Dar es Salaam. Jua linapochomoza katika mitaa ya Kariakoo, kitakachoashiria siku mpya imeanza ni ngurumo ya magari na sauti za wachuuzi wa bidhaa, ambao baadhi hutumia vipaza sauti.
Katika mazingira hayo yenye kelele, Juma Seleman (25), huanza harakati za siku za ‘uwinga’ akiingia duka hili na lile kutafuta bidhaa kwa ajili ya wateja anaotafuta mtandaoni.
Winga kwa mujibu wa Kamusi Kuu ya Kiswahili ni fukuza kitu kitoke au kikimbie kutoka mahali fulani kisipotakiwa.
Hata hivyo, sasa linatumika kumtambulisha mtu wa katika ya wateja na wafanyabiashara; huyo ni mtu wa kati. Kwa uhalisia winga ni dalali.
Seleman katika mahojiano na Mwananchi hivi karibuni anasema uwinga ni kila kitu kwake. Kazi hiyo imemlea, imemvisha na imempa matumaini ya kesho iliyo bora.
“Nilipoacha shule nikiwa kidato cha nne kwa sababu ya matatizo ya kifamilia sikuwa na mahali pa kuanzia maisha. Wazazi wangu walifariki dunia kutokana na ajali ya barabarani, nikabaki kuwa mlezi wa wadogo zangu wawili.
“Niliamua kuja Dar es Salaam kutoka kijijini Mkuranga (Mkoa wa Pwani) nikiwa na matumaini na nguvu ya ujana. Siku ya kwanza mjini ilikuwa ya majaribu, nililala stendi ya mabasi, nikiwa sina pa kwenda,” anasema.
Akiwa hajui pa kuanzia, alikutana na kijana aliyemwelekeza kazi ya udalali wa bidhaa, kutafuta wapangaji na kuwatafutia watu mashamba au viwanja kwa ujira utokanao na malipo wanayofanya (kamisheni).
“Niliikubali kazi hiyo bila kusita, kwani haikuhitaji mtaji, bali juhudi na uaminifu,” anasema na kuongeza:
“Kazi haikuwa rahisi. Nilijifunza kuwa mdomo ndiyo silaha. Nilijifunza kuongea kwa ufasaha, kujua maeneo ya biashara na zaidi ya yote, kuwa mvumilivu. Mara nyingi nilikuwa nikikimbizana jua kali, kutoka duka moja hadi jingine nikitafuta mteja anayehitaji bidhaa au mfanyabiashara anayetafuta wateja.”
Seleman anasema: “Baada ya kufanya kazi hii kwa muda mrefu nikafahamiana na watu wengi. Nilijiunga kwenye mitandao ya kijamii, huko imekuwa njia ya kupata wateja. Hadi sasa sina biashara yangu ila siku si nyingi nitaanzisha,” anasema.
Kwa upande wake, Hassan Ramadhan (24), mkazi wa Mwananyamala jijini Dar es Salaam aliamua kuitumia mitandao ya kijamii kama njia ya kumuingizia kipato, akitangaza na kuuza simu kutoka kwa wafanyabiashara.
“Maisha yangu hayakuwa rahisi mwanzoni, nilijifunza jambo moja muhimu katika dunia ya sasa, ukitumia mtandao kwa akili unaweza kubadilisha maisha yako,” anasimulia.
Ramadhan anasema: “Siku moja, nikiwa napitia Instagram niliona kijana mmoja akitangaza anauza simu. Alikuwa amepiga picha nzuri, akaweka bei na akaandika ‘DM kwa maelezo zaidi.’ Hapo ndipo fikra ziliponijia kama yeye anaweza, kwa nini mimi nishindwe?”
Anasema: “Kesho yake nilimfuata rafiki yangu anayefanya kazi kwenye duka la simu Kariakoo. Nikamwomba anipe ruhusa nipige picha baadhi ya simu nitangaze mtandaoni kwa niaba yake. Tulikubaliana nikipata mteja atanipa kamisheni, nilianza kwa kutumia WhatsApp status, kisha Instagram na baadaye TikTok.”
Baada ya matangazo hayo ndani ya wiki moja akapata mteja wa kwanza aliyehitaji simu aina ya Iphone 11, alipompeleka dukani akainunua yeye akapata ujira wa Sh30,000.
“Ilikuwa hela yangu ya kwanza kutoka mtandaoni. Nilijua kuna fursa. Kazi haikuwa rahisi kila siku, wapo waliodhani ni utapeli. Nilianza kujifunza lugha ya mawasiliano, kupiga picha vizuri na kuandika matangazo yenye mvuto,” anasema na kuongeza:
“Baada ya muda nilijijengea jina, wateja walianza kuniamini kwa sababu situmii picha za uongo wala kusema uongo kuhusu bidhaa. Wateja wengine wako nje ya Dar, hunitumia hela nanunua simu kisha kuwatumia kwa njia ya mabasi.”
Anasema ana akaunti ya Instagram yenye wafuasi zaidi ya elfu 10, pia ana kundi la WhatsApp lenye wanunuzi na wauzaji simu, akilenga kuanzisha duka la simu na kufungua tovuti ya kuuza simu kwa njia ya mtandao.
Renata Ngaiza, mwanafunzi wa chuo yeye anauza vipodozi.
Kama ilivyo kwa mawinga wengine, Renata hana duka wala vipodozi isipokuwa ametengeneza uhusiano na wafanyabiashara wa bidhaa hizo ambao humtumia kuzitangaza na anapouza hulipwa ujira wake.
“Ninachofanya ni kujua kwa undani kuhusu bidhaa za vipodozi, halafu nawatangazia wateja ambao wengi wao ni wanafunzi wenzangu na marafiki nilionao kwenye mitandao ya kijamii,” anasema.
“Nimejenga uaminifu kwa wafanyabiashara ndiyo maana wanaweza kunipa bidhaa ninakaa nazo, wengi wanajua biashara ni yangu ila ukweli ni kwamba mimi ni winga,” anasema.
Renata anasema kutokana na mtandao aliotengeneza ataendelea na biashara hiyo atakapohitimu masomo kwa kuwa uwinga umekuwa ajira kwake inayomwezesha kuendesha maisha.
Shilwa Mboma ni miongoni mwa wafanyabiashara wanaowatumia mawinga, anakiri kuwa wana mchango mkubwa katika kutanua wigo wa biashara.
“Mawinga wanasaidia sana kwenye biashara changamoto zipo ingawa zinategemea na makubaliano yenu, kwangu wapo wanaokuja siwafahamu kabisa wanaomba kutangaza bidhaa na hawa ndiyo wazuri maana analipa kwanza ndiyo anachukua bidhaa.
“Wale ambao nawafahamu huwa wanachukua mzigo akishauza ndiyo analeta fedha. Yeye anapata kutokana na namna anavyouza ile bidhaa ukimpa bei anaongeza cha juu na ndiyo kinakuwa cha kwake. Wapo ambao pesa anayopata ni sawa sawa na faida ninayopata mimi mwenye bidhaa,”anasema Shilwa.
Mtaalamu wa uchumi, Fanuel Lyimo anasema licha ya kazi hiyo kuwa si rasmi, ina mchango mkubwa katika sekta za biashara, makazi na hata usafirishaji.
“Hilo neno winga linatumika kwa sasa ila tafsiri sahihi ni dalali. Udalali ni shughuli inayohusisha kuwa kiunganishi kati ya mteja na mhitaji wa huduma au bidhaa. Jijini Dar es Salaam, maelfu ya vijana na watu wazima hufanya kazi hii kwa lengo la kupata kipato cha kila siku,” anasema.
Lyimo anasema: “Katika wakati huu ambao kumekuwa na changamoto kubwa ya ajira, shughuli hii imekuwa mkombozi kwa vijana, tofauti na ilivyokuwa kwa wale madalali wa zamani ambao walikuwa wanabebwa na ujanja na maneno mengi hawa mawinga wengi wao ni vijana wenye elimu.”
Anashauri Serikali na wadau wa maendeleo kuangalia uwezekano wa kuirasimisha sekta ya udalali ili kuwasaidia wahusika kuwa na mfumo bora wa utambulisho, mikataba na ufuatiliaji wa haki zao.
Pia, anashauri ni muhimu kuwapa mafunzo ya huduma kwa wateja, ujasiriamali na matumizi ya teknolojia ili kuboresha kazi zao.
“Kwa vijana, udalali ni njia mojawapo ya kujiajiri. Badala ya kukaa bila kazi, wanaweza kujiunga na shughuli hii kwa uaminifu na nidhamu. Kwa kufanya hivyo, wanaweza kujenga maisha yao hatua kwa hatua,” anasema.
Anasema kuwapo kwa baadhi ya wanaojihusisha na kazi hiyo kutokuwa waaminifu inachangia watu kukosa imani na kuihusisha kazi hiyo na utapeli.
Kauli hiyo inathibitishwa na Ramadhan anayesema hukutana na watu wanaohusisha kazi yake na utapeli, huku akikiri wapo matapeli wanaojifanya mawinga.
“Ni kweli wapo wanaotangaza wanauza bidhaa fulani halafu uhalisia hana huo mzigo, mwisho wa siku anamwambia mteja atume fedha akishapewa unakuwa mwisho wa mawasiliano. Hawa ndio hutufanya wengine wote tuonekane matapeli licha ya kuwa tupo tunaofanya shughuli vizuri pasipo kuwa na makandokando,” anasema.
Edwin Buguzi, mkazi wa Temeke anasema mara kadhaa amekuwa akinunua bidhaa kupitia mawinga na hajawahi kupata changamoto.
“Watu wengi hawafahamu bidhaa nyingi zinazotangazwa mitandaoni zinauzwa na mawinga. Kinachotakiwa ni umakini kuhakikisha hauingizwi mjini, binafsi sijawahi kukutana na changamoto yoyote tangu nimeanza utaratibu wa kuagiza bidhaa,” anasema.
Buguzi anasema: “Kitu cha msingi ninachozingatia kabla ya kununua bidhaa lazima nimfuatilie huyo anayeposti kwa muda kujua kama kweli anafanya biashara na bidhaa anazo. Pia, akileta lazima niikague kuthibitisha ubora ninaotaka, ukifanya hivyo huwezi kuingia kwenye matatizo na mawinga.”
Maria Massawe anasema hana utaratibu wa kutumia madalali kwa sababu ya historia ya watu wanaotapeliwa.
“Sina utaratibu wa kutumia mtu wa kati, ninapohitaji kitu hasa hivi vidogo-vidogo ambavyo naweza kuvifuata mwenyewe dukani. Kila siku naoma watu wanalizwa mitandaoni, hivyo siwezi kuingia kwenye mtego huo. Nikipenda kitu kinachotangazwa nitatafuta lilipo duka niende nikakague na kulipia dukani,” anasema.
Wakili Bashir Yakubu anasema mawinga kama ilivyo kwa madalali wengine wanatakiwa kuwa chini ya Sheria ya Mikataba na kila dalali anapaswa kusajiliwa kwenye kitengo cha biashara cha halmashauri husika anayofanyia kazi.
Anasema Sura ya 345 ya sheria hiyo inawazungumzia ‘agents’ mawakala ambao ndio wanatambulika kama madalali na wanatakiwa kuweka wazi watu wanaowauzia au kuwasambazia bidhaa.
Anasema kinachoendelea sasa ni shughuli hiyo kufanyika kiholela na hilo linachangiwa na maendeleo ya teknolojia, ambayo mtu yeyote anaweza kuitumia mitandao na kujitangaza kama dalali.
“Hawa mawinga ndio wengi siku hizi huko mitandaoni kuliko hata wafanyabiashara wenyewe, shida ni kwamba wanafanya kazi bila kufuata taratibu. Usahihi ni kwamba nao wanatakiwa kusajiliwa na kuwa na mikataba ambayo itamlinda mnunuzi wa bidhaa,” anasema na kuongeza:
“Uholela unaoendelea sasa ndiyo unasababisha vitendo vya utapeli kutokea, wapo wanaotumia mwamvuli wa uwinga kuwatapeli watu kwa sababu anajua hakuna namna anaweza kufuatiliwa na kupatikana.”
Wakili Yakub anasema: “Halafu unapokuwa agent ni lazima kwenye usajili wako ijulikane unahusika na bidhaa gani, yule mtu anayekupatia anapaswa kujulikana. Haiwezekani wewe ukawa wakala wa kila bidhaa hapo ndipo changamoto zinapoanzia.”
Anatahadharisha kuwa uholela huo unaweza kuwaingiza wanunuzi matatizoni hasa inapotokea mali aliyonunua ni ya wizi au iliyopatikana baada ya kufanyika uhalifu.