Familia ya aliyekuwa Rais wa Zambia, hayati Edgar Lungu, imetangaza mazishi yake yatafanyika nchini Afrika Kusini ambako alifariki dunia Juni 5, 2025.
Hayo yameelezwa kukiwa na mvutano kati ya Serikali ya Zambia na familia ya Lungu kuhusu kurejeshwa mwili wake nyumbani.
Kutokana na mvutano huo, Rais wa sasa wa Zambia, Hakainde Hichilema Jumatano Juni 19 alitangaza kumalizika kwa kipindi cha maombolezo ya kitaifa.
Pia, alimuomba radhi Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, Serikali na wananchi wa Taifa hilo kwa mvutano uliotokea.
Makebi Zulu, msemaji wa familia ya Lungu katika taarifa iliyotolewa leo Ijumaa Juni 20, jijini Johannesburg, Afrika Kusini amesema wiki zilizopita zimekuwa za majonzi na changamoto kubwa kwa familia hiyo.
“Tunashukuru kwa pole nyingi na ujumbe wa faraja kutoka kila kona ya Bara hili na duniani kote,” amesema katika taarifa iliyochapishwa na mtandao wa Zambia Monitor.
Ametoa shukrani za familia kwa Serikali ya Afrika Kusini kwa kuheshimu uamuzi wa familia kufanya mazishi na ibada ya faragha nchini humo.
Zulu amepongeza msimamo wa Afrika Kusini kutokuingilia uamuzi wa familia na kuheshimu Katiba ya nchi hiyo.
“Tutatengewa nafasi ya kuomboleza na kusherehekea maisha ya mpendwa wetu Edgar Lungu kwa heshima na amani,” amesema.
Pia ameeleza faraja waliyopata kutokana na ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa wa Afrika Kusini, Ronald Lamola, aliyepeleka salamu za pole kutoka kwa Rais Ramaphosa.
Zulu amesema familia ya Lungu inaendelea kusisitiza umuhimu wa amani na umoja miongoni mwa Wazambia wakati huu, huku akitoa shukurani kwa marafiki, wafuasi na umma kwa uelewa wao.
“Maelezo zaidi kuhusu ratiba ya mazishi na shughuli nyingine yatawasilishwa kwa umma wa Zambia na Afrika Kusini kwa wakati muafaka,” amesema.
Jumatano Juni 18, Zulu alieleza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Pretoria kuwa, ingawa mwanzoni walifikia makubaliano na mamlaka husika, hatua za Serikali baadaye zilionekana kuvuruga makubaliano hayo.
Miongoni mwa mambo yaliyoibua wasiwasi ni tangazo la Mamlaka ya Maendeleo ya Barabara (RDA) la Juni 16 kuhusu ukarabati wa barabara zitakazotumiwa na msafara wa mazishi, bila kushauriana na familia.
Vilevile, taarifa ya Juni 17 kutoka kwa Katibu wa Baraza la Mawaziri iliwazuia wananchi kushiriki mapokezi ya mwili huo, jambo ambalo familia ilidai halikukubaliwa nao.
Zulu alieleza programu isiyoidhinishwa ilitolewa, ikibadilisha ratiba kwa kuelekeza mwili kutoka uwanja wa ndege moja kwa moja hadi kwenye ibada kanisani na baadaye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mulungushi, bila kupitia nyumbani kwa familia.
“Licha ya kulalamikia masuala hayo, Serikali iliendelea kutoa ratiba zinazokinzana. Kwa masikitiko, tumeamua kuwa mwili wa Rais Lungu hautarejeshwa nyumbani leo,” alisema Zulu.
Katika mkutano huo, Bertha Lungu dada wa Lungu, alisema inasikitisha kuona Serikali ikiendelea kutoa taarifa zinazokinzana licha ya makubaliano yaliyofikiwa na familia.
Familia ilieleza matumaini kuwa siku moja Rais huyo wa zamani atazikwa kwa heshima inayostahili urithi wake na matakwa ya familia.
Wakati huohuo, Jeshi la Ulinzi la Afrika Kusini lilionekana likiondoa zulia jekundu na kuondoka uwanjani baada ya familia ya Lungu kukataa kuusafirisha mwili siku hiyo, wakieleza tofauti zao na Serikali.