Tabora. Wivu wa mapenzi unadaiwa kusababisha vifo vya mama na watoto wake wanne katika Wilaya ya Igunga, mkoani Tabora, baada ya mama huyo kuwanywesha watoto wake sumu ya kuulia wadudu kisha naye kunywa sumu hiyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao amemtaja mama aliyefariki kuwa ni Kang’wa Mahigi, mkazi wa Kata ya Lugubu, Wilaya ya Igunga.
Abwao ametoa taarifa kuhusu tukio hilo leo Juni 19, 2025, akieleza kuwa mama huyo alisubiri mumewe alipokwenda shambani, kisha akaenda kununua pakiti moja ya sumu ya kuulia wadudu, aliichanganya kwenye kikombe na kuwanywesha watoto wake na baadaye naye akanywa sumu hiyo.
Amesema chanzo cha tukio hilo kinadaiwa kuwa ni wivu wa mapenzi ambapo Mahigi (25) alikuwa ni mke mkubwa.
Inadaiwa kuwa mumewe alioa mke wa pili na kumjengea nyumba ya kisasa yenye huduma bora, jambo ambalo Mahigi hakuridhika nalo, kwani mara kwa mara alieleza kutoridhishwa na tofauti ya mazingira kati yao.
“Tukio hili la kikatili, kihalifu na lisilo na utu lililoangamiza maisha ya watu wasiostahili kuumizwa na pia hakuna mazingira yanayoruhusu kuumiza watu wengine kwa sababu ya hasira, wivu au kwa namna yoyote ile,” amesema Abwao.
Kwa mujibu Abwao amewataja watoto waliopoteza maisha katika tukio hilo ni Sengi James (8), Simon James (6), Elisha James (3), na Kashinje James (miezi saba), pamoja na mama yao, Kang’wa Mahigi (25), ambaye ndiye anadaiwa kutekeleza mauaji hayo.
Aidha, Kamanda Abwao amesema miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Igunga kwa ajili ya uchunguzi kabla ya kukabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya taratibu za mazishi.
Ameongeza kuwa jamii inapaswa kuepuka kujichukulia sheria mikononi, kwani hakuna changamoto isiyokuwa na suluhisho.
Hili ni tukio la pili kutokea ndani ya wiki moja mkoani Tabora. Tukio la kwanza lilitokea Juni 15, 2025, katika Kata ya Kalunde, Manispaa ya Tabora, ambapo mwanamke mwenye umri wa miaka 21 alijiua kwa kunywa sumu ya kuulia wadudu.