Mongella: Hata CCM vichaa hawakosekani

Simiyu. Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, John Mongella amesema katika boma la watu wengi na ukubwa wa Kanda ya Ziwa ambayo ni moja ya ngome kubwa za chama hicho, hawakosekani vichaa ambao wanakwenda kinyume na msimamo wa chama.

Amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni mwenyekiti wa chama hicho, kuwaachia vijana kazi ya kuwafunza adabu baadhi ya watu ambao amewaita ‘vichaa’.

Mongella ametoa kauli hiyo leo Jumatano Juni 18, 2025 wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara mjini Bariadi mkoani Simiyu katika ziara ya Rais Samia inayoendelea mkoani humo.

Akitolea mfano wa boma ambalo lina watu wengi, Mongella amesisitiza kwamba hapawezi kukosekana wenye nia ovu, huku akiwataka Watanzania kutobweteka kwani adui bado yupo.

“Niwaombe wana Simiyu na Watanzania, tusibweteke adui bado yupo na Mheshimiwa Rais, nakumbuka nilipokuwa mdogo, pale kwenye boma letu tulikuwa wengi, lakini nakumbuka kuna bwana mmoja alikuwa akili siyo nzuri sana na kwa sababu kwenye boma tulikuwa wengi, alikuwa kila siku anakula nyumbani,” amesema Mongella na kuongeza;

“Lakini siku moja akamwambia bibi, wewe siku moja nitakuua, kwa hiyo ikabidi wana boma pale vijana wamtulize kidogo kwa kumchapa viboko. Nataka kusema kwenye boma la watu wengi, kama hivi kwenye kanda hii, hakuwezi kukosekana vichaa mmoja au wawili, tunakuomba utuachie hawa watatokea vijana na wanaCCM kuwafundisha adabu,” amesema.

Mongella amemtoa wasiwasi Rais Samia na kumhakikishia kwamba Kanda ya Ziwa ni salama kwa chama hicho kutokana na mwitikio mkubwa ambao ameupata katika ziara yake mkoani Simiyu, huku wakitarajia mapokezi na mwitikio mkubwa zaidi katika ziara yake ya kikazi itakayoanza kesho Juni 19 hadi 21, 2025 mkoani Mwanza na kudhihirisha kwamba yeye ndiye chaguo la Watanzania.

“Nilichokigundua Mheshimiwa Rais, hawa watu tunaowaona wakati mwingine wanatubeza, mimi nipishane na baadhi ya wana CCM wenzangu, huwa tunawaona kama hawana akili, akili wanazo, katika utaratibu huu mtu mwenye akili lazima utabeza kwa sababu hakuna jambo la maana la kusema,” amesema Mongella.

Ameongeza kuwa: “Tumeona leo siku ya tatu wananchi kwa maelfu wakishiriki ziara yako, lazima mtu mwenye akili unajua hapa mchezo mechi imeisha na hapa kampeni hazijaanza, Rais anapita kwa wananchi wake kukagua aliyoyahidi, hatuko kwenye kampeni.”

Amesema Ilani ya chama hicho ya mwaka 2025-2030 itakuwa na mapinduzi makubwa katika kuleta maendeleo kwa wananchi kuliko ilivyo ilani ya sasa, huku akisisitiza kuwa kuna miujiza mikubwa inakuja.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Bariadi Mjini, Andrew Kundo (CCM) amesema jimbo hilo halimdai Rais Samia kwani amefanya maendeleo makubwa na wanachomdai ni kuchukua fomu ya kugombea urais.

“Moyo usiokuwa na shukurani hukausha mema yote sisi wana Bariadi tunasema haya ambayo yameshafanyika katika jimbo letu hatukudai, lakini kuna jambo moja tu ambalo tunaomba uridhie tukudai, Mama wana Bariadi tunakudai ukachukue fomu halafu mengine utuachie,” amesema Kundo.

Kundo ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji, amesema katika kipindi cha miaka mitano ya awamu ya sita, jimbo hilo limepiga hatua katika sekta ya afya ikiwemo ujenzi wa Hospitali ya Dutwa iliyogharimu zaidi ya Sh3 bilioni, ukarabati wa Hospitali ya Mkoa ya Somanda uliogharimu zaidi ya Sh1 bilioni, ujenzi wa vituo vipya vitano vya afya na zahanati zaidi ya 10.

“Wana Bariadi walioko mbele yako kitu kilichowavuta kuja kukuona wewe ni kwa sababu umetuheshimisha. Kwa kipindi cha miaka mitano ndani ya jimbo la Bariadi hakuna rekodi ambayo hujaivunja. Wanaotamani kukuona siyo kwa sababu wanakudai wanatamani kukuona kwa sababu wanataka kukushukuru ana kwa ana,” amesema Kundo.

Related Posts