezi kwa muda mrefu ujao.

Hatuna nafasi ya kutegemea mikopo na misaada kwa sababu hao watoaji wameshabadilika mazima, na wanaendelea kubadilika kila uchao. Huu ni wakati wa kuwalazimisha viongozi wetu wafanye kazi tunazowataka kufanya. Hiyo ndiyo nguvu halisi ya kura zetu.

Wagombea waliowahi kuwania au kushika nafasi za uongozi hujulikana kwa ahadi walizotoa awali. Angalia iwapo walitekeleza ahadi hizo kwa wakati, kama sivyo watoe sababu zenye mashiko za kutokufanya hivyo.

Kama walishindwa kwa uzembe basi waachwe na wengine wapewe nafasi ya kufanya hivyo. Ndio maana nasema tutumie akili ya ziada maana hapa ndipo kwenye hatari kubwa ya kudanganywa.

Wapiga kura wawe makini sana wakati wa kumhoji mgombea. Wagombea wa kweli mara nyingi hutoa majibu ya kina na kueleweka wanapoulizwa maswali.

Wenye ahadi za uongo hujibu kwa maneno ya jumla na kuepuka maelezo ya kina. Majibu yanayohusisha “hali ya uchumi” au “mabadiliko ya tabianchi” yatolewe ufafanuzi kuonesha hali hizo ziliathiri vipi utendaji, na nini kinatarajiwa kufanyika kuzikabili.

Wananchi wafuatilie mijadala, makala, na taarifa za vyombo vya habari kuongeza uelewa wa hali ya uchumi na mabadiliko ya tabianchi.

Wagombea waongo watatumia hali hizo kama kichaka cha kujifichia, lakini mtu hawezi kukudanganya jambo unalolifahamu.

Pia wagombea wafuatiliwe kwa yanayosemwa juu yao, mara nyingi maoni ya wananchi hufichua udhaifu au ukweli kuhusu wagombea.

Mwisho mgombea atazamwe iwapo amewahi kuonesha juhudi binafsi katika kusaidia jamii hata kabla ya kugombea au amejitokeza tu wakati wa uchaguzi.

Kila kinachokuja kirahisi huondoka kama kilivyokuja; kama wagombea wetu wanaonekana wakati wa kuomba kura tu, basi tusitarajie kuwaona wakati wa kazi za kijamii.

Hao si viongozi bali “wasaka tonge” na “wachumia tumbo”. Waogopwe kama homa ya nyani.

Related Posts