Moshi. Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Hashimu Rungwe maarufu Mzee wa Ubwabwa ambaye alikuwa amelazwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) ameruhusiwa baada ya afya yake kuimarika.
Rungwe ambaye alikuwa katika ziara ya operesheni ya C4C mkoani Kilimanjaro, alipata changamoto ya afya Juni 14, 2025 na kupelekwa KCMC kwa ajili ya uchunguzi wa kidaktari baada ya afya yake kuonekana imedhoofu.
Juni 14, 2025 afya ya kiongozi huyo ilibadilika na kuonekana amechoka walipokuwa wakitoka Wilaya ya Mwanga kwenda Wilaya ya Same kwa ajili ya kuhitimisha ziara yao eneo la Hedaru ambapo ilibidi kukatiza ziara hiyo na kupelekwa hospitalini hapo.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Juni 18, 2025 Makamu Mwenyekiti wa Chaumma Zanzibar, Issa Abbas Hussein amesema hali ya kiongozi huyo ni njema na tayari wameruhusiwa kutoka hospitalini hapo jana jioni Juni 17, 2025.
“Tunamshukuru Mwenyezi Mungu, kiongozi wetu yupo salama na afya yake imerejea katika hali yake ya kawaida na sasa tumeruhusiwa kutoka hospitalini,” amesema Issa.
Aidha, amesema kwa sasa wapo Dar es Salaam kujipanga kuendelea na majukumu yao ya kikazi kama kawaida.
Akizungumza Ofisa Uhusiano hospitali ya KCMC, Gabriel Chiseo amesema baada ya afya ya kiongozi huyo kuimarika, ameruhusiwa kuendelea na majukumu yake kama kawaida.
Operesheni hiyo ya C4C ilizinduliwa Juni 3, 2025 jijini Mwanza ikishirikisha viongozi mbalimbali wa Chaumma akiwamo Rungwe. Baada ya Mwanza walikwenda mikoa ya Mara, Kigoma, Tabora, Geita, Kilimanjaro na Arusha.