Mambo 10 ya kuzingatia vijana wanaojiunga JKT

Dodoma. Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Meja Jenerali Rajabu Mabele ametaja mambo 10 ambayo vijana waliojiunga na mafunzo kwa mujibu wa sheria, Operesheni Nishati Safi, wanayopaswa kuzingatia kwa kipindi chote cha mafunzo.

Mambo hayo ni kujiepusha na utovu wa nidhamu, wizi, utoro, ugomvi, uhusiano wa kimapenzi, siasa, uvutaji wa bangi, dawa za kulevya, unywaji wa pombe, kuheshimu dini ya kila mmoja na kutotoa siri.

Mafunzo hayo yaliyoanza leo Juni 18, 2025, yanaendeshwa kwenye makambi ya JKT Rwamkoma (Mara), Msange (Tabora), Ruvu na Kibiti (Pwani), Mpwapwa na Makutopora (Dodoma).

Kambi nyingine za JKT ni Mafinga (Iringa), Mlale (Ruvuma), Mgambo na Mramba (Tanga), Makuyuni na Orjolo (Arusha), Bulombora, Kanembwa na Mtabila (Kigoma), Itaka (Songwe), Luwa na Milundikwa (Rukwa) pamoja na Nachingwea (Lindi).

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo katika kikosi cha JKT 834, Makutopora jijini Dodoma, leo Juni 18, 2025, Meja Jenerali Mabele amewatoa hofu vijana hao kuwa jeshini hakuna mateso bali kuna mafunzo yanayolenga kuwafanya kuwa wakakamavu.


Amesema watawatengenezea utaratibu wa kutoa taarifa pale wanapoona kuna jambo linalokwenda ndivyo sivyo.

“Muwe tayari kueleza ama kujulisha mambo yoyote yatakayokwenda kinyume na taratibu za mafunzo…Msitishwe na mtu yoyote kwa maana ya Jeshi la Kujenga Taifa, mimi ndio niko juu na mimi ndiye niliyekwambia usitishwe na mtu yoyote,” amesema.

Meja Jenerali Mabele amewataka vijana hao kujiepusha na utovu wa nidhamu, tabia ya wizi, ulevi, utoro katika maeneo watakayotakiwa kuwepo kwa wakati wa mafunzo na ugomvi kwa kuwa wanataka kutengeneza kizazi kinachopendana.

Pia, amewataka kujiepusha na uhusiano wa kimapenzi kati yao wenyewe ama na watu wengine wakati wakiwa katika mafunzo hayo.

Meja Jenerali Mabele amewataka vijana hao katika kipindi chote watakachokuwepo katika mafunzo hayo, wasijihusishe na ushabiki wa vyama vya siasa.

Pia, amewataka kuheshimu dini za wengine wakiwa katika mafunzo hayo ili kujenga umoja wa kitaifa.

Meja Jenerali Mabele amesema watakuwa wakisomewa shughuli za kila siku za kikosi hicho ambazo haziruhusiwi kusomwa wala kufahamika na mtu aliye nje ya mafunzo hayo.

“Kama kijana tunakuandaa kutotoa nje siri za eneo lako, usitoe nje siri za mafunzo yako, tunakuandaa pia usitoe nje siri za taasisi yako. Tunaanza kidogokidogo baadaye inafika katika level (ngazi) ya Taifa kwa kutotoa siri ya Taifa lako,” amesema.

Kwa upande wa wakufunzi, Meja Jenerali Mabele amewataka kuwalea vijana hao kama familia zao kwa kutowatendea kile ambacho wasingependa watoto wao watendewe.

Kuhusu wazazi, Meja Jenerali Mabele amewashukuru kwa kuelewa umuhimu wa mafunzo hayo na kuwapeleka wakiamini kuna vitu watavipata, na hivyo vijana hao watakaporudi majumbani mwao wanatakiwa kuonyesha mabadiliko.

Mkuu wa Tawi la Mafunzo wa JKT, Kanali Longinus Nyingo amesema  vijana hao watapata mafunzo ya awali ya kijeshi ili kuwawezesha kuwa walinzi wa Taifa, kutambua na kuchanganua mabadiliko ya mara kwa mara ya sayansi na teknolojia na kujua namna gani ya kukabiliana nayo.

“Kuwafundisha kuwa wazalendo na wakati wote wawe tayari kulitumikia Taifa pindi wanapohitajika. Lengo jingine ni kuhimiza fikra endelevu za kizalendo pamoja na kuwapatia tunu mbalimbali za kupambana na kukabiliana na changamoto bila kuathiri sheria za nchi,”amesema.

Naye Mkuu wa Kikosi cha Makutopora JKT, Kanali Festo Mbanga amesema vitu vyote kwa ajili ya mafunzo hayo vipo na wakufunzi wameandaliwa vizuri kuhakikisha yanafuata vigezo na maelekezo yote yaliyotolewa.

“Nikuahidi kuwa vigezo vilivyowekwa kwa ajili ya kozi hii na taratibu zote zitazingatiwa ili tuendelee kuweka taswira nzuri ya mafunzo haya kwa vijana wa Kitanzania,”amesema.

Akiwasilisha bajeti ya mwaka 2025/26 bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Stergomena Tax alisema katika kuhakikisha vijana wote wa kidato cha sita wanapata fursa ya kujiunga na mafunzo ya JKT, miundombinu na makambi yanaendelea kuboreshwa.

Alisema hadi kufikia mwaka 2025, JKT imefikia uwezo wa kuchukua vijana 60,000 ukilinganisha na uwezo wa kuchukua vijana 40,000 mwaka 2021.

Related Posts