Unguja. Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), imeshangazwa na baadhi ya taasisi za umma kuendelea kurudia makosa licha ya kuwepo kwa juhudi za kuyarekebisha.
Akizungumza wakati wa kuwasilisha taarifa ya PAC kuhusu ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2022/23 katika mkutano wa 19 wa Baraza la Wawakilishi leo Juni 19, 2025, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Juma Ali Khatib amesema hali hiyo inahatarisha misingi ya utawala bora na demokrasia, hasa pale makosa yale yale yanapoendelea kujirudia.
Kamati hiyo imetaja dosari 17 zinazojirudia, ikiwamo taasisi kutowasilisha hesabu zao kwa wakati, waajiriwa kutothibitishwa kazini, kutojumuishwa kwa matumizi yote katika taarifa za kifedha, malipo kwa watoa huduma wasiosajiliwa, matumizi nje ya bajeti na upungufu wa vielelezo vya matumizi.
Dosari nyingine ni kutowasilishwa kwa mapato serikalini, mikataba kutofikishwa kwa Mwanasheria Mkuu na kucheleweshwa kwa miradi ya maendeleo.
Khatib amesema dosari hizo ni kielelezo cha utekelezaji duni kutoka kwa baadhi ya watendaji wa Serikali na ukiukwaji wa utaratibu wa kisheria, hali aliyosema inatakiwa kushughulikiwa haraka.
Kamati hiyo pia imeitaka Serikali kuchukua hatua dhidi ya watendaji waliohusika na ubadhirifu wa mali na fedha za umma.
Mei 12, 2025, CAG, Dk Othman Abbas Ali alimkabidhi Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi ripoti 11 za ukaguzi, ambazo baadaye zilikabidhiwa kwa Spika Zubeir Maulid, lakini kwa tofauti na miaka iliyopita, safari hii ripoti hizo hazikuwasilishwa hadharani, jambo lililoibua maswali kwa baadhi ya wajumbe wa baraza.
Ripoti hizo zilijumuisha ukaguzi wa miradi ya maendeleo ya wadi, miradi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo (CDF), ukaguzi wa fedha za Serikali kuu, ukaguzi wa mifumo ya Tehama (Teknolojia ya Habari na Mawasiliano), mashirika ya umma, ununuzi wa magari ya Serikali, pensheni kwa wazee, viwanja vya michezo na miradi ya ujenzi wa madarasa, barabara na usambazaji wa maji Zanzibar.
PAC pia, imesisitiza umuhimu wa kuwepo kwa mpango madhubuti wa kuwajengea uwezo wajumbe wapya wa kamati hiyo baada ya uchaguzi, kwa sababu wengi hawatakuwa na uzoefu wa uchambuzi wa ripoti za CAG.
Hivyo, imependekeza kuwa muda ukifika, Baraza la Wawakilishi liandae mafunzo hayo kwa wataalamu wa kamati kusudi waweze kuwasaidia wajumbe wapya kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
“Mafunzo haya yajikite zaidi katika masuala ya fedha, ununuzi, kodi na usimamizi wa miradi ya maendeleo,” amesema Khatib.
Amesema Serikali pia inapaswa kuhakikisha ofisi ya CAG inapatiwa fedha zote ilizopangiwa kwenye bajeti ya mwaka 2025/26 kwa ajili ya kufanikisha jukumu hilo.
Akiwasilisha ripoti ya CAG, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora), Haroun Ali Suleiman amesema jumla ya hati 102 za ukaguzi zilitolewa, 95 kati ya hizo sawa na asilimia 93.14 zilikuwa na maoni yanayoridhisha, huku saba zikiwa na shaka. “Hakuna hati yoyote ya kushindwa kutoa maoni iliyotolewa mwaka huo,” amesema Suleiman.
Spika wa Baraza la Wawakilishi, Zubeir Maulid amesema kwa mujibu wa kanuni za baraza, ripoti hiyo haiwezi kujadiliwa mpaka mkutano mwingine, hata hivyo, aliwaruhusu wajumbe kuuliza maswali matatu ya ufafanuzi.
Mwakilishi wa Fuoni, Yussuf Hassan Idd amehoji hatua zilizochukuliwa katika utekelezaji wa mapendekezo ya CAG ya mwaka uliopita na kuhusu hoja zinazojirudia kila mwaka pamoja na ukiukwaji wa sheria.
Akijibu, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Saada Mkuya amesema mapendekezo ya CAG yanaendelea kutekelezwa, jambo linalothibitishwa na ongezeko la hati zinazoridhisha.
Kuhusu sheria za ununuzi, Waziri Mkuya amesema Serikali imetunga sheria mpya ambayo imeridhiwa na Benki ya Dunia na hatua hizo zinalenga kupunguza changamoto siku zijazo.