Dodoma. Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) imetoa wito kwa wanandoa na wenza wapya kupima afya zao kabla ya kuamua kuoana au kupata watoto, ili kuepuka hatari ya kuzaa watoto wenye changamoto za kiafya, ikiwemo ugonjwa wa selimundu.
Mbali na kuhimiza upimaji wa afya kabla ya kuoana au kupata watoto, BMH pia imetoa wito kwa Watanzania kutambua umuhimu wa kuwa na Bima ya Afya, ili kupunguza mzigo wa gharama kubwa za matibabu ya magonjwa sugu kama selimundu.
Wito huo umetolewa leo, Alhamisi Juni 19, 2025, na Mkurugenzi wa BMH, Profesa Abel Makubi, wakati akizungumza na wazazi pamoja na watoto waliopata matibabu na kufanyiwa upandikizaji wa uroto katika hospitali hiyo.
Profesa Makubi amesema kuwa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, hospitali hiyo imefanikiwa kuwafanyia upandikizaji wa uroto watoto 21, ambao wote wamepona.
Aidha, ameongeza kuwa matibabu yanaendelea kutolewa kwa wagonjwa wengine wanaohitaji huduma hiyo.

New Content Item (1)
Kuhusu umuhimu wa kupima afya, Profesa Makubi amesema kuwa kutofanya vipimo kabla ya ndoa au kuzaa kunachangia ongezeko la watoto wanaozaliwa wakiwa na ugonjwa wa selimundu.
Amesisitiza kuwa hali hiyo inaweza kuongeza mzigo mkubwa wa gharama kwa Serikali katika kuwahudumia wagonjwa hao.
Kuhusu gharama za matibabu, Profesa Makubi amesema kuwa hadi sasa, matibabu ya mgonjwa mmoja wa Selimundu yanakadiriwa kugharimu hadi Sh75 milioni, kiwango ambacho wengi hawawezi kumudu bila msaada wa bima ya afya au uingiliaji wa Serikali.
“Kama tunavyopima maambukizi ya VVU kwa wanandoa kabla ya kuoana, ndivyo inavyotupasa kuwapima watu hata kwenye ugonjwa huu,” amesema Profesa Makubi.
Amesisitiza umuhimu wa wananchi kuwa na mwamko wa kujiunga na Bima ya Afya, hasa wakati nchi inaelekea katika utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote.
Profesa Makubi ameeleza kuwa ingawa bima hiyo haitagharamia kila huduma ya matibabu kwa asilimia 100, bado inasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza gharama kubwa za matibabu.
Katika hatua nyingine Profesa Makubi amesema Tanzania imepewa heshima ya kujenga kituo kikubwa cha kupandikiza uroto kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na kituo hicho kitaanza kujengwa katika viwanja vya Hospital ya Benjamin Mkapa.
Kauli ya Profesa Makubi imekuja wakati ambapo tayari zipo takwimu zinazoonyesha ukubwa wa tatizo la ugonjwa wa selimundu nchini.
Mwishoni mwa mwaka jana, akijibu swali bungeni, Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel, alieleza kuwa takribani watu 200,000 nchini wanaishi na ugonjwa wa Selimundu (Sickle Cell).
Aidha, Dk Mollel alibainisha kuwa watoto wapatao 11,000 huzaliwa kila mwaka wakiwa na ugonjwa huo, ambao ni wa kurithi na unaosababishwa na vinasaba kutoka kwa wazazi.
Hali hiyo inasisitiza umuhimu wa kupima afya kabla ya kuoana, ili kusaidia kupunguza visa vya watoto kuzaliwa na changamoto hiyo ya kiafya.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara katika Shule ya Tiba ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Shakilu Jumanne, amesema kuwa safari ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa Selimundu bado ni ndefu na inahitaji juhudi za pamoja na kujitolea zaidi kutoka kwa wataalamu, jamii na wadau wa afya.
Dk Jumanne ameeleza sababu katika mapambano hayo ni ukosefu wa elimu kwa wananchi, lakini gharama kubwa za matibabu kwamba zinachangia kutokufikia malengo.
Mmoja wa wazazi wa watoto waliopandikizwa uroto Maryconsolatha Mkungano amesema wagonjwa wengi wanashindwa kuzifikia huduma hizo kwa kukosa fedha hata kama wanaujua ukweli kuhusu matatizo yao.
Mkungano amesema elimu kuhusu selimundu inapaswa kutolewa kwa uwazi kwani baadhi ya watu wanaamini kuwa ni ugonjwa wa kulogwa.