Dodoma. Serikali ya Tanzania haina sheria ya kuwalazimisha watoto kuwatunza wazazi wao pindi watakapozeeka.
Hata hivyo, itaendelea kufanya tathmini wakati wa utekelezaji wa sera ya wazee iliyoboreshwa ambayo ina tamko la kuwataka watoto kuwajibika kuwatunza wazazi, na endapo kutakuwa na umuhimu wa kuwepo na sheria maalumu kwa ajili hiyo.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Mwanaidi Hamisi leo Jumatano Juni 18, 2025, bungeni jijini Dodoma.
Mwanaidi alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Moshi Vijijini (CCM), Profesa Patrick Ndakidemi aliyeuliza lini Serikali itatunga sheria itakayojumuisha mtoto kuwatunza wazazi wake wakizeeka.
Katika swali la msingi, Profesa Ndakidemi ameuliza ni kwa nini Serikali isione haja ya kulazimisha watoto kumtunza mzazi wake akizeeka, badala ya kuweka tamko peke yake na kupanua wigo kwa watoa huduma.
Naibu Waziri amesema Serikali itaendelea kuwalea na kuwapatia matunzo wazee wasiojiweza ambao hawana familia na ndugu wa kuwatunza, kupitia makazi ya wazee na wasiojiweza 13 inayoyamiliki.
“Vilevile wizara itaanzisha mchakato huo wa sheria kama itaona inafaa ili kusaidia ulinzi wa wazee wetu,” amesema Mwanaidi.
Akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Matiko kuhusu kujenga vituo zaidi vya malezi, amesema Serikali itaendelea kufanya hivyo kwa kushirikiana na wadau ili kuongeza vituo hata kwa ngazi ya wilaya.