Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Mwakiposa Kihenzile, ametembelea banda la Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika viwanja vya Chinangali Park, jijini Dodoma.
Katika ziara hiyo, Mhe. Kihenzile alipokelewa na maafisa wa TAA waliompatia maelezo kuhusu majukumu ya msingi ya Mamlaka hiyo, ikiwemo kusimamia, kuendeleza na kuendesha jumla ya viwanja 61 vya ndege vya serikali kote nchini, vikiwemo viwanja viwili vya kimataifa vya Julius Nyerere (JNIA) na Kilimanjaro (KIA).
Naibu Waziri alielezwa kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika viwanja vya ndege vya mikoa mbalimbali, ikiwemo Msalato, Tabora, Shinyanga, Musoma, Kigoma, Sumbawanga, Moshi na Lake Manyara. Vilevile, alifahamishwa kuhusu miradi iliyokamilika katika viwanja vya Iringa, Mtwara, Dodoma, Mpanda na Kahama, inayolenga kuongeza ufanisi, usalama na viwango vya huduma vinavyotolewa katika sekta ya usafiri wa anga.
Akizungumza baada ya kutembelea banda hilo, Mhe. Kihenzile aliipongeza TAA kwa utekelezaji mzuri wa miradi na kwa juhudi zinazofanywa katika kuhakikisha viwanja vya ndege nchini vinakuwa na miundombinu ya kisasa inayokidhi mahitaji ya sasa. Alisisitiza kuwa sekta ya usafiri wa anga ni kichocheo muhimu cha uchumi wa taifa na kwamba Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi kama TAA katika kukuza maendeleo hayo.
Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kwa mwaka huu yanafanyika kwa kaulimbiu “Himiza Matumizi ya Mifumo ya Kidijitali Ili Kuongeza Upatikanaji wa Taarifa na Kuchangia Uwajibikaji,” yakilenga kuonesha jinsi taasisi za umma zinavyotumia teknolojia kuboresha huduma kwa wananchi. TAA ni miongoni mwa taasisi muhimu zilizo chini ya Wizara ya Uchukuzi zinazoshiriki kikamilifu katika maonesho haya kwa lengo la kuonesha mafanikio na mchango wake katika sekta ya uchukuzi wa anga.
Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Mwakiposa Kihenzile akipata maelezo kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi Kiwanja Cha Ndege cha Kimataifa Msalato Bw. Jeff Shantiwa alipotembelea banda la Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) wakati wa maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2025 yanayofanyika katika viwanja vya Chinangali Park, jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Mwakiposa Kihenzile akizungumza alipotembelea banda la Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) wakati wa maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2025 yanayofanyika katika viwanja vya Chinangali Park, jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Mwakiposa Kihenzile akisaini kitabu katika banda la Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) wakati wa maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2025 yanayofanyika katika viwanja vya Chinangali Park, jijini Dodoma.
Picha ya pamoja