Mwanza. Rais Samia Suluhu Hassan, ametoa maagizo manne muhimu mkoani Simiyu, likiwemo alilolielekeza Wizara ya Kilimo kuhakikisha kuwa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inafungua ofisi katika mikoa yote itakayohusishwa na mradi mkubwa wa umwagiliaji kutoka Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika.
Mradi huo unalenga kuwahudumia wakulima wa mikoa ya Kanda ya Ziwa na Kanda ya Magharibi, ambapo Rais amesisitiza utekelezaji wake ufanyike kwa kasi na kwa ufanisi mkubwa.
Rais Samia ametoa maagizo maalumu leo Jumatano, Juni 18, 2025, wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Bariadi.

Mkutano huo umehudhuriwa na makada wa CCM, mawaziri, wabunge, watendaji wa Serikali, wawakilishi wa taasisi binafsi pamoja na wananchi wa maeneo hayo.
Katika maagizo hayo, Rais Samia ameielekeza Wizara ya Kilimo kuhakikisha kuwa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inafungua ofisi katika kila mkoa utakaohusika na utekelezaji wa mradi mkubwa wa umwagiliaji unaotegemea maji kutoka Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika, kwa lengo la kuwahudumia wakulima wa mikoa ya Kanda ya Ziwa na Kanda ya Magharibi.
Aidha, Rais amesisitiza kuwa utekelezaji wa mradi huo uanze haraka ili kuchochea maendeleo ya kilimo katika maeneo hayo.

Kwa mujibu wa Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, mradi huo unatarajiwa kuhudumia jumla ya hekta milioni tatu katika mikoa yote ya Kanda ya Ziwa na Kanda ya Magharibi.
Waziri Bashe ameongeza kuwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa mradi huo tayari umekamilika, na kabla ya Julai 1, 2025, mshauri mwelekezi atakuwa amepatikana kwa ajili ya kuanza hatua za utekelezaji.
“Pamoja na haya yote umesema kuna mradi mkubwa wa umwagiliaji maji ambao utaenda sambamba na mradi wa usambazaji maji ndani ya mkoa (Simiyu), lakini tutakwenda mpaka Dodoma. Nataka Tume ya Umwagiliaji ofisi zake ziwemo ndani ya mikoa hii ambayo mradi huu wa maji utapita.”
“Kwa hiyo mbali ya taasisi zilizopo hapa, ofisi ya Tume ya Umwagiliaji maji iwepo ndani Simiyu na ndipo mradi huu utakwenda harakaharaka naomba ulichukue hilo,” amesema Rais Samia.

Rais Samia pia ameagiza wizara hiyo kuusimamia ushirika na kuufanyia mabadiliko hasa wa wakulima wa pamba ili wapate manufaa na tija ya kulima zao hilo.
Pia, ameagiza urejeshwaji wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri usimamiwe, akiwataka wahusika kulegeza masharti ili wahitaji wa fedha hizo wapewe na kujiendeleza kiuchumi. Aidha, ameahidi tatizo la maji Simiyu kuwa historia baada ya kesho kuzindua mradi mkubwa wa maji mkoani humo.
Aidha, Rais Samia ameagiza Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), pamoja na Waziri wa Ujenzi kuhakikisha wanakamilisha kwa haraka ujenzi wa daraja la Itembe lililopo mkoani Simiyu, sambamba na kuboresha miundombinu ya barabara, hususan ndani ya miji.

Pia, ameagiza kuwekwa kwa taa za barabarani ili kuruhusu wafanyabiashara kuendesha shughuli zao nyakati zote, ikiwemo usiku.
Katika sekta ya mifugo, Rais ameelekeza kuwa Ofisi ya Wakala wa Maabara ya Veterinari ya Mkoa wa Simiyu itumike katika kuongeza tija ya uzalishaji wa mifugo, hatua itakayowezesha kufungua fursa za soko kubwa la kimataifa kwa bidhaa za mifugo kutoka mkoa huo na maeneo jirani.
Kauli za mawaziri kuhusu mafanikio
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema Mkoa wa Simiyu ulikuwa miongoni mwa maeneo yaliyokuwa na shida kubwa ya maji miaka minne iliyopita, hali ambayo ilisababisha baadhi ya ndoa kuvunjika kutokana na kina mama kutumia muda mwingi kutafuta maji.

Amesema hali ya upatikanaji wa maji ilikuwa chini ya asilimia 25 mwaka 2021, huku maeneo ya vijijini yakikumbwa na uhaba mkubwa wa maji salama kwa matumizi ya binadamu.
Amesema kuwa mitambo ya kuchimba visima ilikuwa chakavu huku baadhi ya maeneo visima vilivyokuwa vinachimbwa vikitoa maji ya chumvi.
“Ulinipa maelekezo mahususi kama Waziri wa Maji, uliniambia wewe ni mama na huwezi kuvumilia kuona akinamama wa Bariadi, Simiyu na Tanzania wanapata shida ya maji. Unatambua baadhi ya kina mama walipoteza ndoa zao kwa sababu ya kwenda kutafuta maji na ukaenda mbali na kunitaka mimi Waziri wa Maji kwamba nikizingua utanizingua mchana kweupe,” amesema.

Amesema kuwa baada ya maelekezo hayo, alifanya ziara nchi nzima na alipokwenda Simiyu alipita majimbo yote na kubaini kuwa wananchi walikuwa katika dhiki kubwa ya maji, mifugo haikuwa na maji na maeneo mengi yakitegemea mabwawa yaliyokuwa yamekauka.
Amesema Serikali ilinunua mitambo ya kisasa ya kuchimba visima kuondokana na changamoto hiyo hivyo kufanikiwa kujenga miradi 97 kwa kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita, ambapo imetumia zaidi ya Sh93 bilioni na kuufanya mji wa Simiyu kuwa na upatikanaji maji wa asilimia 62 huku vijijini kukiwa na asilimia 71.
Amesema kuwa moja ya ajenda kubwa ya mikoa ya Kanda ya Ziwa ilikuwa ni matumizi ya maji ya Ziwa Victoria, na kwamba Serikali imetekeleza kwa kuhakikisha maji ya ziwa hilo yanawafikia wananchi wa mikoa hiyo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Masauni amesema zaidi ya Euro milioni 313 zimepatikana kupitia Mfuko wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi kwa juhudi za Rais Samia ambazo zimeanza kusaidia kukabiliana na changamoto ya maji na athari nyingine za mabadiliko ya tabianchi nchini, hususan mkoani Simiyu.
Masauni amesema mabadiliko ya tabianchi yamechangia kwa kiasi kikubwa ukame, mafuriko na mabadiliko ya hali ya hewa, hali inayochangia pia ukosefu wa maji safi na salama kwa wananchi wa mikoa mbalimbali.
“Changamoto ya maji hapa Simiyu na maeneo mengine imesababishwa na mabadiliko ya tabianchi. Athari hizi ni kubwa na zinasababishwa na shughuli za mataifa yaliyoendelea, lakini sisi ndio tunaumia zaidi,” amesema Masauni.
Naye Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema kuwa kanda maalumu ya viwanda (eneo maalumu la uzalishaji yaani industrial park) ya kwanza inajengwa mkoani Simiyu, ambapo hadi sasa Serikali imetoa Sh10 bilioni kwa ajili ya ujenzi huo.

Amesema Serikali itapeleka miundombinu yote muhimu ikiwemo maji, umeme na maghala, na jukumu la wawekezaji litakuwa ni kufunga mashine za kuzalisha marobota yatakayotumika nchi nzima.
Amesema uzalishaji utakapoanza, Serikali itapiga marufuku uagizaji wa nyuzi za kufungia tumbaku kutoka nje ya nchi, ambazo zimekuwa zikitumia zaidi ya dola milioni 20 kwa mwaka.
“Kuanzia sasa, nyuzi zote za kufungia tumbaku zitazalishwa hapahapa Simiyu. Vifaatiba vinavyotengenezwa kwa kutumia pamba pia vitazalishwa Simiyu,” amesema Bashe.
Ameongeza kuwa eneo hilo maalumu la viwanda litapewa ruzuku ya asilimia 20 ya gharama za umeme, na tayari viongozi wa mkoa huo wameombwa eneo ili ujenzi uanze na huduma za msingi kama maji na umeme zitapelekwa kwa haraka.

Bashe amesema kuwa Serikali tayari imepeleka matrekta 205 yenye thamani ya Sh12 bilioni kwa ajili ya kusaidia wakulima mkoani Simiyu, ambapo kila mkulima analimiwa ekari moja kwa gharama ya Sh35,000 chini ya mpango wa ruzuku.
Naye, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk Ashatu Kijaji amesema ndani ya Mkoa wa Simiyu Serikali imejenga mabwawa 27 na majosho 27 katika wilaya za mkoa huo yenye thamani ya Sh386 milioni.
“Tumejenga majosho haya ili tuendelee kuyafikia masoko ya kimataifa na kwa kujenga majosho haya na kupeleka dawa ya kuogeshea mifugo yetu kwenye kipindi chako cha miaka minne tumeweza kupunguza vifo vya wanyama wetu hasa ng’ombe kutoka asilimia 72 hadi asilimia 42,” amesema.