Arusha. Mahakama ya Rufaa imemuachia huru Stephen Mduma, aliyekuwa amekuhukumiwa kifungo cha miaka saba jela baada ya kukutwa na hatia ya kumuua bila kukusudia aliyekuwa mke wake, Jackline Mwanjombe.
Hukumu iliyomuachia huru Stephen imetolewa Juni 17, 2025 na jopo la majaji watatu wa mahakama hiyo walioketi Dar es Salaam ambao ni Barke Sehel, Khamis Ramadhan Shaaban na Dk Uben Agatho na nakala yake kuwekwa kwenye mtandao.
Jaji Sehel amesema baada ya kupitia hoja za pande zote na mwenendo wa rufaa hiyo wamebaini kuwa ushahidi uliomtia hatiani Stephen ulikuwa dhaifu.
Amesema wamejiridhisha kuwa upande wa mashtaka ulishindwa kumuunganisha moja kwa moja mrufani na kifo cha marehemu.
Rufaa hiyo ya jinai namba 842/2023 inapinga uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam uliotolewa Juni 30, 2023 katika kesi ya jinai namba 17/2022.
Stephen na Jackline (marehemu kwa sasa), walikuwa wakiishi kama mume na mke katika eneo la Kimara Baruti, Wilaya ya Ubungo ndani ya Jiji la Dar es Salaam.
Ilielezwa kuwa mara ya mwisho walionekana pamoja Oktoba 4, 2016 katika baa ya Plateau iliyopo Kimara Bucha inayomilikiwa na Julius Lema (shahidi wa sita), walipoenda kwa ajili ya kunywa pombe.
Upande wa mashtaka ulieleza kuwa ulipofika muda wa kuondoka Jackline (marehemu), alikuwa amelewa sana hawezi kusimama wala kutembea.
Shahidi huyo wa sita pamoja na kijana mwingine walimsaidia Stephen kumbeba mkewe hadi nyumbani kwao na kumwacha hapo mikononi mwake.
Shahidi wa pili na mkewe (shahidi wa tatu) ambao ni Andrew Peter na Lydia Joseph, wakiwa kwenye ufukwe wa Ununio Dynasty, Andrew alipokea simu ya Stephen akimjulisha mkewe hayuko sawa na amempeleka Hospitali ya Sinza Palestina.
Baada ya kupata taarifa hizo Andrew na Lydia, walienda hospitali ila walipofika hawakuweza kumuona Jackline kwani waliambiwa wasubiri nje wakati daktari akimhudumia na baada ya muda mfupi walijulishwa amefariki.
Ilielezwa mahakamani hapo kuwa taarifa za kifo cha marehemu ziliifikia familia ya marehemu akiwemo shahidi wa kwanza Erasto Mwanjombe na shahidi wa tano, Grayson Mwanjombe.
Kutokana na Erasto kuwa na mashaka na chanzo cha kifo hicho, aliripoti Kituo cha Polisi Gogoni kwa uchunguzi.
Oktoba 5, 2016, shahidi wa saba, F. 7180 Koplo Mbise, alipewa jukumu la kuchunguza tukio hilo,ambaye alitembelea eneo la tukio na kukuta kitambaa, simu ya mkononi na Malapa ya marehemu.
Alisema mwili wa marehemu ulihamishwa kutoka Hospitali ya Mwananyamala na kupelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa uchunguzi.
Shahidi wa nne, ambaye ni daktari bingwa wa hospitali hiyo, Dk Praxeda Atieno aliufanyia mwili huo uchunguzi mbele ya shahidi wa tatu, tano na saba.
Katika uchunguzi wa nje, aliona meno kwenye ulimi, kucha na midomo kuwa nyeusi, kinyesi na michubuko kwenye pande za shingo yake na katika uchunguzi zaidi, aliona michubuko kwenye sehemu ya mbele ya shingo.
Shahidi huyo alihitimisha chanzo cha kifo hicho ni ukosefu wa oksijeni kwa kukosa hewa kutokana na kubanwa kwa shingo na kitu kizito.
Katika utetezi wake, Stephen alikana kuhusika na mauaji hayo na kueleza kuwa walikuwa kwenye baa hiyo na kukiri kuwa alisaidiwa na shahidi wa sita kumbeba mkewe hadi nyumbani.
Alieleza kuwa akiwa nyumbani kwake alisaidiwa na mama yake mzazi Edina Mduma na shemeji yake Elizabeth Tumaini (waliokuwa mashahidi wake) ambao walimsaidia kumuogesha mkewe kwani alikuwa amejikojolea.
Edina aliieleza mahakama kuwa siku ya tukio alikuwa dukani kwake na alimuona Jackline akipekekwa nyumbani kwake kwa usaidizi wa watu akiwemo mumewe na alikuwa amelewa sana na amejikojolea.
Alieleza kwa msaada wa Elizabeth walimbadilisha nguo zake na kumweka eneo la wazi ili apate hewa safi lakini hali ilizidi kuwa mbaya hivyo wakampeleka hospitali.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, mahakama hiyo ya chini ilieleza upande wa mashtaka umethibitisha kesi hiyo pasipo kuacha shaka kuwa mrufani ndiye alikuwa mtu wa mwisho kuoneakana akiwa na Jackline akiwa hai.
Ilieleza kuwa Stephen alishindwa kutoa maelezo yanayokubalika kuhusiana na michubuko kwenye shingo ya marehemu na kuvunjika kwa mfupa na alitiwa hatiani kwa kosa la kuua bila kukusudia na kuhukumiwa kifungo cha miaka saba jela.
Katika rufaa iliyomuachia huru, Stephen alijitetea mwenyewe bila uwakilishi wa wakili huku upande wa Jamhuri ukiwakilishwa na mawakili watatu.
Miongoni mwa sababu za rufaa ni pamoja na mahakama kueleza yeye ndiye alikuwa mtu wa mwisho kuoneana na Jackline akiwa hai, upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha kosa la mauaji bila kukusudia.
Alieleza kuwa kabisa ushahidi uliowasilishwa dhidi yake hakukuwa na ushahidi wa moja kwa moja unaomhusisha na kifo cha marehemu kwa kuwa upande wa mashtaka ulishindwa kutoa ushahidi wa kuthibitisha mlolongo wa matukio yasiyopingika yanayoonyesha hatia yake.
Alihitimisha kuwa ushahidi uliotolewa haukumhusisha na kifo cha marehemu, hivyo shtaka la kuua bila kukusudia halikuthibitishwa kwa kiwango kinachotakiwa.
Mawakili wa Jamhuri walipinga rufaa hiyo na kukubaliana na uamuzi wa mahakama ya awali.
Jaji Sehel amesema kutokana na mawasilisho ya pande zote, suala la uamuzi wao ni iwapo hukumu ya kuua bila kukusudia inaungwa mkono na ushahidi wa kimazingira wa mtu wa mwisho kuonekana akiwa na marehemu akiwa hai kama inavyoshikiliwa na mahakama ya mwanzo.
Amesema kanuni ya mtu wa mwisho kuonekana na mtu aliyekufa akiwa hai ni moja ya aina za ushahidi wa kimazingira na kuwa kama ilivyojadiliwa kwa usahihi na mrufani, upande wa mashitaka unabeba mzigo wa kuthibitisha ukweli.
Jaji Sehel amesema katika rufaa ya sasa Stephen alipatikana na hatia kutokana na ushahidi wa shahidi wa sita kuwa alikuwa mtu wa mwisho kuonekana akiwa na marehemu akiwa hai.
“Kwa upande wetu, tumechunguza kwa makini ushahidi wa shahidi wa sita na kuona kwamba hakuwa mtu pekee aliyesaidia mrufani kubeba marehemu siku ya tukio,” amesema
Jaji huyo amesema hawaoni uamuzi wa mahakama ya chini kuwa wenye ushawishi,Stephen alikana kuachwa peke yake na marehemu nyumbani kwa vile kulikuwa na watu wengine waliomsaidia na kuwa ushahidi wa shahidi wa sita uliacha mambo mengi.
Ameongeza kuwa upande wa mashtaka una wajibu wa kuwaita mashahidi ambao kutokana na uhusiano wao na shughuli inayohusika, wanaweza kutoa ushahidi juu ya ukweli ikiwemo mashahidi kutoka hospitali ya Sinza Palestina.
“Tunakubaliana juu ya msimamo huo wa sheria, kama ilivyoainishwa chini ya kifungu cha 143 cha Sheria ya Ushahidi, tuna maoni madhubuti kwamba, kila kesi lazima iamuliwe kulingana na ukweli na mazingira yake ya kipekee.
Kuhusu idadi ya watu waliokuwepo nyumbani kwa mrufani Jaji huyo amesema wanaona kijana aliyesaidiana na shahidi wa sita na Stephen kumbeba Jackline (marehemu),kurudi nyumbani alikuwa ni shahidi muhimu.
Jaji Sehel amesema kutokana na mikanganyiko ambayo inaenda kwenye mzizi wa kesi ya mashtaka na kudhoofisha uaminifu wa ushahidi wa mashtaka.
“Tunafahamu kuwa kifo cha marehemu hakikuwa na mzozo lakini suala la msingi katika rufaa iliyopo ni iwapo mrufani ndiye aliyesababisha kifo chake.Kutokana na kukosekana kwa ushahidi wa wazi wa chanzo cha kifo hicho, tumejiridhisha kuwa upande wa mashtaka ulishindwa kumuunganisha moja kwa moja mrufani na kifo cha marehemu,”
Jaji alihitimisha kuwa katika uchambuzi wa mwisho, wanakubaliana na Stephen kuwa ushahidi uliotegemewa na mahakama ya mwanzo kumtia hatiani ni dhaifu na kutupilia mbali hukumu dhidi ya Stephen na kuamuru aachiwe huru.