Soraga: Maonyesho ya Nyamanzi kusisimua mapato, kuongeza ajira

Unguja. Maonyesho ya utalii na uwekezaji yanayotarajiwa kuanza kesho Juni 20, 2025, yanakusudia kuleta msukumo mpya katika kuongeza idadi ya watalii, kuimarisha mapato ya Taifa na kukuza ajira kwa vijana wa Zanzibar kupitia sekta ya utalii na huduma zinazohusiana.

Maonyesho haya ya pili kufanyika kisiwani hapa pia yana lengo la kuwa jukwaa muhimu la kukuza utalii, kuvutia wawekezaji wapya, na kuimarisha ushirikiano kati ya wadau wa sekta ya hiyo kutoka ndani na nje ya nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari katika eneo la Nyamanzi yatakakofanyika maonyesho hayo leo Juni 19, 2025, Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mudrik Ramadhan Soraga amesema matarajio ya Serikali kupitia ni kuhakikisha sekta hiyo inaendelea kukua kwa kasi kubwa.

Amesema mbali na kuitangaza na kuonyesha vivutio vya utalii Zanzibar, lakini tukio hilo limelenga kuwaleta watu pamoja na kupeana fursa ikiwemo kubadilishana biashara na uzoefu.

“Vitaonyeshwa vivutio vya utalii Unguja na Pemba na  tunaitangaza Zanzibar kufikia viwango vya kimataifa,” amesema.

Waziri Soraga amesema Serikali inachukua jitihada mbalimbali za kutangaza visiwa vya Zanzibar na kutoa ujumbe wazi kuhusu malengo ya kisiwa hicho.

Amesema ili kufanikisha hilo kwa ufanisi, ni muhimu kuandaa matukio ya aina hiyo yanayowaunganisha wadau kutoka ndani na nje ya nchi.

“Tunataka haya maonyesho yawe ya kipekee barani Afrika. Kwa kupitia ushiriki wa taasisi za kimataifa, watoa huduma za utalii, wawekezaji na wadau mbalimbali, tunaamini Zanzibar itazidi kujitangaza duniani kama kivutio kikuu cha utalii na uwekezaji,” amesema Waziri Soraga

Amesema anaamini kuwa mwelekeo waliouona pamoja na mageuzi makubwa yanayoonekana katika kipindi kifupi, watakuwa na uwezo wa kufanikisha malengo yao.

Hivyo ametumia fursa hiyo kuwaomba wadau wa sekta za biashara na wananchi kwa ujumla kujitokeza kwa wingi ili kushuhudia kazi nzuri ya kutangaza utalii na kuonyesha vivutio vyake katika visiwa vya Unguja na Pemba. 

Mjasiriamali wa kuuza vinyago kisiwani hapa, Haji Ali Haji amesema wanategemea kupitia maonyesho hayo pamoja na kutangaza vivutio, lakini itakuwa fursa kwa wajasiriamali na wafanya biashara kuongeza vipato vyao.

“Hii ni fursa pande zote mbili, ni hamasa katika uwekezaji katika sekta ya utalii lakini ni kukuza pato la wananchi na Taifa kwa ujumla,” amesema.

Related Posts