Dar es Salaam. Jeshi la Polisi limevunja ukimya kuhusu taarifa za matukio ya utekaji na mauaji likitoa ufafanuzi wa matukio kadhaa yaliyoripotiwa kwa nyakati tofauti huku uchunguzi ukibaini kuwa mengi yakiwa ya kujiteka.
Mbali na kujiteka sababu nyingine zilizobainika ni wivu wa mapenzi, imani za kishirikina, kugombea mali, kulipiza kisasi, kwenda nchi nyingine kujifunza misimamo mikali na kukimbia mkono wa sheria baada ya kufanya uhalifu.
Taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi leo, Juni 18, 2025, kupitia msemaji wake, David Misime, imeeleza kuwa matukio mbalimbali ya watu kuripotiwa kupotea yamewasilishwa katika vituo vya polisi na kufanyiwa uchunguzi wa kina.
Katika baadhi ya matukio hayo, waliodaiwa kupotea wamepatikana wakiwa hai, huku wengine wakikutwa wamefariki dunia.
Aidha, uchunguzi umebaini kuwa katika baadhi ya matukio hayo, ushahidi unaonesha kuwa sababu kuu ya kupotea ilikuwa ni watu kujiteka wenyewe, kwa sababu mbalimbali ambazo bado zinaendelea kuchunguzwa.
Taarifa iliyotolewa leo Juni 18, 2025 kupitia kwa msemaji wa jeshi hilo, David Misime imetaja matukio ambayo yameripotiwa katika vituo vya polisi na uchunguzi wa kina kufanyika na walioripotiwa kupotea kupatikana wakiwa hai na wengine wakiwa wamekufa, hadi sasa ushahidi kwa baadhi ya matukio yameonesha sababu zake ni kujiteka.
Hata hivyo taarifa hiyo iliyoorodhesha na kufafanua matukio kadhaa ya mauaji na utekaji haikuhusisha matukio yaliyoibua mijadala mikali ikiwemo ya makada wa Chadema kama vile Mdude Nyangali aliyechukuliwa na watu wasiojulikana, Ali Kibao aliyekutwa ameuwawa baada ya kuchukuliwa na watu wasiojulikana na Deusdedith Soka ambaye hajulikani alipo hadi sasa.
Kuhusu matukio yote yaliyoripotiwa yakihusisha watu mbalimbali kupotea, taarifa ya msemaji huyo imeeleza kwamba uchunguzi bado unaendelea hadi pale ukweli utakapopatikana wa nini kilichowatokea.
Kwa upande wa matukio ambayo yalitokea na kuhusishwa na vitendo vya utekaji na wahusika wake bado hawajapatikana, jeshi la hilo limewataka ndugu, jamaa na marafiki wa watu hao kuendelea kuwa watulivu wakati vyombo vya dola vikiendelea na uchunguzi ili kubaini uhalisia wa matukio hayo.
“Ikumbukwe kuwa kitendo cha kusambaza taarifa za uongo ni kinyume cha sheria kwa mujibu wa kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao namba 14 ya mwaka 2015 na adhabu yake ni kulipa faini ya kiasi cha fedha kisichopungua Sh5 milioni au kifungo gerezani kisichopungua miaka mitano au vyote kwa pamoja.
“Hivyo ni vyema wananchi kutoa taarifa za kweli na zilizo sahihi ili zisaidie kupata ukweli wa tukio lililotokea kuliko kusambaza taarifa ambazo hauna uhakika nazo,” imenukuliwa taarifa hiyo.
Misime katika taarifa yake ameeleza kwamba kwa mujibu wa kifungu cha 117 cha Sheria ya Ushahidi Sura ya 6 marejeo ya mwaka 2022 na kifungu cha 161 cha Sheria ya Ndoa Sura ya 29 marejeo ya mwaka 2019, dhana ya mtu kuchukuliwa kuwa amekufa inapaswa kuthibitishwa na mahakama baada ya miaka mitano kupita kulingana na vielelezo na ushahidi utakaowasilishwa.
“Kumekuwepo na kuripotiwa kwa taarifa katika vituo vya Polisi na nyingine katika mitandao ya kijamii zikijulisha kwamba mtu au watu fulani wamepotea, hawaonekani au wamekamatwa na watu waliojitambulisha kuwa askari wa Jeshi la Polisi.
“Jeshi la Polisi linapopokea taarifa hizo, huanza uchunguzi kwa kukusanya ushahidi kutoka vyanzo mbalimbali ili kupata ukweli wa taarifa ya nini kilichotokea kwani hauwezi kusema moja kwa moja kuwa mtu aliyeripotiwa kupotea, kutekwa, kulazimishwa kupotea au kuuawa bila ya kumpata anayedaiwa kupotea na ushahidi wa kuthibitisha taarifa hiyo ya nini kilichomtokea, kama alitendewa uhalifu ni nani wahusika, kulingana na sheria, kanuni na taratibu”.
Baadhi ya matukio aliyoyatolea ufafanuzi ni la kutekwa mwalimu wa dini na kiongozi katika taasisi ya Islam Foundation iliyopo mkoani Singida Shekhe Zuberi Said Nkokoo (53).
Katika tukio hilo kupitia vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo mitandao ya kijamii kulisambaa taarifa za kutekwa kwa Shekhe huyo na watu aliowataja kuwa ni askari wa Jeshi la Polisi usiku wa Juni 2, 2025 akiwa na Sh42 milioni.
Misime kwenye taarifa yake ameeleza kuwa baada ya uchunguzi, inadaiwa kuwa Nkokoo hakuwa ametekwa bali alitengeneza tukio la uongo la kutekwa kwa madai ya kukimbia madeni aliyokuwa akidaiwa na watu mbalimbali ya Sh521 milioni.
Tukio lingine ni lililotokea Juni 7, 2025 katika Kijiji cha Mtakuja Kata ya Nanganga Wilaya ya Ruangwa likimhusisha Ritha Ndambalilo (41) mfanyakazi wa kituo cha kuuza mafuta cha Kampuni ya Specialized Petrol Station ya Mtwara, alikutwa ameuwa kwa kunyongwa na mtandio na kutupwa kando ya makarasha ya Wachina katika Kitongoji cha Nahungo Kijiji cha Mtakuja Kata ya Malolo Wilaya ya Ruangwa.
Taarifa za awali zilidai Ritha siku ya tukio alikuwa na fedha kwenye mkoba iliaminika ametekwa na watu wasiojulikana, lakini baada upelelezi ilidaiwa kuwa mtu huyo aliuwawa na Juma Salum Nyenje (49) aliyekuwa akimtumia kama dereva wake wa bodaboda.
Tukio lingine ni linamuhusu Regina Chaula (62) aliyekuwa na makazi Bahari Beach Kinondoni Dar es Salaam na nchini Denmark aliyedaiwa kuuawa na Fred Chaula na Bashiri Chaula kisha mwili wake kutumbukizwa kwenye shimo la maji taka.
Regina ambaye alikuwa na kesi za madai Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi dhidi ya watuhumiwa hao aliripotiwa kupotea ghafla Desemba 13, 2024 hadi Januari 18, 2025 mwili wake ulipokutwa kwenye shimo hilo la maji taka baada ya upelelezi wa Jeshi la Polisi. Watuhumiwa hao walikamatwa na kufikishwa mahakamani.
Novemba 11, 2024 lilitokea tukio lililomuhusu Deogratius Tarimo Mkazi wa Kibaha Mkoa wa Pwani, ambaye alionekana kwenye picha mjongeo akipambana na watu waliotaka kumteka ambao hata hivyo walishindwa kutekeleza adhima yao hiyo.
“Taarifa zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusiana na tukio hilo zilisema kuwa waliokuwa wanatekeleza uhalifu huo ni askari polisi. Uchunguzi ulibaini kuwa waliohusika sio askari polisi na chanzo cha tukio hilo ni wivu wa mapenzi. Watuhumiwa sita walikamatwa na kufikishwa mahakamani”.
Tukio lingine lililofafanuliwa kwenye taarifa hiyo lilitokea Agosti 24,2024 ambapo Saulo Samweli (44) mkazi wa Kijiji cha Hyderere Kata ya Hyderere Wilaya ya Mbulu, Mkoa wa Manyara alitoa taarifa ya uongo kwa kutumia simu ya mkononi kuwa ametekwa tangu Agosti 22, 2024 na watu wasiojulikana na kumpeleka Karatu Mkoa wa Arusha kwa lengo la kumtoa figo.
Hata hivyo, upelelezi ulibaini kuwa mtuhumiwa aliamua kutoa taarifa hiyo baada ya kutumia fedha za mahari ya mtoto wake wa kiume kiasi cha Sh280, 000 ambazo aliaga nyumbani kuwa anazipeleka ukweni.
Tukio lingine ni la Agosti 23, 2024 lililomhusisha Elia Mchome (3) mkazi wa kitongoji cha Kwedijava wilayani Handeni aliyeuwawa na kufukiwa ndani ya chumba.
Kabla ya kubainika kwa mwili wa mtoto huyo taarifa zilisambaa kuwa alikuwa ametekwa na watu wasiojulikana, hata hivyo mtuhumiwa aliyehusika na mauaji hayo alikamatwa na kesi ipo mahakamani.
Agosti 19,2024 Ezania Kamana (36) aliyetoweka bila kufahamika mahali alipokuwa, alikutwa akiwa ameuwawa na mpenzi wake aliyefahamika kwa jina la Abdallah Miraji Musa (42) kisha mwili wake kukatwakatwa na kuwekwa katika mifuko minne ya sandarusi na kutupwa maeneo ya Ununio. Mtuhumiwa alikamatwa, kesi ipo mahakamani.
Aidha, jeshi hilo lilipokea taarifa ya kupotea na kutekwa watu saba mkoani Singida, lakini uchunguzi ulipofanyika ilibainika kuwa watu hao ambao ni Samwaja Said (22) na wenzake waliuawa kwa kukatwa sehemu mbalimbali za miili yao kisha kunyofolewa baadhi ya viungo vya miili yao na kufukiwa kwenye mashimo tofautitofauti na waganga wa kienyeji waliofahamika kwa majina ya Saidi Haji Msanghaa (24) Mkazi wa Kijiji cha Migungu pamoja na Kamba Kasubi (34) wakishirikiana na wenzao 12.
Baada ya ufuatiliaji ilibainika miili mingine mitatu iliyofukiwa wilayani Chemba mkoani Dodoma na kufikisha jumla ya watu 10 waliouawa.
Julai 31, 2024 wafanyabiashara wawili wa Wilaya ya Songea, mkoani Ruvuma, Ray Hyera na Riziki Mohamed walidaiwa kutekwa baada ya kutoonekana kwa siku kadhaa bila taarifa huku simu zao zikiwa hazipatikani.
Upelelezi ulibaini kuwa watu hao waliuwawa na mganga wa kienyeji aliyefahamika kwa jina la Mtila Msua Ausi (29) Mkazi wa Ligunga Wilaya ya Tunduru, katika Pori la Mdingula Uwanja wa ndege kwa kuwanywesha sumu na yeye kuchukua pesa kiasi cha Sh15 milioni.
Tukio lingine lililoripotiwa Julai 3, 2024, likiwahusu watoto wawili mmoja miaka (12) aliyekuwa mwanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Busenga na mwingine miaka minane aliyekuwa mwanafunzi wa darasa la pili katika Shule ya Akiba English Medium iliyopo Wilaya ya Ilemela waliojiteka na kupanga nyumba eneo la Wilaya ya Nyamagana na kuanza kuwapigia simu wazazi wao kuwa wametekwa wako Buhemba mkoani Mara na watekaji wanahitaji Sh100,000
Siku hiyohiyo polisi ilipata taarifa za kutekwa John Mboge mkazi wa Goba Center aliyekuwa akitokea Benki ya CRDB tawi la Coco Plaza, mtu huyu alikamatwa na watu saba na kumuingiza kwenye gari kisha kudaiwa kumpora pesa. Watuhumiwa hao saba walikamatwa na kufikishwa mahakamani.
Tukio lingine ni la Juni 17,2024 lililotokea katika Kitongoji cha Kabyonda Kijiji cha Mulele kata ya Ruhanga tarafa ya Kamachumu Wilaya ya Muleba Mkoa wa Kagera, ambapo mtoto aliyefahamika kwa jina la Noela Asimwe (2.5) mwenye ulemavu wa ngozi aliripotiwa kutekwa na watu wasiojulikana.
Uchunguzi wa Polisi ulibaini kuwa mtoto huyo ameuawa kwa kunyongwa shingo na kunyofolewa baadhi ya viungo vya mwili ikiwemo mikono yote miwili kisha mwili wake kutupwa kwenye daraja ukiwa umefungwa kwenye mfuko wa sandarusi. Watuhumiwa tisa akiwemo baba yake mzazi walikamatwa, kesi ipo mahakamani.
Katika tukio lingine lililotokea Mei 15,2024 mtoto ambaye jina lake limehifadhiwa aliripotiwa kutekwa Mwanjelwa Ilomba mkoani Mbeya, ilidaiwa kuwa utekaji huo ulitekelezwa na Winfred Komba (36) mkazi wa Vingunguti Dar es Salaam kwa kushirikiana na mama mzazi wa mtoto huyo aitwaye Agnes Mwalubuli, ikiwa ni njama waliyopanga ili kumshinikiza baba mzazi wa mtoto huyo atoe fedha kiasi cha Sh20 milioni.
Watuhumiwa watatu walifikishwa mahakamani na mmoja alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela, mmoja alihukumiwa (mama mzazi) kifungo cha nje miezi 12 na mama ambaye mtoto alikutwa kwake aliachiliwa huru.
Februari 12,2024 Buki Kizigina (52) mkazi wa Magaoni Mkoa wa Tanga alidaiwa kutekwa na watu waliofahamika kwa majina ya Shilingi Saidi na Khalid Salim Mwarangi kwa madai ya kudhulumiana kwenye kinachodaiwa biashara zao za dawa za kulevya na kwenda kumficha katika eneo la Putin wilayani Pangani, watuhumiwa walikamatwa na kufikishwa mahakamani na Buki alipatikana akiwa hai.
Tukio lingine lilitokea Novemba 6,2024 katika Kijiji cha Kemondo Wilaya ya Bukoba, Mkoa wa Kagera ambapo Amri Abdulahan (21) mkazi wa Kashai Manispaa ya Bukoba aliyejiteka mwenyewe, kisha kutengeneza taarifa na kumdanganya baba yake mzazi kuwa ametekwa.
Uchunguzi wa polisi ulibaini kuwa Abdulahan alifanya hivyo kwa lengo la kujipatia Sh5 milioni hata hivyo alikamatwa na kufikishwa mahakamani ambapo alikutwa na hatia na kuhukumiwa kifungo cha nje miezi 12.
Taarifa hiyo ilihusisha pia tukio lililotokea Julai 15,2029 huko Gezaulole Kigamboni ambapo mfanyabiashara aliyefahamika kwa jina la Hamis Luongo (38) alimuua mke wake aliyefahamika kwa jina la Naomi Marijani (36) kisha kuuweka mwili huo ndani ya shimo alilochimba katika banda la kufugia kuku lililopo nyumbani kwao, na kuuchoma kwa kutumia magunia mawili ya mkaa kisha majivu kuyafukia shambani.
Kabla ya kubainika, mtuhumiwa huyo alisambaza taarifa kuwa mke wake huyo ametoweka na hajulikani alipo kwa kipindi kirefu hata hivyo, uchunguzi ulibaini kuwa chanzo cha mauaji hayo ni wivu wa mapenzi. Mtuhumiwa alifikishwa mahakamani na kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa.