Dar es Salaam. Kiasi cha Sh916.7 bilioni kimetengwa kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2025/ 2026.
Fedha hizo zitawanufaisha jumla ya wanafunzi 99,620 wa mwaka wa kwanza katika ngazi za diploma, shahada ya kwanza na shahada za uzamili.
Akizungumza leo Alhamisi, Juni 19, 2025 wakati wa kutangazwa kufunguliwa kwa dirisha la uombaji mikopo kwa mwaka wa masomo 2025/2026, Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Dk Bill Kiwia amesema wanafunzi 88,000 wa shahada ya kwanza watapangiwa mikopo hiyo.
Amesema idadi hiyo ni ongezeko la wanufaika 8,000 ikilinganishwa na mwaka wa masomo 2024/2025 ambapo wanufaika 80,000 walipangiwa mikopo.
Kwa upande wa wanafunzi wa diploma amesema mwaka huo wa masomo wanufaika 10,000 watapata mikopo hiyo ikiwa ni ongezeko la wanufaika 3,000 ikilinganishwa na ilivyokuwa katika mwaka wa masomo uliopita.
Amesema fedha hizo zitatumika pia kwa wanafunzi 173,783 wanaoendelea na masomo.
“Tunazidi kuongeza wigo wa wanafunzi wanaopata mikopo, mwaka huu hata wanafunzi wa diploma idadi yao imeongezeka hapa lengo ni kuhakikisha kwamba wanapata elimu bila kujali hali zao,” amesema Kiwia.
Akizungumzia hilo, Mdhibiti Ubora Mkuu wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), Kassim Ndumbo amesema baraza hilo linaguswa na hatua mbalimbali zinazochukuliwa kuhakikisha wanafunzi wa vyuo vya kati nao wanapata mikopo.
“Tulikuwa na vijana wengi huko vyuoni wakati mwingine wanalazimika kukatisha masomo kwa sababu ya kushindwa kumudu ada na fedha za kujikimu, tangu kuanza kwa hii mikopo angalau sasa kuna watu ndoto zao zinakwenda kutimia hii inatupa motisha sisi kama wasimamizi wa vyuo vya kati,” amesema Ndumbo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utawala na Fedha wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), Godwin Mkisi amesema mfuko kwa kushirikiana na HESLB wamewezesha wanafunzi kutoka kaya maskini kupata mikopo hiyo kwa asilimia 100.
Amesema tangu ushirikiano huo umeanza wanafunzi zaidi ya 11,000 kutoka kaya maskini wamefanikiwa kupata mikopo hiyo kwa kiwango cha asilimia 100.

“Tunafahamu kuna viwango vya mikopo vinatolewa kulingana na hali ya mnufaika, lakini Tasaf kwa kushirikiana na bodi ya mikopo tumehakikisha wale wanaotoka kwenye kaya maskini zaidi wanapata mikopo kwa asilimia 100,” amesema Mkisi.
Kuhusu kuanza kwa mwaka mpya wa masomo, Kiwia amesema dirisha la uombaji mikopo lilifunguliwa Juni 15, 2025 na linatarajiwa kufungwa Agosti 31, 2025 hivyo litadumu kwa miezi mitatu.
“Huu ni muda wa kutosha natumai, waombaji watazingatia kutuma maombi yao katika muda uliopangwa na sio kusubiri mwishoni. Tunasisitiza waombaji kusoma miongozo kabla ya kuomba, kufuata maelekezo na kuhakikisha wana nyaraka zote zinazohitajika.”
“Kwa waombaji wenye Namba ya Utambulisho (NIN), wanashauriwa kujaza wakati wa kuomba mkopo. Hata hivyo, kama mwombaji hana, anaweza kuendelea na maombi bila namba hiyo,” amesema.
Amesema katika maombi ya mikopo ya mwaka wa masomo 2025/2026, waombaji wa mikopo watatambuliwa kwa kutumia anwani zao za makazi (NaPA).
“Mwombaji mkopo atapaswa kuwasilisha kumbukumbu namba iliyopo kwenye barua ya utambulisho kwa kuijaza kwenye mfumo wa maombi ya mkopo ‘OLAMS’. Kila mwombaji atapaswa kuwa na akaunti ya benki na ahakikishe majina yanayosomeka kwenye akaunti yanafanana na yaliyopo kwenye cheti chake cha kidato cha nne (CSEE),” amesema Kisiwa.
Kuhusu wanufaika wa ruzuku za ‘Samia Scholarship’ amesema kwa mwaka wa masomo 2025/2026 ufadhili huo utatolewa kwa wanafunzi 700 watakaopata ufaulu wa juu katika tahsusi za sayansi kwenye mitihani ya kidato cha sita, inayoendeshwa na Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta).