Morogoro. Ama kweli sheria ni msumeno hukata mbele na nyuma, ndio maneno unaweza kuyatumia kuelezea namna mzee wa miaka 70, Victory Rudongo, alivyojikuta akifungwa kifungo cha maisha jela bila kujali umri mkubwa alionao.
Kwa hukumu hii na kama atatumia haki yake kukata rufaa na akagonga mwamba na mahakama ya rufani ikabariki adhabu hii, maana yake umauti utamkuta mzee Rudongo akiwa gerezani labda tu kama atapata msamaha wa Rais kikatiba.
Hukumu hiyo imetolewa Juni 17, 2025 na Jaji Sedekia Kisanya wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Masjala ndogo ya Morogoro na nakala yake kuwekwa katika mtandao wa mahakama leo Juni 18.
Mzee huyo amepatikana na hatia ya kukutwa na kilo 202 za bangi, tukio lililotokea usiku wa manane wa Julai 28, 2023 katika eneo la Mbakana katika kijiji cha Mgeta katika wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro.
Katika utetezi wake mzee Rudongo, maarufu Kalori, alikanusha mashitaka yaliyokuwa yakimkabili na kujitetea kuwa yeye anaishi kijiji cha Mgeta kata ya Luwale iliyopo kitongoji cha Kasangala A na kukanusha eneo alilokamatiwa.
Aliieleza mahakama kuwa Julai 28,2023 usiku, akiwa amelala katika makazi yake, alivamiwa ghafla na kukamatwa na kundi la watu walioingia katika nyumba yake ambao baadaye alikuja kuwafahamu kuwa walikuwa maofisa wa Polisi.
Mzee huyo aliiambia Mahakama kuwa hakukamatiwa katika kijiji cha Mbakana kama ambavyo ushahidi wa upande wa mashitaka unavyodai, na wala hafahamu kijiji cha Mbakana kilipo na kukanusha vikali kukutwa na bangi.
Aliieleza Mahakama kuwa alilazimika kuheshimu maagizo aliyopewa na Polisi waliomkamata kwa vile walikuwa wengi na walimpa vitisho hasa baada ya kufyatua risasi mbili hewani, na kudai hana hatia na kuomba aachiwe huru.
Ushahidi unaonyesha kuwa Julai 28, 2023, wakati maofisa kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), wakifanya operesheni eneo la Kisaki huko Morogoro, walipokea taarifa fiche kutoka kwa raia mwema.
Inspekta Wamba Msafiri aliyekuwa shahidi wa tano, ndiye aliyepokea taarifa hiyo ya kiintelijensia kwamba kuna mtu anajihusisha na ulimaji na usafirishaji wa bangi na kuwajulisha maofisa wenzake akiwamo shahidi wa pili, Seleman Mbwambo.
Saa 6:05 usiku walianza safari kuelekea kijiji walichoelekezwa na baada ya kufika na kukutana na mtoa taarifa wao, walianza safari kuelekea katika eneo hilo kililopo kijiji cha Mbakana ambapo walifika saa 9:00 alfajiri.
Inspekta Msafri aliieleza kuwa eneo lenyewe lilikuwa halifikiki kwa usafiri wa gari na kulikuwa hakuna kiashiria kuwa linaishi binadamu, hivyo waliamua kuacha magari na kutembea kwa miguu na njiani walishuhudia mashamba ya bangi.
Baada ya kufika katika eneo la tukio waliona kichanja kikiwa kimezungushiwa chandarua kwa ajili ya kuzuia mbu, ambapo walikizingira na kufanikiwa kumkamata mshitakiwa akiwa ndani ya kichanja hicho amelala.
Maofisa hao walifanya upekuzi katika mazingira ya eneo hilo ambapo Inspekta Msafiri aliona turubai likiwa limezungukwa na majani na wakashuku itakuwa ni bangi, ambapo walimuuliza mshukiwa naye akawathibitishia ilikuwa ni bangi.
Taratibu za ukamataji zilifanyika kwa kujaza nyaraka muhimu za kisheria ambapo siku iliyofuata yaani Julai 29,2023, sampuli za majani zilizokamatwa zilipelekwa Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali na kuthibitishwa kimaabara kuwa ni bangi.
Ni kutokana na ushahidi huo, Jaji alimuona mzee huyo ana kesi ya kujibu na kumpa nafasi ya kujitetea kwa kiapo ingawa utetezi wake ulikataliwa.
Hukumu ya Jaji ilivyokuwa
Katika hukumu yake, Jaji Kisanya alisema Jamhuri walikuwa na wajibu wa kisheria kuthibitisha kuwa mshitakiwa ndiye aliyepatikana na dawa hizo na pili kiasi alichokamatwa nacho ni kilo 202 kinachozidi kilo 100 za kiwango cha kisheria.
Jaji alisema ni wajibu wa Mahakama yake kujibu hoja tano ambazo ni pamoja na kama mshitakiwa alikamatwa Mbakana akiwa na turubai lenye dawa hizo na kama upekuzi uliofanyika wakati wa kumkamata ulikuwa ni kwa mujibu wa sheria.
Hoja nyingine ni pamoja na kama majani yale yaliyopatikana katika turubai yalithibitishwa ni bangi, kama uteketezaji wa dawa hizo ulizingatia sheria na kama mnyororo wa makabidhiano ya vielelezo haukukatika.
Akichambua ushahidi kujibu hoja ya kwanza, Jaji alisema ushahidi wa shahidi namba 2 na 5 ulithibitisha na unaaminika, ulielezea namna mshitakiwa alivyokamatwa na dawa hizo katika eneo la Mbakana, akiwa amelala.
“Mshitakiwa hakuwahi kutoa mahali popote, madai kuwa alikamatwa kijiji cha Luwale hadi siku anapotoa utetezi wake kortini. Huu ushahidi haukuwekwa mbele ya shahidi wa pili na wa tano ambao wanasema walimkamata Mbakana,”alisema Jaji.
“Kitendo cha mshitakiwa kushindwa kuwadodosa mashahidi hao muhimu wa Jamhuri katika jambo muhimu kama hilo kunafanya utetezi wake usiaminike na uonekane kama ni njia ya kujinasua tu na shitaka linalomkabili.”
“Hakuna dalili zozote za kuwapo kwa ugomvi kati ya mshitakiwa na mashahidi hao muhimu wa Jamhuri kiasi kwamba wamtungie hadithi ikiwamo ya kusafiri kutoka Dar es Salaam hadi kijiji cha Luwale ili tu kumbambikia kosa la dawa za kulevya.”
“Ni kwa ushahidi uliopo, sioni msingi wa kutoamini ushahidi ulio wa wazi wa mashahidi hao wawili ambao walisimama imara kuthibitisha mshitakiwa alikamatwa kijiji cha Mbakana akiwa na dawa hizo za kulevya,” alieleza Jaji.
Kuhusu upekuzi kama ulizingatia sheria, Jaji alisema ushahidi unaonyesha mashahidi hao walisafiri na kufika eneo la tukio usiku wa manane na ni porini katikati ya mashamba hivyo isingekuwa rahisi kupata shahidi huru kushuhudia.
“Baada ya kupima ushahidi dhidi ya vigezo vya kisheria, naona upande wa mashitaka umeweza kuthibitisha kuwa upekuzi na ukamataji wa dawa hizo ulizingatia sheria. Hati ya ukamataji ilisainiwa na mshitakiwa pia,”alisema Jaji.
Jaji alisema ushahidi wa shahidi wa tatu aliyeandaa kielelezo namba saba ambacho kilipokelewa mahakamani, ulithibitisha uchunguzi wa kimaabara uliofanywa na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kuwa sampuli ilikuwa ni bangi uzito kilo 202.
Katika hitimisho lake, Jaji alisema mshitakiwa ana hatia kama alivyoshitakiwa na anamuhukumu kifungo cha maisha licha ya kwamba umri wake umeenda (miaka 70), kwa kuwa hiyo ndio adhabu ya lazima kwa kosa alilolitenda.