Morogoro. Wananchi wa Manispaa ya Morogoro wakiwemo madereva wa daladala na vyombo vingine vya moto wamelalamikia ubovu wa baadhi ya barabara katika manispaa hiyo unaosababisha uharibifu wa vipuri vya magari zikiwemo springi, sampo na kuchanika kwa magurudumu.
Akizungumza na Mwananchi leo Juni 19, 2025, mmoja wa madereva wa daladala zinazofanya safari zake Kihonda – Manyuki – Azimio – katikati ya mji, Mussa Namgoli amesema ubovu huo haukuanza mwaka huu, bali tangu mwaka jana baada ya kutokea mafuriko makubwa.
“Tulitegemea baada ya yale mafuriko ya mwaka jana barabara hizi zingetengenezwa hata kwa kuchongwa na kuwekwa kifusi cha changarawe, lakini hazikutengenezwa mpaka mwaka huu mvua zilipokuja kuongeza uharibifu, sisi madereva tunapata tabu kwa sababu tunatumia mafuta mengi kutokana na mwendo wa kunyata na kukwepa mashimo,” amesema Namgoli.
Amesema changamoto hiyo ya ubovu wa barabara, pia, imekuwa ikiwafanya washindwe kukamilisha fedha za wamiliki wa magari (vipande vya matajiri) kwa sababu badala ya kutembea safari (ruti) 10 kwa siku, wamejikuta wakitembea saba au nane.
Dereva bajaji anayefanya safari zake barabara ya Mazimbu kwenda Lukobe, Abdalah Rashid amesema wapo baadhi ya matajiri ambao ni wamiliki wa daladala hawafahamu changamoto hiyo na inapotokea hitilafu ya vyombo vyao iliyosababishwa na ubovu wa barabara, wamekuwa wakiwanyang’anya vyombo hivyo kwa madai kuwa wameshindwa kuvitunza.
“Baadhi ya matajiri wapo mikoa mingine au wengine kwa makusudi wanajifanya hawajui, hii changamoto ya barabara, dereva ukishapiga simu na kumweleza tajiri springi imekatika, cha kwanza anakwambia lete bajaji nyumbani na funguo waachie watoto, na kitakachofuata hapo kama dereva huna mkataba, ni kunyang’anywa funguo na kazi huna,” amesema Rashidi.
Baadhi ya abiria wanaotumia usafiri wa daladala, bajaji na bodaboda kwenda maeneo ya manispaa ya Morogoro nao wameeleza namna ubovu wa barabara unavyowaathiri hasa wanapokuwa na wagonjwa wanaohitaji kupeleka hospitali ya rufaa.
Flora Joachim, mkazi wa Manyuki amesema mara kadhaa hasa nyakati za usiku madereva wa daladala, bajaji na bodaboda wamekuwa wakipandisha bei ya nauli wakidai kuwa barabara ni mbovu huku madereva wengine wakikataa kupeleka vyombo vyao vya usafiri katika maeneo hayo wakihofia kuharibu vipuri.
Haruna Aziz, mkazi wa Azimio amesema tangu Machi 2025 ameegesha gari lake nyumbani kwa kuwa anahofia lisiharibike kutokana na ubovu wa barabara.
“Tangu Machi gari nime-park (egesha) nyumbani, napanda bodaboda kwenda kazini na kurudi nyumbani, naogopa nisije nikakata spring, naitumia katika safari muhimu, labda mtoto anaumwa au nakwenda kufuata mahitaji ya dukani kwangu,” amesema Aziz.
Pamoja na ubovu wa barabara za Kihonda lakini pia zipo barabara kwenye kata nyingine ambazo zipo katikati ya mji ikiwemo kata ya Kiwanja cha Ndege, Mafiga na Mazimbu.
Catherine Bombwe, mkazi wa Mawenzi, kata ya Kiwanja cha Ndege, amesema barabara zote zinazoingia katika soko la Mawenzi zimesahaulika na kwa muda mrefu hazijafanyiwa matengenezo.
“Hata wateja wenye magari wanapokuja kununua bidhaa mbalimbali katika soko hili wanapata tabu, inabidi waegeshe magari yao mbali kwa sababu barabara hazipitiki, barabara zimechimbika tunaoomba Tarura (Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura)) ikumbuke hizi barabara,” amesema Bombwe.
Akifafanua jambo hlo, Meneja wa Tarura Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Emanuel Ndyamukama amekiri kuwepo kwa ubovu wa barabara nyingi katika manispaa hiyo, hata hivyo amesema tayari makandarasi wamerudi kwenye baadhi ya maeneo ya kazi na wanaendelea na matengenezo.
“Ni kweli barabara nyingi za Manispaa ya Morogoro zimeharibika kutokana na mvua zilizonyesha mwaka huu, lakini tayari wale makandarasi ambao walisimama kufanya kazi kipindi cha mvua wamesharudi kazini baada ya mvua kukatika na matengenezo yanaendelea,” amesema Ndyamukama.
Ameongeza kuwa wiki ijayo wataanza kutangaza kazi kwa ajili ya kupata makandarasi wengine wenye sifa watakaofanya matengenezo kwenye barabara nyingine kwa kutumia bajeti ya 2025/26.