Dar, Njombe zaongoza kwa upasuaji wa kujifungua

Arusha. Wajawazito wanaoishi katika mikoa ya Njombe, Dar es Salaam na Iringa wametajwa kuvuka kiwango cha idadi ya kujifungua kwa njia ya upasuaji, hali inayoashiria baadhi yao wanafanyiwa bila sababu za msingi za kitabibu.

Mkoa wa Njombe umetajwa kuongoza kwa kuwa na asilimia 32 ya wanawake wanaojifungua kwa upasuaji, Dar es Salaam asilimia 26 na Mkoa wa Iringa ni asilimia 24.

Hali hiyo imetajwa kuwa ni kinyume na mwongozo wa Shirika la Afya Duniani (WHO) linalopendekeza wastani wa wanaojifungua kwa upasuaji uwe chini ya asilimia 12 mpaka 15 kwa eneo husika.

Hayo yameelezwa leo Alhamisi, Juni 19, 2025 jijini Arusha na Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Wizara ya Afya, Dk Hamad Nyembea wakati akitoa mada kuhusu hali ya utoaji huduma za afya nchini, kwenye kongamano la kitaifa la tiba linalokwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 60 ya Chama cha Madaktari Tanzania (MAT).

Amesema hali hiyo inaashiria wajawazito wengi wanafanya uamuzi wa kufanyiwa upasuaji bila ulazima wowote na kwamba hiyo ni miongoni mwa changamoto za kitaalamu zilizopo katika huduma za uzazi, na huenda inatokea wananchi wakiwa hawana uelewa.

“WHO inapendekeza wastani wa wanaojifungua kwa upasuaji uwe chini ya asilimia 12 mpaka 15, lakini kuna baadhi ya mikoa imefanya upasuaji wa kina mama zaidi ya kiwango hicho, hii inaashiria huduma za upasuaji zinafanyika pasipo na sababu za msingi,” amesema.

Dk Nyembea amesema kujifungua kwa njia ya kawaida ni nzuri, kwani hakuna madhara kwa mama, na anabaki kuwa na afya njema pamoja na mtoto anayezaliwa.

“Wanawake wengi wanaojifungua kwa upasuaji, ambao pengine sababu ikawa wateja wenyewe wanashawishi upasuaji kumtoa mtoto, ambayo si njia sahihi. Kuna hatari zaidi kutokana na dawa wanazopatiwa, ikiwemo ile hatua yenyewe.

“Lakini sababu nyingine ni wataalamu, pengine wanaona warahisishe wapate huduma ya upasuaji. Mfano Iringa asilimia 24, Dar es Salaam asilimia 26 na Njombe wana asilimia 32 wamevuka kabisa kiwango,” amesema.

Dk Nyembea ametoa wito kwa wataalamu wa afya wafanye upasuaji pale tu wanapoona viashiria vya kufanya hivyo na kuwataka kufuata miongozo inavyotaka.

Amesema ni muhimu pia jamii ijue kuwa kujifungua kwa upasuaji ni hatari zaidi ikilinganishwa na kujifungua kwa njia ya kawaida.

“Muhimu wajawazito wapimwe mapema, waanze kliniki na wajue mapema watajifungua kwa njia gani. Hii itaboresha afya za watoto na kinamama kwa ujumla,” amesema.

Pamoja na hilo, Dk Nyembea amesema pia kuna mikoa inayoonekana kuna baadhi ya wajawazito walipaswa kujifungua kwa upasuaji, lakini wamelazimishwa kujifungua kwa njia ya kawaida, hali aliyoitaja inachangia matatizo mbalimbali kwa mama na mtoto.

“Maeneo yaliyoonyesha upasuaji haufanyiki kama kiwango kinachotakiwa na inaonyesha kuna kina mama waliopaswa kujifungua kwa upasuaji, lakini hawakupata hiyo huduma ni pamoja na mikoa ya Simiyu, Tabora na Katavi.

“Hii mikoa tunashauri wataalamu wawapime vizuri kina mama wabaini kama wanapaswa kufanyiwa upasuaji ili wajifungue salama na wapate watoto wao bila changamoto yoyote. Wito kwa jamii wawafikishe kina mama katika vituo kwa muda unaotakiwa,” amesema Dk Nyembea.

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, mgonjwa ana haki ya kuchagua njia ipi itumike wakati wa kujifungua, lakini wakati mwingine hali aliyonayo hufanya wataalamu kuamua ili awe salama yeye pamoja na mtoto.

Daktari bingwa wa kina mama, Cyrill Masawe amesema hakuna tabia zinazoweza kufanywa na mjamzito zinazomuweka katika hatari ya kujifungua kwa upasuaji, na badala yake ni mabadiliko yanayokuwepo katika ujauzito.

Amesema mama akipata uchungu kuna vigezo huangaliwa, ikiwamo uchungu kuendelea kama unavyotakiwa na mtoto kushuka.

“Kama kuna tatizo kuhusu mama au mtoto hushauriwa kufanyiwa upasuaji. Kama njia ni ndogo, mtoto hawezi kutoka, anatakiwa kujifungua kwa upasuaji kwa wakati ili wote wasipate tatizo,” amesema Dk Masawe.

Amesema wakati mwingine upasuaji hutumika kama njia ya dharura ikiwa mjamzito shinikizo la damu litapanda kiasi cha kumpa kifafa cha mimba, kutoka damu nyingi.

Naye daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi wa Hospitali ya Salaamani iliyopo Temeke, jijini Dar es Salaam, Dk Abdul Mkeyenge amesema changamoto nyingine husababishwa na nyonga ndogo ambayo ni maumbile ya mtu tangu alivyoumbwa.

Amesema, si kwamba watu wanapenda kujifungua kwa upasuaji, ila kuna sababu maalumu ambazo mjamzito anaweza kuwa nazo, hivyo kutakiwa kufanyiwa upasuaji.

Amezitaja baadhi ya sababu hizo kuwa ni, kupata uchungu lakini mtoto hatoki, aliyebeba ujauzito wa watoto pacha ambao wamekaa vibaya, shinikizo la damu la hali ya juu, presha ya kupanda ambayo inasababisha kupata kifafa cha mimba pamoja na ujauzito kufikia kipindi cha kujifungua, lakini mtoto amegeuza makalio.

“Ndiyo maana kuna masaa maalumu ya uchungu, kwa hiyo yakipitiliza inaweza ikachangia yule mtoto akapata matatizo, kwa hiyo tunalinda afya ya mama na mtoto, ndiyo maana inatakiwa afanyiwe upasuaji.

“Mwanamke aliyejifungua kwa upasuaji anaweza kupewa saa kadhaa za kusukuma, lakini ikishindikana itabidi afanyiwe tena upasuaji ili asipate madhara. Kwa hiyo si kwamba madaktari wanapenda kuwafanyia watu upasuaji ila inatokana na viashiria vitakavyojitokeza,” amesema Dk Mkeyenge.

Amefafanua kuwa, si watu wengi siku hizi wanafanyiwa upasuaji ila zamani ilikuwa kati ya wajawazito 10,000, wajawazito 450 walifariki kutokana na changamoto za uzazi kwa mwaka.

“Kwa sasa ukija kuangalia hizi takwimu zinapungua, vifo vya uzazi vimepungua na hii ni kutokana na Serikali kujitahidi kuanzisha vituo vingi vya afya, na vitendea kazi vya kutosha,” amesema Dk Mkeyenge.

Hata hivyo, ametoa wito kwa Serikali kuendelea kuongeza vituo vya afya, na endapo mwanamke akijigundua ni mjamzito anatakiwa aanze kliniki katika wiki 12 za kwanza.

Ripoti ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria (TDHS) wa mwaka 2022 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) hivi karibuni inaeleza kuwa, kiwango cha wanawake wanaojifungua kwa upasuaji kiliongezeka kutoka asilimia 7 katika utafiti wa mwaka 2015/2016 hadi asilimia 11 katika utafiti wa mwaka 2022.

Ufafanuzi unaonyesha kuwa ni asilimia nne pekee ya wanawake wasiokuwa na elimu na waishio katika kipato cha chini ndiyo wanatumia njia ya upasuaji katika kujifungua, ikilinganishwa na asilimia 20 ya wanawake wenye elimu na asilimia 24 ya wanawake wenye kipato fulani.

Ripoti hiyo pia inaeleza kuwa, kiwango cha wanawake kujifungua kwa njia ya upasuaji ni kikubwa zaidi katika hospitali za binafsi kwa asilimia 30, ikifuatiwa na hospitali za dini kwa asilimia 28, huku vituo vya kutolea huduma vya umma vikiwa na asilimia 12.

Katika mikoa, Njombe inaongoza kwa kuwa na asilimia 33, ikifuatia Kilimanjaro kwa asilimia 30, na Dar es Salaam ikiwa na asilimia 26.

Mkoa wa Simiyu ambao unaongoza kwa wanawake wake kuwa na uwezo wa kupata watoto wengi nchini, lakini ni asilimia 2 pekee ndiyo wanajifungua kwa upasuaji.

Related Posts