Wawakilishi wataka misamaha ya kodi izuiwe, wigo wa mapato uongezwe

Unguja. Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar wameitaka Serikali kupitia upya mfumo wa utoaji misamaha ya kodi na kuongeza juhudi katika usimamizi wa miradi ya kimkakati, ili kuhakikisha kuna matumizi bora ya rasilimali na kupunguza utegemezi wa wahisani katika bajeti.

Wakijadili Bajeti ya Serikali ya mwaka 2025/2026 ya Sh6.982 trilioni, wajumbe hao wameelezea wasiwasi kuhusu kiwango kikubwa cha fedha kinachopotea kupitia misamaha ya kodi, fedha ambazo zingeweza kusaidia utekelezaji wa miradi ya kijamii kama huduma za afya ya mama na mtoto.

Akizungumza leo Jumatano, Juni 18, 2025, kwenye Baraza la Wawakilishi mjini Unguja, Mwakilishi wa Chumbuni, Miraji Khamis Mussa amesema kuna haja kwa Serikali kuongeza kasi ya upatikanaji wa mapato ya ndani badala ya kutegemea wahisani.

Ametilia mkazo umuhimu wa kupanua wigo wa kodi kwa kuirasimisha sekta isiyo rasmi ili kuongeza mapato ya taifa.

Mwakilishi wa Mfenesini, Miraji Othman Said akichangia mpango wa Maendeleo na Bajeti Kuu ya Serikali wakati wa mkutano wa 19 wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar



Amesema mashirika ya umma yanapaswa kutoa gawio kama ishara ya ufanisi wake na amependekeza kuanzishwa kwa “Siku ya Gawio” ili kuonyesha uwazi wa mashirika yenye tija kwa Taifa.

Kuhusu misamaha ya kodi, Mussa amesema kwa upande mmoja inaweza kuwa mizuri au mibaya kulingana na matumizi yake.

Amesema Serikali imetoa misamaha ya kodi ya Sh119 bilioni kwa mwaka 2025/2026 ikilinganishwa na Sh66 bilioni mwaka uliotangulia, na kusisitiza haja ya kupunguza au kuondoa kabisa misamaha isiyo na tija.

Mwakilishi wa Malindi, Mohamed Ahmada Salum, ametilia shaka ongezeko la kodi katika saruji, akieleza kuwa maisha ya wananchi bado ni magumu na hawawezi kumudu gharama za juu za vifaa vya ujenzi.

Aidha, Othman Machano Said wa Mfenesini ameonya kuwa kuongeza kodi kwenye maji yanayoingizwa kutoka nje bila kuwa na uzalishaji wa kutosha nchini, kunaweza kuleta taharuki kwa wananchi.

“Ni muhimu kulinda viwanda vya ndani, lakini lazima tujiulize kama tuna uwezo wa kuzalisha vya kutosha kabla ya kuongeza kodi,” amesema Othman.

Ameongeza kuwa wakati wa kiangazi, maji ya ndani hayakuwa yanapatikana kwa uhakika, hivyo bei ya juu ya maji kutoka nje inaweza kuwaumiza wananchi.

Kwa upande mwingine, ameipongeza Serikali kwa uamuzi wa kuongeza ushuru kwenye bidhaa kama pipi na biskuti kwa lengo la kulinda afya za watoto.

Yahya Rashid Abdalla wa Kwahani, amesema Serikali inapaswa kupunguza utegemezi na kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani, ili kufanikisha miradi mikubwa ya kimkakati. Amesisitiza kuwa miradi hiyo itaongeza mapato, kuboresha miundombinu na kuinua ustawi wa jamii.

Akizungumzia uwekezaji katika miradi ya kimkakati, Abdalla amependekeza uende sambamba na maendeleo ya miundombinu, hasa maeneo yanayohusiana na utalii.

Amesema changamoto ya ukosefu wa upembuzi yakinifu na ulipaji fidia kwa wananchi, zikiachwa bila kushughulikiwa mapema zinaweza kusababisha matatizo.

Hivyo, ameitaka Serikali kufanya tathmini mapema na kulipa fidia ili kuepuka migogoro.

Naye Hussein Ibrahim Makungu, Mwakilishi wa Mtoni, amesema ipo haja ya Serikali kuwajengea walimu na madaktari nyumba bora za kuishi kutokana na umuhimu wao.

Akijibu hoja hizo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Fedha na Mipango, Dk Saada Mkuya, ameahidi kuzingatia mapendekezo yote yaliyotolewa na wawakilishi, akisema dhamira kuu ya Serikali ni kuhakikisha maendeleo na ustawi wa wananchi unapatikana kwa njia endelevu.

Amesema lengo la hatua zilizochukuliwa, kama kuongeza ushuru kwa baadhi ya bidhaa, si kuwaumiza wananchi, bali kulinda bidhaa na viwanda vya ndani.

“Tutaangalia namna ya kuboresha zaidi maeneo yote yaliyoibuliwa. Tunataka kujenga uchumi imara na wa kujitegemea,” amesema Dk Mkuya.

Related Posts