IMANI POTOFU MATUMIZI YA BANGI KWA WAVUVI ZIWA VIKTORIA

…….

Na Daniel Limbe,Chato

BANGI ni mmea maarufu sana hapa Duniani ambao umekuwa ukitumiwa kwa miongo kadhaa na baadhi ya watu licha ya nchi nyingi kupiga marufuku matumizi yake kutokana na madhara kiafya.

Licha ya marufuku hiyo, baadhi ya wataalamu wa tiba asili wamekuwa wakieleza kuwa maji maji ya mmea huo husaidia kutibu sikio linalouma na kutoa usaha.

Tanzania kama zilivyo nchi zingine matumizi ya bangi hayaruhusiwi kwa namna yoyote ile, japo baadhi ya watu hufanya shughuli za kilimo hicho kwa usiri mkubwa na wengine kuvutaji kilevi hicho kwa kujificha.

Uchunguzi wetu umebaini kuwa bado kasi ya utumiaji wa kilevi hicho ni mkubwa kwa baadhi ya maeneo ya wavuvi wa samaki ndani ya ziwa viktoria kutokana na imani potofu za kufukuza majini (mapepo) yanayohusishwa na suala la upatikanaji wa samaki.

WANAVYO AMINI

Makala hii imefanikiwa kuzungumza na Makoye Vicent, mkazi wa wilaya ya Chato ambaye ni mvuvi wa samaki kwenye mwalo wa Kitela, anasema matumizi ya bangi husaidia kupatikana kwa samaki wengi wakati wa kuwavua kutoka ndani ya ziwa.

Anasema baadhi yao hutumia kwa kuvuta kabla ya kwenda kutandaza nyavu zao ndani ya maji na kwamba wanapoanza shughuli ya uvuvi mapepo yote hukimbia kutoka zilipo samaki kutokana na kusikia harufu ya mmea huo.

“Baadhi yetu tunatumia kwaajili ya kujipatia samaki, maana ndani ya ziwa kuna miujiza mingi sana ya mapepo wachafu na usipo kuwa makini unaweza kwenda kuvua samaki na ukazama na kupoteza maisha,kwa hiyo lazima uingie kwa tahadhali kubwa,”

Vicent anasema baadhi ya wavuvi hufunga kwenye nyavu zao vitambaa vilivyo zungushwa na bangi ndani yake kabla ya kuingiza nyavu ziwani, jambo linalosaidia kupatikana kwa samaki wengi.

Marko Andrea,mvuvi mwalo wa Chato Beach anasema utumiaji wa bangi unafaida kubwa kwa wavuvi walio wengi kutokana na manufaa wanayopata ki uchumi.

“Siwezi kusema kuwa bangi ni mbaya wakati inanisaidia kupata pesa, kazi za uvuvi ni ngumu na zina mazingaombwe mengi, unaweza kutega eneo moja na mwenzako ukashangaa yeye anapata samaki wa kutosha wakati wewe umechoma mafuta bure,” anasema

“Ukitaka kuamini ninayokueleza twende pamoja kuvua samaki tukiwa na mtumbwi mmoja wa wenye bangi na mwengine unaotegemea kudra za Mungu ili uone ni nani atatoka na samaki.” amesisitiza Andrea.

Helena Masanja,mchuuzi wa samaki mjini Chato, anathibitisha wavuvi wengi kujihusisha na matumizi ya dawa za kulevya kwa kuamini kuwa zinawasaidia kupata samaki wa kutosha.

Anasema kundi la vijana wanaovua samaki ndilo linaongoza kwa uvutaji wa bangi licha ya baadhi yao kupata shida za kiafya ikiwemo kuchanganyikiwa akili.

“Bahati njema mie huwa nakwenda kuchukua samaki mwaloni kila siku, baadhi ya vijana wanavuta bangi hata alfajili wanapotoka kuvua na wengine wanavuta hadharani kabisa muda wa jioni kabla hawajaingia kwenye uvuvi”anasema Masanja.

Mwenyekiti wa kikundi cha usimamizi wa raslimali za uvuvi ndani ya ziwa Viktoria (BMU) mwalo wa Chato Beach, Kamese Malima, anasema licha ya kwamba yeye hajawahi kutumia bangi katika shughuli za uvuvi lakini anakiri wapo baadhi ya wavuvi wanao amini katika matumizi ya bangi.

Anasema suala hilo linatokana na baadhi ya wavuvi kuwa na imani kuwa bangi hufukuza majini ndani ya ziwa na kwamba hali hiyo huwasaidia kupata samaki wengi jambo analodai linahitaji utafiti wa kisayansi kulithibitisha.

“Ni kweli wapo baadhi ya wavuvi hasa vijana hujihusisha sana na matumizi ya bangi, siwezi kuwa na jibu la moja kwa moja iwapo inawasaidia kupata samaki au hapana maana mie sijawahi kutumia licha ya kuwa nami ni mvuvi,”anasema

“Ninachoweza kuamini ni kwamba shughuli za uvuvi wa samaki muda frani huchagizwa na bahati ya kila mtu,maana unaweza kuvua sehemu moja ukapata samaki wa kutosha lakini mwenzako aliye eneo hilo hilo anaweza asipate kitu” anasema Kamese.

Ofisa uvuvi mwandamizi kutoka Idara ya uvuvi halmashauri ya wilaya ya Chato, Deograthias Ngeleshi, anashangazwa na baadhi ya wavuvi kuamini mafanikio katika bangi na kwamba suala la mafanikio katika uvuvi wa samaki halihusiani kabisa na matumizi ya bangi.

Anasema hakuna utafiti wa kisayansi unaothibitisha kuwa bangi husaidia kupatikana samaki wengi na kwamba hatua hiyo inatokana na imani potofu iliyojengeka kwa baadhi ya wavuvi ndani ya ziwa Viktoria.

“Pamoja na kwamba Mimi ni mtaalamu wa masuala ya uvuvi wa samaki, hakuna maandiko yoyote niliyofundishwa shule kuwa bangi husaidia kupatikana samaki wengi, huu ni mchezo machafu unaofanywa na baadhi ya wavuvi kukiwekea uhalali wa kutumia kilevi hicho kinyume cha sheria,”anasema

“Sisi kama wataalamu wa masuala ya uvuvi siku zote tunawasisitiza na kuwaelimisha wadau wetu kuwa mafanikio katika uvuvi yanatokana na bidii na maarifa ikiwa ni pamoja na kuwekeza katika zana za kisasa zinazokubalika kisheria, na kwamba suala la mafanikio halina njia ya mkato zaidi ya uwekezaji wa kisasa” anasema Deograthias.

MSAIKOLOJIA TIBA

Msaikolojia tiba, Said Kisenge, anasema baadhi ya matumizi ya dawa za kulevya huchochewa na kundi rika hasa mtu anapokutana na jamii ambayo inaamini jambo furani kuwa ni sahihi naye hulazimika kuingia katika mkumbo huo ili kufanana na jamii husika.

Anasema hakuna ukweli wowote wa upatikanaji wa samaki kwa kufukuza mapepo ziwani ili mtu apate samaki wengi, ispokuwa mtu anapotumia kilevi kama pombe au bangi humjengea ujasiri wa kufanya jambo ambalo kwa hali ya kawaida asingeweza kulitenda.

“Mara nyingi watu kuvuta bangi ili kufanikiwa katika shughuli za uvuvi ni suala la kisaikolojia, maana mtu akivuta bangi inamuondoa katika akili ya kawaida na anaweza kufika eneo ambalo watu wengine ambao hawajavuta bangi hawawezi kufika,”

“Kwa kuwa anakuwa kaondoa uoga anaweza kupeleka nyavu zake kwenye kina kirefu zaidi ambacho watu wengine wanaogopa na kwa kuwa hakufikiwi na wengine anaweza kupata samaki kwa kuwa eneo hilo yuko pekee yake na siyo kweli kwamba bangi inakuwa imefukuza mapepo wanaozuia samaki,”

“Kwa ujumla bangi huvuruga mfumo wa kawaida wa akili na hiyo humsababishia mtu kuona au kufanya vitu tofauti na wengine, kitu ambacho ni hatari kwa maisha ya kawaida”anasema Kisenge. 

Kwa mujibu wa tovuti ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA), matumizi ya dawa za kulevya yameendelea kuwa changamoto katika jamii hasa kwa vijana wenye umri kati ya miaka 14 hadi 24.

Matumizi ya dawa za kulevya huchangiwa na sababu mbalimbali zikiwemo za kifamilia, na kijamii ambapo baadhi ya vijana husukumwa na rika na kufuata mkumbo.

Baadhi ya vijana hurubuniwa na kushawishiwa na wenzao wanaotumia dawa hizo na kwamba mara nyingi tatizo hilo huwapata vijana wenye malezi na makuzi duni.

Kadhalika baadhi ya Imani potofu, Mila na desturi za jamii zimekuwa zikitajwa kuchochea matumizi ya dawa za kulevya ikiwemo baadhi yao kuamini kuwa wakitumia bangi hupata nguvu za kufanya kazi zaidi.

 NINI KIFANYIKE

Baadhi ya wadau waliozungumza na makala hii Benedicto Masudi na Gresiana Mathias, wamependekeza baadhi ya mambo yanayopaswa kuzingatiwa ili kuondoa Imani potofu ya matumizi ya bangi katika kundi la baadhi ya wavuvi ikiwa ni pamoja na elimu sahihi kutolewa kwenye mialo inayokusanya wavuvi wengi kabla na baada ya kwenda kuvua samaki.

Serikali ichukue jukumu la kuwaelimisha wavuvi kuwa mafanikio hayapatikani kutumia dawa za kulevya badala yake wajikite kununua zana bora za uvuvi ikiwa ni pamoja na kuweka utaratibu wa kusitisha shughuli za uvuvi angalau miezi mitatu kwa kila mwaka ili kutoa fursa kwa samaki kuzaliana.

Hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi ya wavuvi na watu wote wanaothibitika kujihusisha na matumizi ya bangi kinyume cha sheria za nchi.

Wataalamu wa saikolojia tiba pamoja na madaktari wa afya ya akili wapewe jukumu la kwenda shule za msingi, sekondari, vyuo vya kati na juu kwa lengo kutoa elimu ya madhara ya bangi katika ustawi wa akili na saikolojia.

Jamii isifumbie macho vitendo vya kuuza na kutumia bangi badala yake watoe ushirikiano wa kutoka kwa Mamlaka zenye jukumu la kuzika na kudhibiti dawa za kulevya ikiwemo jeshi la polisi nchini.

“Huu siyo wakati wa kuleana tena maana kwa muda mrefu watu wamekuwa wakitumia bangi kana kwamba ni sigara ya kawaida tu, jambo linalochochea vijana wengi kuingia kwenye mkumbo huo ikiwemo vijana wanaojihusisha na uvuvi wa samaki ndani ya ziwa Viktoria”anahitimisha Masudi.

Related Posts