Wabunge walalama wanaojipitisha majimboni, tozo kwenye gesi asilia

Dodoma. Wabunge wa Tanzania wameibana Serikali kuhusu kodi na tozo katika gesi asilia wakitaka isicheze na hilo kwani ndiyo injini ya uchumi.

Mbali na hilo, wabunge wameingia na kauli ya ‘hatukudai’ ambayo imeonekana kuteka mjadala wa Bunge wakati wakichangia Mpango na Bajeti Kuu ya Serikali 2025/26.

Wametoa kauli hizo kwa nyakati tofauti leo Jumatano Juni 18, 2025 walipokuwa  wakichangia Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka 2025/26 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka wa fedha 2025/2026 ambapo baadhi wamekejeli makada wanaojipitisha majimboni mwao.

Mbunge wa Muleba Kaskazini (CCM), Charles Mwijage amesema kutoza kodi katika sekta ya gesi asilia ni kucheza na injini ya uchumi badala yake akashauri Serikali kutafuta vyanzo vingine.

Amesisitiza kitendo cha Serikali kuweka tozo kwenye gesi kuna wakati kitakuja sababisha nchi ishindwe kutembea na kufanya hali iwe mbaya.

Mwijage aliyewahi kuwa waziri wa viwanda na biashara ameshauri Serikali kama inataka kuongeza mapato kwa kuweka ushuru kwenye samaki wanaoingia kutoka nje na kupunguza ushuru wa makaa ya mawe ili upate wateja wengi kutoka nje, lakini akaomba kukaa na wizara ili awape vyanzo mbadala.

“Gesi asilia ni usalama wa nchi hivyo Serikali isiweke ushuru wowote katika bidhaa hii ila wasaidiane kutafuta vyanzo vingine vya mapato vitakavyoisaidia nchi kuinua uchumi wake, hao wakubwa wanapigana kuna siku meli hazitatembea kabisa lakini tukiwa na gesi magari yetu yanaendelea kuwa barabarani,” amesema Mwijage.

Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Najma Giga amesema makusanyo ya kodi ni muhimu lakini utaratibu wa kukusanya uwe rafiki usioumiza.

Giga amesema mpango wa kufungia biashara siyo kitu chema kwani unawaumiza wafanyabiashara lakini akisisitiza wakipewa elimu ya ulipaji kodi inawezekana.

Wakati wabunge hao wakizungumzia mpango wa kodi, baadhi ya wabunge wamemmwagia sifa Rais Samia Suluhu Hassan wakisema hawana cha kumdai zaidi asubuhi ya Oktoba (siku ya uchaguzi mkuu) wampe tiki.

Mbunge wa Manyoni Mashariki (CCM), Dk Pius Chaya amesema kuna mambo mengi yaliyofanyika katika jimbo lake ambayo yanatokana na uamuzi wa kimapinduzi wa Rais Samia.

Dk Chaya amesema katika jimbo hilo hawana deni kabisa la kumdai Rais kwani ilani ya CCM imetekelezwa kwa vitendo na hawataki kumwangusha kwani wanamuhitaji tena kwa ajili ya maendeleo.

“Nataka Watanzania wafahamu, sisi anamanyoni hatuna tunachomdai mama, yeye ndiyo anatudai hapa, kuna mambo mengi yalikuwa yamesimama lakini katika kipindi cha mama huyu kila kitu kinakwenda vizuri ikiwemo daraja la siku nyingi la Sanza,” amesema Dk Chaya.

Kauli kama hiyo ilitolewa na Mbunge wa Iramba Mashariki (CCM), Isack Mtinga ambaye amesema jimbo lake linadaiwa na Rais Samia na kwamba Oktoba wanatarajia kulipa deni hilo kwa kumpa kura nyingi.

Mtinga amesisitiza wamekuwa na deni kwa Rais lakini ndani ya jimbo wao hawana cha kumdai kabisa kutokana na ukweli katika kipindi cha uongozi wake amefanya maendeleo makubwa akieleza amejenga historia kubwa.

Katika hatua nyingine, Mtinga amelalamika kuwa wako watu wanaojipitisha jimboni kwake wakigawa fedha kwa ajili ya kushawishi wachaguliwe kwenye ubunge, lakini akasema yupo imara na wananchi wake wanamwamini ndiyo maana yupo bungeni wao wanahangaika na jimbo.

“Mimi mbunge wenu nipo imara, naendelea kuwatetea huku jimboni lakini wao wako huko wanagawa elfu hamsini hamsini kwa wapiga kura, nawaambia hao ni wavamizi hawana maana yoyote naomba muwapuuze,” amedai Mtenga.

Malalamiko ya Mtinga yametolewa pia na Mbunge wa Nzega Vijijini (CCM), Dk Hamis Kigwangalla ambaye amesema jimboni kwake kuna watu wanajipitisha lakini hawatamuweza anachoamini atakwenda na Rais Samia Oktoba.

Mbunge wa Hai, Saashisha Mafuwe amesema mbali na viporo alivyobakiza katika jimbo lake lakini hakuna wanachomdai Rais Samia katika jimbo lao isipokuwa wanasubiri muda wa uchaguzi wakamalize kazi.

Hata hivyo, amejipigia chapuo akisema bado ni kijana mwenye nguvu na uwezo wa kuwatumikia wananchi, hivyo anaomba wananchi wampe ushirikiano ili arudi kwa mara nyingine kwenda kukamilisha baadhi ya miradi iliyobakia.

Related Posts