Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ametaka watafiti katika sekta ya afya, wataalamu na wapangaji wa sera kuwekeza kwenye tafiti zenye tija kwa Watanzania ili matokeo yake yafanye kazi kwenye utoaji wa huduma nchini.
Majaliwa ametoa kauli hiyo leo Jumatano Juni 18, 2025 wakati akifungua kongamano la 13 la Sayansi lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) lililowaleta pamoja wanasayansi, wanavyuo na watunga sera katika tawi la Mloganzila, jijini Dar es Salaam.
Kongamano hilo lenye kaulimbinu isemayo: ‘Kubadili mifumo ya afya Afrika, kuweka kipaumbele katika bunifu na utafiti katika kukabiliana na changamoto za afya zinazoendelea duniani’.
Kongamano hilo lina mpango wa kuweka mkakati wa kupambana na changamoto za sekta ya afya na kuishauri Serikali hata kama itahusisha kubadili sheria na kanuni, katika kutekeleza na kuimarisha mazingira bora ya afya nchini.
Akifafanua hilo, Majaliwa amesema kwa sasa sekta ya afya nchini na duniani kiujumla inakabiliwa na changamoto zenye kuhitaji mbinu mpya za kukabiliana nazo.
“Tunashuhudia ongezeko la kasi la magonjwa yasiyoambukiza yanayotokana na mitindo mibaya ya maisha, kama vile kisukari, saratani, magonjwa ya moyo, matatizo sugu ya upumuaji yanayosababisha vifo vingi, ulemavu na gharama za matibabu kwa wanafamilia na taifa kwa ujumla.

“Kwa upande mwingine dunia inakumbwa na mlipuko wa magonjwa ya kuambukiza kama vile Uviko 19, Ebola, Marburg na Mpox yanayotishia usalama wa watu,” amebainisha.
Katika kukabiliana na hali hiyo, Majaliwa ametaka wataalamu wa afya kuendelea kufanyika kwa tafiti zenye tija kwa ajili ya kutengeneza usalama wa watu sambamba na Watanzania wenyewe kuzingatia mtindo bora wa maisha, akisisitiza kuepuka ulaji usio sahihi.
“Wekezeni kwenye tafiti zenye tija kwa wananchi, zisiishie kwenye makabati tunahitaji kuona matokeo ya tafiti hizo yakifanya kazi kwenye utoaji wa huduma hapa nchini, kama kutengeneza sera na mipango ya utekelezaji ili kuleta mabadiliko halisi kwenye utoaji huduma ya sekta ya afya,” amesisitiza.
Katika hatua nyingine, Majaliwa amewataka Watanzania kufuata mtindo bora wa maisha hasa ulaji na ufanyaji mazoezi ili kuepuka maradhi yatokanayo na mtindo mbaya wa maisha.
“Wananchi waendelee kuhamasishwa kutumia vyakula bora kufanya mazoezi kufuata ushauri wa wataalamu wa afya, mtindo wa maisha wa kula kwa kujichana…chipsi kuku, soda unashushia na bia ni matatizo,” amesema.

Hata hivyo, amesema hamasa inayotolewa na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kuwataka Watanzania kufanya mazoezi kila siku ni muhimu. Akifafanua kuwa licha ya kitaifa kutengwa Jumamosi kuanzia saa 12 hadi saa 3 asubuhi kufanya mazoezi, lakini hazuiwi kufanya wakati wowote.
“Tutaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora hadi vijijini. Tunataka kuhakikisha usalama wa watu wetu popote walipo kwa kupata huduma bora za kiafya,” amesema.
Aidha, amewataka wataalamu wa sekta ya afya, wasimamizi na wahudumu kutumia teknolojia katika kutoa huduma ya afya ikizingatiwa kuwa matumizi yake kwa upande wa kujifunza yanaleta uelewa zaidi na utoaji huduma wa haraka.
Amesema Serikali inajikita katika matumizi ya teknolojia ikiwemo Akili Mnemba katika utoaji wa huduma ili kuhakikisha Watanzania wananufaika katika huduma za kiafya.
Pia, Waziri Mkuu ameipongeza MUHAS kwa juhudi na mchango wake katika sekta ya afya ikiwemo kufanya tafiti mbalimbali zilizosaidia kuboresha sera na miongozo mbalimbali ya afya, kuongeza vifaa, upanuzi wa matawi ya Mloganzila, Kigoma, matibabu ya kibingwa huku akiahidi ushirikiano zaidi.
Aidha ametaka taasisi zote za afya, vyuo vikuu kuwekeza kwa wataalamu wa afya, vifaa tiba kwa kushirikiana na Serikali na wadau wa maendeleo.
Katika kongamano hilo, Makamu Mkuu wa Chuo cha MUHAS, Profesa Appolinary Kamuhabwa amesema linawasilisha matokeo ya tafiti ili kuona kama kuna haja ya kubadili mifumo ya afya, matibabu au uchunguzi wa magonjwa.
“Baada ya kuwasilisha kuna kamati inayoratibu kwa kuchukua mapendekezo yote kila wasilisho kisha inatengenezwa bangokitita ili kutoa ushauri kwa Wizara ya Afya,” amesema Profesa huyo.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Daniel Mushi akimuwakilisha waziri wa wizara hiyo, Profesa Adolf Mkenda amesema kongamano hilo muhimu kwa sekta ya afya kwakuwa inawakutanisha wataalamu wa ndani na nje ya nchi.

“Teknolojia imeleta mapinduzi makubwa ndio maana wataalamu wanakutana kubadilishana maarifa kutokana na tafiti na teknolojia,” amesema Profesa Mkenda.
Amesema wataalamu wanapaswa kujipanga upya kutokana na ujio wa magonjwa yanayoibuka.