NSSF yawatega waajiri, yatoa siku 14 wadaiwa sugu

Babati. Mfuko wa Taifa wa hifadhi ya jamii (NSSF) Mkoa wa Manyara, unatarajia kuanzisha operesheni maalumu baada ya siku 14 ya ukusanyaji wa madeni kwa waajiri wenye malimbikizo ya michango ya wafanyakazi wao.

Umesema lengo ni kuhakikisha haki za msingi za wanachama zinalindwa.

Hayo yamesemwa leo Jumatano, Juni 18, 2025 na Ofisa Matekelezo mkuu wa NSSF Mkoa wa Manyara, Amina Kassim alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Babati

Kassim amesema operesheni hiyo itafanyika kwenye wilaya zote tano za Mkoa wa Manyara.

Amesema watafanya ufuatiliaji wa karibu kupitia barua zote za madai, ziara za ukaguzi na mahojiano ya kikaguzi kwa waajiri wote wadaiwa. Amesema jumla ya waajiri 100 kati ya 559, wanadaiwa.

Kassim amesema operesheni hiyo maalumu inalenga kuhakikisha haki za msingi za wanachama wake zinalindwa kwa kusimamia kikamilifu uwasilishaji wa michango ya kila mwezi kwa wakati, kama inavyotakiwa na Sheria ya Hifadhi ya Jamii, Sura ya 50.

Akizungumzia kuhusu operesheni hiyo, ofisa huyo wa NSSF amesema itaongeza uwajibikaji wa waajiri katika kutekeleza wajibu wao wa kisheria.

Aidha, amesema itasaidia pia kukusanya michango yote inayodaiwa kwa ajili ya kuimarisha uendelevu na uhimilivu wa mfuko na kuhakikisha wanachama wanapata mafao yao kwa wakati.

Akizungumzia namna inavyoenda kutekelezwa, Kassim amesema itahusisha hatua mbalimbali ikiwemo kufanya ukaguzi kwa waajiri katika wilaya zote ili kubaini kiwango halisi cha michango ambayo haijawasilishwa na kutakuwa na ufuatiliaji wa karibu kupitia barua za madai, ziara za ukaguzi na mahojiano ya kikaguzi kwa waajiri wote waliobainika kuwa na madeni.

Amesema kwa waajiri watakaokaidi au kushindwa kuwasiliana na NSSF kwa ajili ya kuweka mpango wa ulipaji madeni, watachukuliwa hatua za kisheria.

Aidha, amesema NSSF inatoa wito kwa waajiri wote wanaodaiwa kufika katika ofisi zao ndani ya siku 14 na kuweka utaratibu wa ulipaji kabla ya hatua kali kuchukuliwa.

Amekumbusha kuwa mwajiri kushindwa kuwasilisha michango hiyo kwa wakati ni kosa la kisheria linaloweza kusababisha adhabu mbalimbali ikiwemo faini, riba na hata kufikishwa mahakamani.

Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti kuhusiana na hatua hiyo, baadhi ya wafanyakazi akiwamo Adrian Doto ameipongeza NSSF kwa kuanzisha operesheni hiyo.

Amesema itasaidia kuhakikisha wafanyakazi wanapata mafao yao stahiki huku akisisitiza umuhimu wa operesheni hiyo kuwa endelevu kwa waajiri wote ili kuondoa usumbufu kwa wafanyakazi.

Naye mkazi wa mtaa wa Mji Mpya, Halima Iddy amesema kama utaratibu huo utazingatiwa, waajiri wataanza kuwajibika ipasavyo kwa kuwasilisha michango ya wafanyakazi kwa wakati, jambo litakalosaidia haki kupatikana pindi wanapostaafu.

Related Posts