Rais Samia kuzindua daraja la JPM, Tanzania ikiandika historia

Mwanza. Historia imeandikwa! Hiyo ndio kauli inayoweza kutumika kujumuisha yote kuanzia wazo la mradi, utekelezaji, kukamilika hadi kuzinduliwa kwa daraja la JPM, maarufu kama Kigongo-Busisi.

Daraja hilo limezinduliwa leo na Rais Samia Suluhu Hassan baada ya kukamilika kwa gharama ya zaidi ya Sh700 bilioni.


Utekelezaji wa mradi huo umefanywa na mkandarasi, China Civil Engineering Construction Corporation na China Railway 15 Bureau Group Corporation na ulifikia asilimia 25 wakati Rais Samia anaingia madarakani Machi 19, 2021 baada ya kifo cha mtangulizi wake, John Pombe Magufuli.


Katika taarifa yake wakati wa ziara ya Rais Samia, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Mohamed Besta anasema licha ya changamoto zilizotokea mwanzoni ikiwemo kuongezeka kwa kina cha maji ya Ziwa Victoria, utofauti wa hali ya kijiolojia na mlipuko wa ugonjwa wa Uviko-19, mradi huo umekamilika mapema kutokana na mkandarasi kufanya kazi kwa Saa 24 kuanzia Machi, 2023 kufidia muda uliopotea.

Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Mwanza, Paschal Ambrose anasema daraja hilo refu kuliko yote ukanda wa Afrika Mashariki na Kati lina urefu wa kilomita 3, upana wa mita 28.45 na barabara unganishi zenye urefu wa kilomita 1.66.


Daraja hilo lina njia mbili za magari zenye upana wa mita 7 kila upande na njia za waenda kwa miguu kila upande yenye upana wa mita 2.5 na maegesho ya dharura yenye upana wa mita 2.5 kila upande.

Ikipita juu ya maji ya Ziwa Victoria kuunganisha eneo la Kigongo Wilaya ya Misungwi na Busisi Wilaya ya Sengerema, daraja la JPM lina nguzo 804, kitako cha nguzo za madaraja 65, nguzo kuu 67 zikiwemo nguzo kuu 3 na nguzo za mlalo 806.

Hili ndilo daraja lenye upenyo mkubwa zaidi ya madaraja yote nchini kwa kuwa na upenyo wa mita 120 kati ya nguzo zake kuu kuruhusu meli na vyombo vingine vya usafirishaji majini kupita bila shida yoyote.

Faida za kiuchumi, kijamii

Daraja la JPM lina faida kadhaa ikiwemo kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, Tanzania kwa ujumla na nchi jirani za ukanda wa Maziwa Makuu za Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).


Kijiografia, daraja la JPM liko katika ushoroba wa Ziwa Victoria unaoanzia kuanzia mpaka wa Sirari Wilaya ya Tarime nchini Tanzania na mpaka wa Isibani County ya Migori nchini Kenya hadi katika mipaka ya Mutukula Wilaya ya Misenyi mkoani Kagera inayopakana na nchi jirani ya Uganda.

Ushoroba huo pia unahusisha mipaka wa Rusumo na Kabanga Wilaya ya Ngara inayopakana na nchi jirani za Rwanda na Burundi.

‘’Daraja la JPM litachochea biashara na shughuli zingine za kiuchumi katika ushoroba wa Ziwa Victoria na hivyo kuongeza siyo tu pato la wananchi, bali pia mapato ya Serikali kupitia kodi na ushuru,’’ anasema Ambrose.

Kupungua kwa muda wa kuvuka eneo la Kigongo-Busisi kutoka wastani wa dakika 45 hadi saa nzima kwa kutumia vivuko vya MV Mwanza na MV Misungwi hadi kufikia dakika 5 kwa kutumia gari na dakika 15 kwa waenda kwa miguu ni faida nyingine kuu za daraja la JPM.

Kuokoa maisha ya wagonjwa

Kuokoa maisha ya wagonjwa kutoka mikoa ya Kagera, Kigoma na Geita wanaowahishwa kwenye huduma za rufaa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza ni faida nyingine ya kukamilika kwa mradi huu inayotajwa na Injinia Ambrose.


‘’Kuna wakati nilisubiri zaidi ya saa nzima kuvuka kutoka Busisi kwenda Kigongo kumuwahisha mtoto wangu mgonjwa Hospitali ya Bugando; hali ya mtoto ilibadilika tukiwa eneo la kivuko na nilipofika hospitali nilipelekwa moja kwa moja ICU. Daraja hili litatuokoa na adha hiyo,” anasema Halima Mohamed, mkazi wa mji wa Geita.

Ujuzi, maarifa na teknolojia mpya

Ujuzi, maarifa na teknolojia mpya nay a kisasa walioupata wahandisi na mafundi wazawa walioshiriki utekelezaji wa mradi huo ni faida nyingine kwa Taifa unaotokana na ujenzi wa daraja la JPM.


“Teknolojia za kisasa na usanifu zilizotumika katika mradi wa ujenzi wa daraja la JPM ni fursa kwa wahandisi, mafundi na waajiriwa wa ndani kujifunza kwa kupata ujuzi kutoka kwa wenzao wa nje. Ujuzi huo utasaidia utekelezaji wa miradi ya aina hii siku zijazo,” anasema Abdulkarim Majuto, Mhandisi Mshauri mradi huo.


Miongoni mwa walionufaika kwa kupata ujuzi, maarifa na teknolojia mpya wa ujenzi wa madaraja ni wahandisi kutoka Tanroads na wahandisi wahitimu 11 walioko chini ya mpango unaoratibiwa na Bodi ya Usajili Wahandisi nchini (ERB).


Ajira za kudumu na za muda kwa makandarasi 17 wa ndani, watoa huduma 20, zaidi ya wahandisi 1,200 na wafanyakazi wa kada tofauti wa Kitanzania wenye juzi ni faida nyingine wa mradi wa ujenzi wa daraja la JPM.

Related Posts