:::::::
Ikiwa Juni 19, 2025 ni siku ya Kabila la Wahehe Kitaifa, Wakili Sosten Mbedule ambaye pia ni mdau wa maendeleo katika eneo la Kalenga, amewataka Wahehe na Watanzania kwa ujumla kutumia siku hiyo kumkumbuka Mtwa Mkwawa, shujaa wa kihistoria wa Wahehe, na kutafakari umuhimu wa kupata viongozi bora, hasa kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba.
“Leo kwetu Wahehe ni siku muhimu ya kumuenzi Mtwa Mkwawa, shujaa aliyeunganisha Wahehe, aliyetetea haki na kupigania utawala bora. Ni siku ya kutafakari urithi wetu na namna ya kuuenzi kupitia uongozi makini,” amesema Wakili Mbedule.
Amesema kuwa Mtwa Mkwawa alikuwa kiongozi mwenye maono, asiyevumilia uonevu, ambaye alijitoa kuilinda ardhi na watu wake, hivyo maadhimisho ya siku ya Wahehe Kitaifa yana umuhimu wa kipekee katika kutunza historia, heshima, na misingi ya kizalendo.
Wakili huyo ametoa wito maalum kwa wakazi wa Jimbo la Kalenga, akisema kwa kuwa ni jimbo la kihistoria lenye asili ya kichifu, linahitaji kiongozi shupavu mwenye kujali maslahi ya wananchi, na anayeweza kudumisha mila na desturi, ambazo ni sehemu muhimu ya urithi wa Wahehe.
“Jimbo la Kalenga ni la kihistoria na kiheshima, linahitaji kiongozi mwenye uzalendo na anayejua thamani ya urithi wa Mtwa Mkwawa. Tujiandae kwa kuchagua kiongozi anayewajibika na mwenye maono,” ameongeza Mbedule.
Aidha, ametoa rai kwa wananchi wa Kalenga na maeneo jirani kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi mkuu mwezi Oktoba 2025, kushiriki kwa amani na kuchagua viongozi bora watakaosimamia maendeleo na heshima ya jamii.