Dar es Salaam. Aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa CUF (Bara), Maftaha Nachuma amesema mapambano ya kweli ya haki za wananchi yanayofanywa na ACT Wazalendo, ndio sababu iliyomfanya kuhamia chama hicho, huku akiomba viongozi kumpa ushirikiano.
Maftaha ambaye ni mbunge wa zamani wa Mtwara Mjini amesema alikuwa uwezo wa kwenda vyama vingine vya upinzani, lakini kwa mtazamo wake ameviona havina mapambano ya kweli yatakayowakomboa Watanzania.
Ameeleza hayo leo Alhamisi Juni 19,2025 mkoani Mtwara wakati akipokelewa na vigogo wa ACT Wazalendo wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho (Bara), Isihaka Mchinjita na Ado Shaibu ambaye ni Katibu Mkuu wa chama hicho.

“Nimechagua chama ambacho kinapambania haki za wananchi na si kingine bali ni ACT Wazalendo, Taifa la wote, masilahi ya wote’. Ndio maana nimekuja huku na sikuja peke yangu, niwaombe viongozi tuwe na mapambano ya kweli, tusifanye siasa za mzahamzaha,”amesema Maftaha.
“Ndugu zetu naomba mtupokee, mimi na pamoja na wenzangu tumekuja kwa wingi na wapo wengine watajiunga na ACT Wazalendo. Nimefuata ukombozi na mapambano ya kweli, lakini si vyama vingine vilivyobaki ambapo niliahidiwa vyeo,” amesema Maftaha.
Kwa mujibu wa Maftaha, amechagua jukwaa la ACT Wazalendo ili kuwa huru kwa ajili ya kuwatetea Watanzania na wananchi wa Mtwara, akisema hatua ya kujiunga na chama hicho, ndio mwanzo wa kuanza mapambano rasmi.

“Keshokutwa tutaanza rasmi mikutano ya hadhara, niwaambie nimekuja ACT Wazalendo wapo makini sana, tofauti na chama nilichotoka,” amesema Maftaha ambaye mwaka 2024 alijitosa kuwania uenyekiti wa CUF lakini hakufanikiwa mbele ya Profesa Ibrahim Lipumba.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara), Magdalena Sakaya amesema Maftaha kuondoka chama hicho lilikuwa suala la muda kwa sababu baada ya kukosa uenyekiti hakuwa akishiriki shughuli za ujenzi wa chama.
“Angemalizia kuwa baada ya kukosa uenyekiti nimeamua kuondoka CUF, kusema chama cha CUF hakina mapambano. Tunachojua Maftaha alikuwa anataka cheo ndani ya CUF, alipokikosa akaanza harakati za kutaka kuhama.
“Yeye aliamini atashinda, lakini ndani ya CUF kuna demokrasia, wajumbe waliamua kwa kura akapata nafasi ya tatu kati ya wagombea tisa waliokuwa wakiwania uenyekiti. Kukosa uongozi kwake kumekuwa nongwa awe anasema ukweli basi…,”amesema Sakaya.
Aweka heshima kuhamia ACT
Kwa upande wake, Ado amesema mwanasiasa makini lazima atafute heshima ambayo si cheo, mali au utajiri bali kupendwa kuheshimiwa na kukubalika na watu wako.

“Hapa Tanzania wako wanasiasa ambao wameonyesha kuwa wanayo heshima ya kupendwa na kukubalika na kusikilizwa na wananchi wao. Mmewahi kusikia wanasiasa wengi wanahama vyama, ila nataka kuwaambia ni wanasiasa wachache wanaoweza kuhama chama na umma wao ukafuata wanakokwenda,” amesema.
“Wapo wachache sana, mimi namkumbuka mmoja tu ambaye ni marehemu Maalim Seif Sharif Hamad ambapo alipoamua kujiunga CUF umma ulimfuata na nyinyi ni mashahidi. Nampongeza sana Maftaha, leo ni siku yake, tulitaka ajiunge nasi mapema akatukatalia akasema yupo na wenzake tusubiri azungumze nao,” amesema Ado.
Ado amesema Maftaha ameandika rekodi ambayo baadhi ya watu walishindwa kwa hatua yake ya kuhamia ACT Wazalendo pamoja na umma unaomuunga mkono.
“Maftaha ametuambia mapinduzi haya hayataishia Mtwara, bali yatakwendea nchi nzima bandika bandua. Hiki kinachofanyika leo ni mapinduzi ya kusini, tunakwenda kuikomboa kusini sasa,” amesema Ado.
Naye, makamu mwenyekiti wa chama hicho, Mchinjita amesema wananchi wa Mtwara hawana sababu ya kuendelea kusalia chama tawala badala yake wanapaswa kujiunga na ACT Wazalendo chenye ukombozi wa kweli.